Alice Guo: Kutoka Meya kipenzi cha watu hadi mshukiwa wa utapeli na Jasusi wa China

 Alice Guo
    • Author, Tony Han
    • Nafasi, BBC Global China Unit
    • Akiripoti kutoka, Bamban and Manila, Philippines
  • Muda wa kusoma: Dakika 8

Katika mapema mwaka wa 2022, wakazi wa mji mdogo wa Bamban, kaskazini mwa Manila nchini Ufilipino, walikusanyika kwa ajili ya mkutano wa kampeni wa mgombea wa umeya, mwanamke kijana mwenye bidii aliyeitwa Alice Leal Guo.

Wafuasi walikuwa wamevaa mavazi ya rangi ya waridi – rangi aliyopenda mgombea wao – wakisubiri kwa hamu kuwasili kwake.

Kisha, sauti ya mzunguko wa helikopta ilisikika angani, na umati ulianza kushangilia. Ndani ya chumba cha marubani, Guo, akiwa amevaa fulana ya waridi na vichwa vya sauti vya marubani, alitabasamu na kuwapungia mkono wafuasi wake.

Helikopta ilipotua, watu walianza kupiga kelele: "A-lice Guo! A-lice Guo!"

Akiwa na umri wa miaka 31, nyota ya Guo ilionekana kung'aa: akiwaahidi wakazi ruzuku kubwa na maendeleo ya kiuchumi kwa sauti yake yenye nguvu na matumaini, aliweza kuvutia wafuasi wengi na hatimaye akawa meya wa kwanza mwanamke wa Bamban.

Lakini wachache kati ya waliomshangilia wangetarajia kuwa chini ya miaka mitatu baadaye, Guo angekuwa gerezani akikabiliwa na mashtaka ya ulanguzi wa binadamu na madai ya kuwa jasusi wa China.

Anguko lake lilianza baada ya uvamizi wa polisi ambao uligundua eneo la utapeli mkubwa lililokuwa nyuma ya ofisi yake. Uchunguzi wa mamlaka ulipozidi, Guo alishindwa kujibu maswali ya msingi kuhusu maisha yake ya awali, jambo lililoleta swali la kushangaza: Alice Guo ni nani hasa?

Meya aliyependwa na watu

Guo alidai kuwa aliingia kwenye siasa akitokea kwenye biashara ya ufugaji wa nguruwe, akisema alikuwa akisimamia shamba la familia yao kwa miaka kadhaa.

Uamuzi wa kuingia kwenye siasa ulitakiwa uwe na mtaji mkubwa na alipoulizwa kuhusu fedha za kampeni yake baadaye, alisema marafiki zake katika sekta ya ufugaji wa nguruwe walimfadhili.

Guo bango
Maelezo ya picha, Nyota ya Guo ilikatishwa baada ya kubainika kwa shughuli za kitapeli zinazoendelea dakika chache kutoka ofisini kwake katika Ukumbi wa Manispaa

Hata hivyo, Guo pia alikuwa na uhusiano na wafanyabiashara matajiri wa Kichina, baadhi yao wakihusishwa na utakatishaji wa fedha haramu na sasa wanakabiliwa na mashtaka ya ulanguzi wa binadamu pamoja naye.

Kampeni yake ilijikita katika haiba yake ya kirafiki. Katika tukio moja, akiwa jukwaani, alisema:

"Kwa timu yetu, kanuni ya kwanza ni: Hakuna madhara! Hakuna madhara yanaruhusiwa, tunapaswa tu kusambaza upendo, upendo, upendo!"

Maneno haya yanaweza kuonekana kuwa ya kejeli sasa, baada ya mamlaka kufichua mambo mengi yaliyokuwa yakifanyika chini ya uongozi wake.

Alipochukua rasmi ofisi mnamo Juni 2022, Guo alileta nguvu mpya na matumaini katika ukumbi wa Manispaa wa Bamban, akiupaka rangi ya waridi na kupamba sehemu ya nje kwa maua.

A

Chanzo cha picha, Rappler/Joann Manabat

Maelezo ya picha, Ukumbi wa Manispaa ya Bamban Municipal Hall unavyoonekana wakati wa utawala wa Guo kama Meya

Mkaazi mmoja, Priscilla May Aban, alisema kuwa alimpigia kura Guo kwa sababu alikuwa mwanamke na aliwasaidia wanawake wengi kupata kazi za usafi.

Wakazi wengine pia walimwona Guo kama kiongozi mwema na mwenye huruma. Baadhi walieleza kuwa alitoa ruzuku kwa wanafunzi na misaada ya kifedha kwa familia maskini.

Mzee mmoja, Francisco Flores, mwenye umri wa miaka 75, alisema kwa hisia:

"Ametusaidia sana maskini hapa Bamban. Aliwaletea watu dawa na alihakikisha mji wetu unaendelea."

Hata hivyo, mwaka mmoja na nusu katika uongozi wake, picha hii nzuri ilianza kubomoka.

Miah

Chanzo cha picha, BBC/Tony Han

Maelezo ya picha, Miah (kushoto) na Francisco (Kulia) wakiwa na moja ya mabango ya kampeni ya umeya ya Alice Guo.

Yaliyojificha nyuma ya Bamban

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Mnamo Februari 2024, polisi wa Ufilipino walipokea taarifa kutoka kwa raia mwema mmoja wa Vietnam aliyekuwa ametoroka kutoka kituo cha kufanyia utapeli la kampuni ya Zun Yuan Technology ndani ya Bamban.

Usiku wa Machi 12, polisi walivamia eneo hilo na kugundua moja ya vituo vikubwa vya utapeli nchini.

"Tulishangazwa," afisa mmoja alisema. "Hii ilikuwa mara ya kwanza kuona eneo la kifahari kiasi hiki kwa ajili ya utapeli."

Ilifichuka kuwa ardhi hiyo ilikuwa awali inamilikiwa na Guo na kwamba kama Meya, alitoa kibali cha biashara kwa Zun Yuan. Kulikuwa bili ya umeme yenye jina lake, ingawa wanasheria wake hawakutoa maoni kujibu maombi ya BBC ya kufanya hiyo.

Uchunguzi zaidi ulibaini kuwa kampuni hiyo ilikuwa inafanya utapeli wa mtandaoni kwa kutumia njia iliyoitwa "pig-butchering", ambapo wahanga huaminishwa kuwekeza fedha zao kwenye biashara feki kwa ahadi ya kupata faida kubwa.

Ndani ya kituo hicho, polisi walikuta zaidi ya watu kutoka 300 wa mataifa tofauti, wengi wao wakiwa wanalazimishwa kufanya kazi za utapeli.

Eneo walilokuwepo wakubwa wa genge la utapeli lilikuwa tofauti kabisa , nyumba za kifahari, bwawa la kuogelea na njia za kutorokea zilizojengwa chini ya ardhi.

Mwishowe, uvamizi huu ulivuta hisia za kitaifa, na Alice Guo akaanza kuchunguzwa zaidi.

A

Chanzo cha picha, BBC/Tony Han

Maelezo ya picha, Jengo kubwa zaidi kwenye eneo hilo linalodaiwa kumilikiwa na Guo lilikuwa na duka la pombe, mgahawa na vilabu vya usiku.

Zun Yuan ilidaiwa kuwa ni kampuni ya kamari au michezo ya bahati nasibu na burudani kupitia mtandaoni, iliyokuwa na leseni ya Ufilipino ya uendeshaji wa michezo ya kubahatisha (Pogo), kibali ambacho hapo awali kiliruhusu taasisi kama hizo kufanya kazi kihalali nchini Ufilipino.

Kuruhusiwa huko kupitia sheria za michezo ya bahati nasibu chini ya Rais wa zamani Rodrigo Duterte mnamo 2017 kulisababisha kuongezeka kwa shughuli za biashara zinazoendeshwa kwa mwamvuli wa leseni za Pogo. Lakini makampuni mengi ya ulaghai pia yalipata leseni za Michezo ya bahati nasibu mtandaoini (Pogo) na kuzitumia kuficha kuficha shughuli zao za uhalifu. PAOCC iliambia BBC walipata ushahidi kwamba Zun Yuan alikuwa akiendesha ulaghai wa "kutapeli" kutoka ofisi yake katika jengo hilo.

Matapeli huchukua muda kujenga imani na waathiriwa kwa kujifanya wapenzi au washirika watarajiwa wa kibiashara, kisha kuwahadaa wawekeze pesa zao katika miradi ya ulaghai, na hapo hutapeliwa.

A

Chanzo cha picha, BBC/Tony Han

Maelezo ya picha, Moja ya daftari ambalo mmoja wa wafanyakazi amerudia maneno ya kichina mara mia

Hii ni mojawapo tu ya njia nyingi ambazo matapeli wa kimtandao hutumia kulaghai mabilioni ya dola ulimwenguni pote. Kwa kawaida huendeshwa na vikundi vya uhalifu vilivyopangwa vyenye uhusiani na wachina katika maeneo ya Kusini Mashariki mwa Asia.

Maeneo haya ama vituo vya aina hii vya utapeli mtandaoni huwa na wafanyakazi mchanganyiko, wale walio tayari kufanya kazi hiyo bila kulazimishwa na wale wanaosafirishwa kutoka maeneo mbalimbali na kulazimishwa kufanya kazi hiyo ya utapeli.

Kwa mujibu wa de la Paz, yeye na wenzake walikuta zaidi ya raia 300 wa kigeni katika jumba la Bamban, wengi wao wakifanya kazi huko kinyume na matakwa yao, walifanya kwa kulazimishwa.

A

Chanzo cha picha, BBC/Tony Han

Maelezo ya picha, Muonekano wa viwanja vya mpira wa kikapu kutoka kwenye moja ya Mabweni
A

Chanzo cha picha, BBC/Tony Han

Maelezo ya picha, Muonekano maridadi wa moja ya majengo ya kifahari

Wakati vikosi vya usalama vinaivamia eneo hili huko Bamban jioni ya tarehe 12 Machi 2024, baadhi ya wakubwa wanaohusishwa na kashfa hii ya utapeli walikuwa tayari wamekimbia kukwepa kukamatwa.

Lakini uvamizi huo uliashiria mabadiliko katika hali ya kisiasa.

Mnamo Juni 2022, Guo alipokuwa anaapishwa kama Meya, muhula wa urais wa Rodrigo Duterte ulikuwa unamalizika.

Mrithi wake, Ferdinand Marcos Jr, hivi karibuni alianza kuchukua hatua kukabiliana na utapeli huu na kupiga marufuku biashara za bahati nasibu za mtandaoni (Pogo), kutokana na kuhusishwa na utapeli. Watu wengi kote katika jamii ya Ufilipino walitahadharisha kuhusu uhalifu huo unaofanyika kwa kificho, au nyuma ya pazia.

Wahusika wakubwa walikuwa Wachina matajiri, ambayo ilisababisha wasiwasi juu ya ushawishi wa kigeni kwani Marcos, alitazama tofauti na mtangulizi wake.

Vikosi vya usalama kuvamia Bamban kulifichua sura mbili za Alice Guo - kiongozi kipenzi cha watu, anayesaidia jamii yake kwa mengi na aliyekuwa na matarajio makubwa kwenye siasa, ni hili la kuhusishwa na kashfa kubwa.

'Binti Msahaulifu'

Mnamo Mei 2024, Guo aliitwa mbele ya Seneti ili kutoa maelezo kuhusu uhusiano wake na genge la utapeli.

Aliwashangaza wengi aliposhindwa kujibu maswali ya msingi kama alipozaliwa, shule aliyosoma na hata jina la mji alikokulia.

Kutokana na majibu yake yasiyoeleweka, mitandao ya kijamii ilimpa jina la utani "Binti msahaulifu".

Katika uchunguzi zaidi, aligunduliwa kuwa alikuja Ufilipino kutoka China akiwa bado mtoto, jina lake halisi likiwa Guo Hua Ping.

Baadhi ya Maseneta walidai kuwa huenda alikuwa jasusi wa China, ingawa hakukuwa na ushahidi wa moja kwa moja kuthibitisha hilo.

Katika hali ya kushangaza, wakati kesi yake ikizungumzwa sana nchini humo, Julai, 2024 Guo alifanikiwa kutorokea kimbilia Indonesia licha ya marufuku ya kutosafiri, lakini baadaye alikamatwa na kurejeshwa Ufilipino.

Aljazeera iliripoti wakati wa kukamatwa kwakwe Indonesia kuwa Guo na washirika wake walijipatia zaidi ya dola $1.8m kutokana na shughuli za uhalifu.

Alice Guo

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Guo alifika mara kadhaa mbele ya Maseneta kuhojiwa kuhusu uhusiano wake na eneo la ulaghai lililokuwepo karibu kabisa na ofisi yake.

Mwezi huo huo wa Julai wachunguzi wa Ufilipino walipiga hatua kubwa ya kumchunguza. Alama za vidole za Guo zilionekana kufanana kabisa na zile za msichana kutoka China aitwaye Guo Hua Ping, ambaye aliwasili Ufilipino pamoja na mama yake, pia Mchina, mapema miaka ya 2000.

Hatua hii ilizua suala lingine la uchunguzi chini ya Seneti, kwamba Guo anaweza kuwa jasusi, anayetumia ushawishi wake na kukusanya taarifa kwa ajili ya China. Suala hilo lilienea haraka miongoni mwa watu waliokuwa wakifuatilia, na limetawala mjadala wa umma wa kesi hiyo.

Jaye Bekema, afisa mkuu wa wafanyakazi wa Risa Hontiveros, mmoja wa Maseneta ambao walichunguza uhusiano unaowezekana kati ya Taasisi ama Kampuni za utapeli na ujasusi wa China, anasema uwezekano kwamba Guo alikuwa jasusi ulihitajika uchunguzi.

"Nadhani kunapaswa kuwa na uwazi kuhusu maana ya jasusi," Bi Bekema alisema, huku akisisitiza kwamba hakuna uthibitisho wa uhakika wa Guo kuwa jasusi.

Tatizo la biashara za bahati nasibu za mtandaoni 'Pogo'

Kwa muda mrefu, kampuni za Pogo zilihalalishwa Ufilipino kama biashara za kamari au bahati nasibu za mtandaoni, lakini zilitumiwa vibaya na magenge ya uhalifu wa kimataifa.

Kesi ya Guo ilisababisha shinikizo kubwa kwa serikali, na hatimaye, Rais Ferdinand Marcos Jr. alitangaza marufuku kamili ya biashara za Pogo (bahati nasibu za mtandaoni) nchini humo. Kwa kuwa nyuma ya pazia kulikuwa na utapeli mkubwa.

Hata hivyo, wachambuzi wanaamini kuwa baadhi ya wanasiasa bado wanafadhiliwa kwa fedha zitokanazo na biashara za 'Pogo', na kwamba polisi wengine wamehusishwa moja kwa moja na magenge ya wahalifu.

A

Chanzo cha picha, BBC/Tony Han

Maelezo ya picha, Mji wa Bamban umepambwa na mabango ya kampeni kwa ajili ya uchaguzi ujao wa Manispaa

Katika mji wa Bamban, hata hivyo, bado kuna watu wanaomkumbuka Guo kwa wema.

Mkaazi mmoja alisema: "Hatujali kama yeye ni Mfilipino au la, kilicho muhimu ni kwamba alitusaidia."

Kwa sasa, Guo anakabiliwa na mashitaka sita tofauti na huenda akahukumiwa kifungo cha miongo kadhaa gerezani.

Hata hivyo, kwa baadhi ya wakazi wa Bamban, kumbukumbu ya meya wao bado inang'aa.