Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Tanzania yatia saini moja ya mikataba mikubwa ya mazingira inayohusisha hifadhi za taifa
Tanzania imetia saini mkataba wa moja ya miradi mikubwa ya upunguzaji wa hewa ya mkaa Afrika Mashariki.
Tanzania, ambayo ina raslimali ya misitu yenye takribani hekta milioni 48, imeibuka kuwa miongoni mwa wahusika wakuu wa Afrika katika biashara ya kimataifa ya kufidia uchafuzi wa mazingira.
Mradi huu unahusisha hifadhi sita za taifa, zenye ukubwa wa hekta milio ni 1.8 (ekari milioni 4.4).
Tangazo hilo linakuja huku viongozi wa dunia wakikutana mjini Dubai kwa ajili ya mkutano wa COP28 unaolenga kutafuta njia za kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.
Miradi ya kukabiliana na uchafuzi wa mazingira: ni kwamba shirika ambalo linachafua mazingira linaweza kulipia mradi wa upanzi wa miti wenye thamani ya tani moja ya hewa ukaa.
Pesa zinazolipwa na shirika zinakusudiwa kwenda kwenye miradi ya kupunguza hewa ukaa, kwa hiyo kwa kila tani ya hewa ukaa iliyotolewa, mradi huo unawakilisha tani ya hewa ukaa ambayo ilinaswa.
Kwa njia hii, kiasi cha jumla cha hewa ukaana uchafuzi mwingine unaozalishwa unatakiwa kukaa sawa, au hata kupunguzwa.
Mkataba huo mpya ni muungano kati ya mamlaka ya hifadhi za taifa nchini Tanzania, Tanapa, na kampuni ya Carbon Tanzania, nchini humo.
Baadhi ya mapato kutokana na mradi wa fidia juu ya uchafuzj wa mazingira yataenda kwa Tanapa na jamii za mitaa, Carbon Tanzania ilisema Alhamisi.
Kando na kuwezesha biashara ya kaboni, mradi huo pia "utazingatia ulinzi, uhifadhi, na usimamizi ulioimarishwa wa maeneo haya ya hifadhi ya taifa, kulinda mazingira yao ya asili na rasilimali muhimu za wanyamapori", kampuni hiyo iliongeza.
Hifadhi sita za taifa zilizotengwa kwa ajili ya mradi huo ni Burigi-Chato, Uwanda wa Katavi, Mto Ugalla, Mkomazi, Mkondo wa Gombe na Milima ya Mahale.
Mradi huo utapokea ufadhili wa ziada kutoka kwa Mohammed Enterprises Tanzania Limited, kampuni ya kilimo na utengenezaji inayomilikiwa na mfanyabiashara maarufu kutoka Tanzania, Mohammed Dewji.
Mwezi Februari, Tanzania iliingia makubaliano ya awali ya mkataba mkubwa zaidi wa kaboni, unaojumuisha hekta milioni 8.1, karibu 8% ya ardhi yote ya Tanzania.
Makubaliano ya Februari yaliwekwa na Blue Carbon, kampuni ya UAE ambayo inasema inatoa suluhu za asili na miradi ya kuondoa kaboni kwa kutumia mbinu za kisasa.
Katika miaka ya hivi karibuni, kumekuwa na ongezeko la makampuni ya kukabiliana na kaboni yanayochukua udhibiti wa ardhi katika Afrika ya Jangwa la Sahara kwa ajili ya miradi ya miaka mingi ya kaboni, ambayo baadhi ya wakosoaji wanasema ni aina ya ukoloni mamboleo.
Blue Carbon imekuwa ikikosolewa haswa na wanamazingira.
Kampuni hiyo inasema miradi yake inafanywa chini ya udhibiti mkali na kunufaisha jamii. Pia inasema kuwa nchi hushirikiana nayo kwa hiari.
Kampuni hiyo ya Emirati pia imetia saini Mkataba wa Maelewano (MoUs) unaohusiana na kaboni na nchi nyingine za Afrika, ikiwa ni pamoja na Liberia, Kenya, Zambia na Angola.
Ukikamilika, mapendekezo haya yanaweza kutoa mikataba ya kutoa udhibiti wa Kaboni ya Bluu ya maeneo makubwa ya ardhi katika nchi hizi kwa ajili ya matumizi ya uzalishaji wa kaboni.
Imetafsiriwa na Seif Abdalla