El Dorado: Jiji la dhahabu lililopotea linalosubiri kugunduliwa na watu jasiri

Chanzo cha picha, Getty Images
Tamaa ya dhahabu imeenea enzi zote, kwa watu wa rangi na mataifa tofauti. Kuwa na kiasi chochote cha dhahabu inaonekana kuwa ni utajiri na huwapa hamu watu hao isiyoshibishwa ya kupata zaidi.
Kwa karne nyingi, shauku hii ilileta hadithi ya kudumu ya jiji la dhahabu. Katika karne ya 16 na 17, Wazungu waliamini kwamba mahali fulani katika Ulimwengu Mpya kulikuwa na mahali pa utajiri mwingi unaojulikana kama El Dorado.
Utafutaji wao wa hazina hii ulipoteza maisha mengi, ulisababisha angalau mtu mmoja kujiua, na kumweka mtu mwingine chini ya shoka la mnyongaji.
"El Dorado ilihamisha maeneo ya kijiografia hadi hatimaye ikamaanisha tu chanzo cha utajiri usioelezeka mahali fulani Huko Marekani," anasema Jim Griffith, mtaalamu wa simulizi za kale huko Tucson, Arizona.
Lakini mahali hapo pa utajiri usiopimika hakujapatikana.
Chanzo cha jiji la dhahabu

Chanzo cha picha, Getty Images
Asili ya El Dorado iko katika eneo la Marekani Kusini. Na kama hadithi zote za kudumu, hadithi ya El Dorado ina baadhi ya ukweli ndani yake. Wavumbuzi Wahispania walipofika Amerika Kusini mapema katika karne ya 16, walisikia hadithi kuhusu kabila la wenyeji walio juu kwenye milima ya Andes katika eneo ambalo sasa linaitwa Colombia. Wakati chifu mpya alipoingia madarakani, utawala wake ulianza na sherehe katika Ziwa Guatavita. Hesabu za sherehe hiyo zinatofautiana, lakini mara kwa mara wanasema mtawala mpya alifunikwa na vumbi la dhahabu, na kwamba dhahabu na vito vya thamani vilitupwa ndani ya ziwa ili kumfurahisha mungu aliyeishi chini ya maji.
Wahispania walianza kumwita chifu huyu wa dhahabu El Dorado, "aliyepambwa kwa dhahabu." Sherehe ya mwanamume aliyevalia mavazi ya dhahabu inasemekana ilimalizika mwishoni mwa karne ya 15 wakati El Dorado na raia wake walishindwa na kabila lingine. Lakini Wahispania na Wazungu wengine walikuwa wamepata dhahabu nyingi sana miongoni mwa wenyeji kando ya pwani ya kaskazini ya bara hilo hivi kwamba waliamini kuwa ni lazima kuwe na mahali penye utajiri mkubwa mahali fulani ndani.
Wahispania hawakupata jiji la El Dorado, lakini badala yake walipata Ziwa Guatavita na wakajaribu kulitoa maji mnamo 1545. Walishusha kiwango chake vya kutosha kupata mamia ya vipande vya dhahabu kando ya ziwa hilo. Lakini hazina iliyodhaniwa kuwa ya ajabu katika maji ya kina zaidi ilikuwa nje ya uwezo wao na hawakuweza kufika.

Chanzo cha picha, Getty Images
Jitihada za Raleigh
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Mfanyakazi Mwingereza na mvumbuzi Sir Walter Raleigh alifunga safari mbili hadi Guiana kutafuta jiji la El Dorado. Wakati wa safari yake ya pili mnamo 1617, alimtuma mwanawe, Watt Raleigh, pamoja na msafara hadi Mto Orinoco. Lakini Walter Raleigh, ambaye wakati huo alikuwa mzee, alibaki kwenye kambi moja kwenye kisiwa cha Trinidad. Msafara huo ulikuwa ndio mwisho wa mtoto wake, Watt Raleigh aliuawa katika vita na Wahispania.
Eric Klingelhofer, mwanaakiolojia katika Chuo Kikuu cha Mercer huko Macon, Georgia, anajaribu kutafuta kambi ya msingi ya Raleigh huko Trinidad. Anasema Walter Raleigh alikasirishwa na manusura ambaye alimwarifu kuhusu kifo cha Watt na kumshutumu aliyenusurika kwa kuruhusu mwanawe auawe. "Mtu huyo aliingia kwenye kibanda chake kwenye meli na kujiua," anasema Klingelhofer.
Raleigh alirudi Uingereza, ambapo Mfalme James aliamuru akatwe kichwa kwa, pamoja na mambo mengine, kutotii amri ili kuepusha mzozo na Wahispania.
Hadithi ya El Dorado inastahimili kwa sababu "unataka iwe kweli," anasema Jose Oliver, mhadhiri katika Taasisi ya Akiolojia katika Chuo Kikuu cha London. "Sidhani kama tumeacha kuitafuta El Dorado."
Kwa hivyo jiji hili la dhahabu lililopotea liko wapi? Katika shairi lake la 1849 "El Dorado," mwandishi Edgar Allan Poe anatoa pendekezo la kutisha na fasaha: "Juu ya Milima ya Mwezi, chini ya Bonde la Kivuli, panda, panda kwa ujasiri ... ikiwa unatafuta El Dorado."

Chanzo cha picha, Getty Images
Jinsi hadithi hii ilivyokua hadi kuwa hekaya ya jiji la dhahabu inaonyesha njia tofauti ambayo dhahabu ilikuwa chanzo cha utajiri wa nyenzo kwa watawala wa Uropa. Walikuwa na uelewa mdogo wa thamani yake ya kweli ndani ya jamii ya Muisca. Akili za Wazungu zilishangazwa tu na ni kiasi gani cha dhahabu lazima kilitupwa kwenye kina kirefu cha maji ya ziwa na kuzikwa kwenye maeneo mengine matakatifu karibu na Colombia.
Mnamo AD1537 ilikuwa ni hadithi hizi za El Dorado ambazo zilimvuta mtawala wa Kihispania Jimenez de Quesada na jeshi lake la watu 800 mbali na misheni yao ya kutafuta njia ya nchi kavu kuelekea Peru na hadi katika nchi ya Andean ya Muisca kwa mara ya kwanza.
Quesada na watu wake walivutwa zaidi katika maeneo ya kigeni na yasiyo na ukarimu ambapo wengi walipoteza maisha yao. Lakini kile Quesada na watu wake walikipata kiliwashangaza, kwa kuwa utengenezaji wa dhahabu wa Muisca ulikuwa kama kitu ambacho hawakuwahi kuona hapo awali. Vitu vya dhahabu vilivyoundwa kwa ustadi vilitumia mbinu zaidi ya kitu chochote kilichowahi kuonekana na macho ya Uropa.
Cha kusikitisha, uwindaji wa dhahabu bado uko hai sana. Wanaakiolojia, wanaofanya kazi katika taasisi za utafiti kama vile Museo del Oro huko Bogota, wanapambana dhidi ya wimbi linaloongezeka la uporaji. Kwa hivyo kama vile watawala wa Uropa wa Karne ya 16, wenzao wa kisasa wanaendelea kuharibu thamani za Amerika Kusini na kutuibia hadithi za kuvutia nyuma yake.
Kiasi cha dhahabu kilichofichuliwa na waporaji hao bado kinashangaza. Katika miaka ya 1970 maeneo mapya yalipogunduliwa na waporaji kaskazini mwa Colombia ilisababisha soko la dhahabu la dunia kuanguka.
Uporaji huu wa dhahabu uliochochewa na kisa cha jiji la El Dorado umemaanisha kwamba sehemu kubwa ya vitu vya thamani vya kabla ya Columbia vimeyeyushwa na thamani halisi ya vitu hivi vya sanaa kama viashiria vya utendakazi wa utamaduni wa kale vimepotea milele.
Kwa bahati nzuri, vitu vilivyohifadhiwa baada ya kukusanywa katika Jumba la Makumbusho del Oro huko Bogota na Makumbusho ya Uingereza huko London vinaweza kutoa ufahamu katika mitazamo hii tofauti juu ya thamani ya nyenzo na mtazamo wa kibinadamu na muhimu zaidi kusimulia hadithi ya kweli nyuma ya hadithi za El Dorado.
Imetafsiriwa na Munira Hussein na kuhaririwa na Ambia Hirsi












