Harakati za China kuikonga mioyo ya Waafrika kupitia TV ya satelaiti

Wakati viongozi wa Afrika wakikusanyika mjini Beijing wiki hii kwa ajili ya mkutano wa kilele wa miaka mitatu kati ya China na Afrika, Rais wa China Xi Jinping anaweza kuwa na jambo la kujivunia - TV ya satelaiti.
Takriban miaka tisa iliyopita, Rais Xi aliwaahidi wakuu wa nchi waliohudhuria Kongamano la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) mjini Johannesburg kwamba China itatoa huduma ya televisheni ya kidijitali kwa zaidi ya vijiji 10,000 vilivyopo mbali katika nchi 23 za Afrika .Na sasa zaidi ya vijiji 9,600 vimepokea miundombinu ya satelaiti, hivyo mradi huo unakaribia kukamilika.
Jukumu la utekelezwaji wa ahadi hiyo kabambe, iliyotangazwa wakati wa uhusiano mwema kati ya China na Afrika na kufadhiliwa na bajeti ya misaada ya China, ilipewa StarTimes, kampuni ya kibinafsi ya China ambayo tayari inafanya kazi katika nchi kadhaa za Afrika.
Hii ilionyesha dhahiri la nia njema na fursa kwa China kubadilisha nguvu yake katika eneo muhimu la kimkakati.
Huku uchumi wa China ukitatizika na Beijing kurekebisha tena mkakati wake wa Afrika, BBC ilitembelea vijiji vinne nchini Kenya ili kujua kama mpango huu wa huu unaofahamika kama "soft power" umezaa matunda.
Katika kijiji cha Olasiti, mwendo wa saa tatu kwa gari kuelekea magharibi mwa mji mkuu, Nairobi, Nicholas Nguku alikusanya marafiki na familia yake kutazama wanariadha wa Kenya wakikimbia kwenye Michezo ya Olimpiki ya Paris kwenye televisheni.
"Nimefurahi sana kuona michezo ya Olimpiki, ambayo kwa miaka mingi tulikuwa hatujaweza kuiona kabla ya kupata StarTimes," alisema, akizungumzia uwekaji wa vyombo vya satelaiti wa kampuni hiyo takriban miaka minne iliyopita.

Nicholas Nguku sio mtu pekee aliyenufaika na uwepo wa StarTimes barani Afrika.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kampuni hiyo ambayo ilianzishwa kwa mara ya kwanza barani mwaka 2008, sasa ni mojawapo ya watoa huduma wakubwa wa televisheni za kidijitali katika Kusini mwa Jangwa la Sahara barani Afrika, ikiwa na wateja zaidi ya milioni 16.
Wachambuzi wanasema kwamba bei ya chini ya huduma zake hapo awali ilisaidia kupata mafanikio yake.
Nchini Kenya, vifurushi vya huduma ya televisheni vya kidijitali vya kila mwezi ni kati ya shilingi 329 ($2.50; £2) hadi shilingi 1,799 ($14; £10.50).
Ukilinganisha na , kifurushi cha mwezi cha DStv, kinachomilikiwa na MultiChoice, ambayo pia ina soko la TV za kidijitali Afrika, kinagharimu kati ya shilingi 700 na 10,500.
Wakati StarTimes kwa kiasi fulani inategemea usajili kwa mapato yake ya msingi, "Mradi wa Vijiji 10,000" unafadhiliwa na Hazina ya Usaidizi ya serikali ya South-South Assistance Fund.
Dishi za satelaiti zote zina nembo ya StarTimes, nembo ya Wizara ya Habari ya Kenya, na nembo nyekundu ya Msaada wa China “China Aid”.
Wakati wa usimikaji wa dishi hizi, wawakilishi wa StarTimes walisema kwamba hii ilikuwa "zawadi" kutoka Uchina, wanakijiji kadhaa walikumbuka.

Kwa mujibu wa Dk Angela Lewis, msomi ambaye ameandika kwa kina Makala kuhusu StarTimes barani Afrika, mradi huo umekuwa na uwezo wa kuacha taswira nzuri ya China kwa watazamaji wa Afrika.
Wanakijiji chini ya mradi huo walipokea kila kitu bila malipo, ikiwa ni pamoja na miundombinu, kama vile dishi la satelaiti, betri, pamoja na usajili wa maudhui ya StarTimes.
Hili lilileta "mabadiliko ," kulingana na Dk Lewis, kwani vijiji vya mbali barani Afrika hapo awai vilikuwa na uwezo wa kufikia TV ya analojia isiyoaminika na isiyotegemewa.
Kwa wengi, ilikuwa ni mara ya kwanza kupata vyombo vya satelaiti, na kubadilisha jinsi wanakijiji walivyoingiliana na ulimwengu wa nje, alisema.
Kwa vituo vya jamii kama vile hospitali na shule katika kijiji cha Ainomoi magharibi mwa Kenya, usajili unafanyika bila malipo.
Katika kliniki ya eneo TV ya dijiti kwenye chumba cha kusubiri matibabu huwasaidia wagonjwa kukupoteza wakati. Na katika shule ya msingi, wanafunzi hufurahia kutazama katuni baada ya shule.
"Baada ya kumaliza kazi ya shule, sote tutatazama katuni pamoja na ni tukio la kufurahisha na la kuunganisha," alisema Ruth Chelang'at, mwanafunzi wa darasa la nane katika shule hiyo.
Hata hivyo, kaya kadhaa za Kenya zilizohojiwa na BBC zinasema kuwa kifurushi cha huduma ya setilaiti cha kilidumu kwa muda mfupi tu.
Licha ya bei yake nafuu, kununua tena usajili kulionekana kuwa mzigo mkubwa wa kifedha kwa wengi.
Pamoja na hayo, msisimko wa awali umepungua miongoni mwa baadhi ya wanufaikaji wa mradi huo, na kuweka doa katika msukumo wa China wa kujenga nia njema.
"Sote tulifurahi sana tulipopata dishi ya satelaiti kwa mara ya kwanza, lakini ilikuwa bila malipo kwa miezi michache tu, na baada ya hapo tulilazimika kulipa," alisema Rose Chepkemoi, kutoka kijiji cha Chemori kaunti ya Kericho. "Ilikuwa ni pesa nyingi kwa hivyo tuliacha kuitumia."

Bila usajili, ni chaneli fulani tu za zinaweza kupatikana , kama vile Matangazo ya Shirika la utangazaji la Kenya, ndizo zinazopatikana, kulingana na wale ambao hawakununua tena vifurushi vya StarTimes.
Wakati wa ziara ya BBC katika vijiji vinne tofauti vilivyopokea dishi za StarTimes kuanzia 2018 hadi 2020, wanakijiji wengi waliripoti kuacha kutumia StarTimes baada ya jaribio la bila malipo kuisha. Chifu wa kijiji cha Ainamoi alisema kuwa kaya nyingi kati ya 25 za awali zilizopokea vifaa vya satelaiti katika kijiji chake zilichagua kutojisajiri.
BBC iliwasiliana na StarTimes kwa maoni kuhusu majaribio hayo ya bila malipo lakini haikupokea jibu.
Ushawishi wa China unaenea hadi kwenye maudhui yanayotangazwa kwenye chaneli za StarTimes, na kuwa na matokeo mchanganyiko.
Hata vifurushi vya bei nafuu zaidi ni pamoja na chaneli kama Kung Fu na Sino Drama, inayoonyesha filamu na vipindi vya tamthilia za Kichina.
Mnamo mwaka wa 2023, zaidi ya filamu 1,000 za Kichina na vipindi vya televisheni vilitafsiriwa kwa lugha za kienyeji, Ma Shaoyong, mkuu wa uhusiano wa umma wa StarTimes, aliviambia vyombo vya habari vya ndani.
Kwa upande wa Kenya, mwaka wa 2014, kampuni hiyo ilizindua chaneli iitwayo ST Swahili, inayotoa maudhui ya Kiswahili.
Miongoni mwa wanavijiji ambao wametazama maonyesho ya Kichina, wengi walisema walipata programu kuwa ya kizamani, inayoonyesha herufi za Kichina, huku vipindi mara nyingi vikiwa na mada zisizo za kawaida.
Vipindi vingi vinahusu suala la uchumba au mapenzi, ikiwa ni pamoja na kipindi maarufu cha maisha halisi kiitwacho Hello, Mr. Right, ambapo washindani hutafuta kupata mtu anayelingana naye kikamilifu.
Maudhui hayo yaliigizwa kutokana na yale yanayotolewa nchini Uchina katika kipindi kiitwacho If You Are the One.
Kwa baadhi angalau, maudhui hayo ni sababu ya kuendelea na usajili. Ariana Nation Ngotiek, mwenye umri wa miaka 21 kutoka kijiji cha Olasiti, "amevutiwa sana" na maonyesho fulani, kama vile msururu wa tamthilia ya Kichina unaohusu mapenzi, Eternal Love, ambao unaitwa sasa umepewa jina la Kiingereza. “I won’t go to sleep without watching it,” (Sitalala bila kuitazama), alisema.
Kandanda ndio kivutio halisi cha watu
Lakini mpira wa miguu unasalia kuwa kivutio kikuu kwa watazamaji wa Kiafrika.
Mnamo mwaka 2023, kwa mfano, Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) lilikuwa na idadi ya watazamaji karibu bilioni mbili ulimwenguni, kulingana na Shirikisho la Soka la Afrika.
Kwa kufahamu fursa hii ya kibiashara, StarTimes imewekeza pakubwa katika kupata haki za utangazaji kwa mechi za soka, zikiwemo Afcon, La Liga ya Uhispania na Bundesliga ya Ujerumani.
Katika "Utangazaji wa michezo ndio StarTimes ilitengeneza jina," alieleza Dk Lewis.
Ushindani ni mkali, hata hivyo, na SuperSport, kampuni tanzu ya MultiChoice, inaripotiwa kulipa zaidi ya $200m (£152m) kila mwaka kwa haki za kutangaza Ligi Kuu ya Uingereza inayopendwa.
Baada ya gwiji wa soka wa Ufaransa, Kylian Mbappé kutangaza kujiunga na Real Madrid ya Uhispania, StarTimes ilichukua fursa hiyo na kutengeneza mabango makubwa jijini Nairobi yaliyosomeka “Feel the full thrill of La Liga”, ikifuatiwa na nembo ya StarTimes.
Lakini , hii haikumsisimua kila mtu.
Shabiki mmoja wa kandanda aliambia BBC kwamba "angependa kufurahia msisimko wa Ligi Kuu."
"Wengi wa Wakenya hawako kwenye La Liga, ni Ligi Kuu ya Uingereza inayovutia watazamaji," alielezea Levi Obonyo, profesa katika Chuo Kikuu cha Daystar cha Nairobi.

Ingawa shirika la utangazaji la taifa la China CGTN linalotazamwa kimataifa, limejumuishwa katika kifurushi chake cha bei nafuu, tofauti na BBC na CNN, haliwavutii watazamaji.
"Ndiyo, pia tuna habari za Uchina, lakini sizitazama," alisema Lily Ruto, mwalimu mstaafu katika kaunti ya Kericho. “Inaitwaje tena? C kitu N? Kuna kitu N?" alicheka huku akiinua mabega yake.
Dk Dani Madrid-Morales, mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Sheffield, anakariri kwamba StarTimes haijaleta mapinduzi katika mazingira ya habari [ya Kiafrika].
Wanakijiji wengi wanasema wanapendelea habari za ndani. StarTimes wanaelewa hilo.
Huku zaidi ya 95% ya wafanyakazi wake 5,000 ni wa Kiafrika, kwa mujibu wa msemaji wa kampuni hiyo, StarTimes inalenga kujionyesha kuwa inazipa kipaumbele sauti za Kiafrika.
Mshauri mmoja wa kampuni za vyombo vya habari za China barani Afrika alisema kuwa StarTimes ilikuwa ikijaribu kuzuia kurudia kwa kile kilichotokea kwa kampuni kama TikTok au Huawei, ambao maudhui yao ya wazi ya kichina yamevutia uchunguzi wa hali ya juu kutoka nchi za Magharibi.
Utafiti wa Dk Lewis kuhusu habari za mwaka 2015 hadi 2019 unathibitisha hilo, akibainisha kwamba habari nyingi zinazotolewa na StarTimes hazirejelei uhusiano wa China au China na Afrika. Kampuni inaonekana kuwa makini isionyeshe waziwazi asili yake ya Uchina.
Kutoka mazungumzo ya mjini hadi kuacha alama
StarTimes kama kampuni binafsi imepata mafanikio makubwa kwa miaka mingi, na "Mradi wa Vijiji 10,000" umeifanya kampuni hiyo kufikia kiwango kipya cha umaarufu.
Lakini, wakati Beijing inaandaa FOCAC nyingine, athari ya ujenzi wa picha ya mradi ambayo China ilitarajiwa kuuukamisha umeshindwa kutekelezwa.
"Kulikuwa na jaribio la serikali kusawazisha mtiririko wa habari ambao ungeiweka China chini ya mwanga mzuri, lakini hilo halijatimia," alisema Dk Madrid-Morales. "Kiasi cha pesa ambacho kimeingia katika hili hakijaifaidi sana serikali ya China."
Wanavijiji wengi ambao BBC ilizungumza nao walikuwa na wasiwasi zaidi kuhusu maudhui na gharama. Mradi huo, ambao mara moja ulikuwa gumzo la jiji hilo, umeonekana kuachwa kwa maelezo ya chini katika ufikivu wa umeme laini wa China.
"Ndiyo, tunajua inatoka Uchina, lakini haileti tofauti ikiwa hakuna anayeitumia," alisema Bi Chepkemoi, ambaye ameghairi usajili wake wa StarTimes.














