Kenya ilivyokumbwa na misukosuko ya kisiasa 2024

Vijana

Chanzo cha picha, Getty Images

Muda wa kusoma: Dakika 4

Kipindi cha baada ya uchaguzi wa Agosti 8, 2022 hadi 2024 kimekumbwa na hali ya wananchi kutoridhishwa na serikali ya Rais William Ruto.

Matatizo ya kiuchumi, yaliyochochewa na mfumko mkubwa wa bei, kupanda kwa deni la umma, ufujaji wa fedha za umma, na ukosefu mkubwa wa ajira, yalizidisha manung'uniko ya wananchi.

Kushindwa kwa serikali kutatua changamoto hizi kulichochea maandamano na machafuko ya kiraia, huku wanasiasa wa upinzani wakitumia vyema hali hiyo kuwahamasisha wafuasi wao kupinga mkakati mpya wa ukusanyaji kodi ulioanzishwa mwaka wa 2023, ili kushinikiza "suluhisho la kisiasa" kati ya mirengo miwili mikuu ya kisiasa.

Tunapoelekea kuupungia mkono mwaka 2024 tunaangazia masuala yaliyogonga vicha vya habari.

Mswada wa Fedha 2024

Mnamo Mei 2024, Serikali ya Kenya iliwasilisha Mswada wa Fedha wa 2024. Kile ambacho kilionekana kama utaratibu wa 'kawaida' uliofanywa na tawala zilizopita na za sasa kuelezea mapendekezo na marekebisho mbalimbali ya kodi yaliyolenga kuongeza mapato ya serikali, kiilizua mjadala mkubwa wa umma na kutoridhika na jinsi serikali inavyoshughulikia. masuala ya kiuchumi, ukosefu wa ajira, rushwa, na maswali ya jumla juu ya uwajibikaji, uwazi, na utajiri unaoonyeshwa na viongozi wakuu wa kisiasa bila kujali idadi mahangaiko ya kubwa ya watu wa kipato cha chini.

Kipindi kilichofuata kuanzishwa kwa Muswada wa Sheria ya Fedha wa 2024 kilikumbwa na machafuko makubwa ya wenyewe kwa wenyewe, yaliyochangiwa na malalamiko ya kina ya kisiasa na kiuchumi.

Kipindi hicho cha machafuko kilifichua mipasuko ya muda mrefu katika mfumo wa kisiasa na kijamii wa nchi, na kuibua wasiwasi juu ya utulivu wa kisiasa wa taifa hilo.

Maandamno ya Gen Z

Maelfu ya waandamanaji ambao wengi wao walikuwa vijana, waliojitambulisha kama Generation Z, waliingia mitaani kupinga Mswada tata wa Fedha wa 2024, lakini baadaye mswada huo ulipotupiliwa mbali wakapanua malengo yao ya kutaka serikali kushughulikia ukosefu wa usawa, ufisadi na siasa.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Machafuko yaliyozuka Juni 2024 yalichangiwa na sababu nyingi, ikiwa ni pamoja na kutoridhika na jinsi serikali inavyoshughulikia masuala ya kiuchumi, hasa mfumuko wa bei na viwango vya juu vya ukosefu wa ajira.

Zaidi ya hayo, kupanda kwa gharama ya maisha, kukichochewa na changamoto za kiuchumi duniani na usimamizi mbaya wa ndani ambao uliathiri sana watu wa kipato cha kati na cha chini.

Madai ya ufisadi na kushindwa kwa utawala kushughulikia masuala yaliyibuliwa yalizidisha kero la wananchi dhidi ya serikali.

Waandamanaji walio kuwa na hamaki walivamia Bunge la kitaifa mnamo Juni 25 katika hatua iliyozua ghasia kubwa huku waandamanaji wakichoma magari mbele ya Mahakama ya Juu na kuchoma afisi ya Gavana wa Kaunti ya Nairobi.

Maandamano hayo pia yaliweka wazi suala la maafisa wa usalama kutumia nguvu kupita kiasi katika kukabiliana na vurugu.

Katika matukio tofauti polisi wa Kenya walifyatua risasi za moto kutawanya umati huo, kuua waandamanaji na kuwajeruhi mamia ya wengine.

Machafuko ya Juni 2024 yalitishia uthabiti wa serikali ya Rais William Ruto, na kumlazimu kufanya mabadiliko makubwa katika serikali yake ili kukabiliana na shinikizo kubwa kutoka kwa umma.

Rais Ruto alifanya mabadiliko ya kimkakati yaliyolenga kuleta utulivu wa serikali yake katika juhudi za kukabiliana na mzozo huo.

Alivunja Baraza lake la Mawaziri na baadaye kuunda tena serikali kwa kushirikisha chama cha upinzani cha Orange Democratic Movement maarufu ODM, kuwateua baadhi ya viongozi wake kushikilia nyadhifa muhimu za kimkakati serekalini.

Kuondolewa madarakani kwa Gachagua

Rigathi Gachagua

Chanzo cha picha, EPA

Mara baada ya maandamano ya vijana kufifia Wabunge walianzisha mchakato usio na kifani ambao ulikamilishwa na kuondolewa madarakani kwa Naibu wa Rais wa Kenya wakati huo Rigathi Gachagua.

Baadaye, Rais William Ruto alimteua Waziri wa Mambo ya Ndani Kithure Kindiki kama Naibu Rais mpya na Bunge la kitaifa likapiga kura kuunga mkono uteuzi wake.

Bw, Kindiki aliapishwa baada ya makabiliano ya kisheria kati ya mawakili wa Gachagua na wale wa upande wa serikali mahakamani.

Rigathi Gachagua aling'olewa madarakani kutokana na kile kilichosadikiwa kuwa utumizi mbaya ya mamlaka, ufisadi, kuhujumu idara ya ujasusi na mahakama, kukiuka katiba na kuchochea siasa za ukabila. Soma zaidi: Je, hiki ndicho kilichomponza Gachagua?

xx

Gachagua hata hivyo alisisitiza kuwa alitimuliwa kwa kuwatetea Wakenya dhidi ya ukandamizaji wa serikali ya Kenya Kwanza.

''Walinishtaki kwa sababu nilipinga ukandamizaji wa Wakenya. Ikiwa hilo lilikuwa kosa langu, ninakubali. Tulikuwa tumewaahidi Wakenya kwamba hakuna mtu ambaye angefurushwa kwa lazima bila kulipwa fidia ya haki,''alisema hivi maajuzi katika mahojiano na runinga ya NTV.

Naibu rais huyo aliyetimuliwa alieleza moja ya mashtaka yaliyotolewa dhidi yake wakati wa hoja ya kuondolewa kwake madarakani ni kupinga serikali kubomoa nyumba za watu.

Gachagua aidha aliongeza kusema sasa anaelewa ni kwa nini rais wa zamani Uhuru Kenyatta alikataa kumuunga mkono Dkt Ruto (ambaye alikuwa naibu wa Kenyatta tangu 2013) katika kinyang'anyiro cha urais mwaka wa 2022.

Gachagua alitofautiana na Bw Kenyatta na kuongoza timu ya wanasiasa Mlima Kenya kumuunga mkono Dkt Ruto, aliteuliwa kuwa mgombea mwenza na kusaidia Ruto kuzoa asilimia 87 ya kura za eneo hilo.

Lakini baada ya Gachagua kumtumikia Dkt Ruto kama naibu rais kwa miaka miwili, alitimuliwa Oktoba 17, 2024 na nafasi yake ikachukuliwa na Prof Kithure Kindiki.

Sasa, Bw Gachagua anasema hajuti kumuunga mkono Dkt Ruto kwa kile anadai alipata funzo, japo linaumiza.