Familia ya Mahsa Amini yapokea vitisho vya mauaji

Familia ya Mahsa Amini - mwanamke wa Kikurdi mwenye umri wa miaka 22 ambaye kifo chake akiwa mikononi mwa polisi wiki tatu zilizopita kilizua maandamano nchini Iran - wanasema wamepokea vitisho vya kuuawa na wameonywa kutojihusisha na maandamano hayo.

Mahsa alikua ishara ya ukandamizaji wa Wairan baada ya kukamatwa na polisi wa maadili, ambao walimshtaki kwa kuvaa hijabu yake isivyofaa.

Uso wake, na matukio yaliyosababisha kifo chake, sasa yanajulikana kote duniani.

"Familia yetu imekuwa chini ya shinikizo kubwa kutoka kwa maafisa wa Jamhuri ya Kiislamu, kwa hivyo hatuzungumzi na mashirika ya kuteea haki za binadamu nje ya Iran na kumjulisha mtu yeyote kutoka ulimwengu wa nje juu ya kifo chake," binamu yake Erfan Mortezai alimwambia mwandishi wa BBC walipokutana akikuvuka mpaka katika Mkoa wa Kurdistan wa Iraq.

Erfan ni mpiganaji wa Peshmerga wa Komala, chama cha upinzani cha Kikurdi kilicho uhamishoni nchini Iraq. Kwa miaka mingi, tangu muda mrefu kabla ya kifo cha Mahsa, amekuwa akijaribu kuiangusha Jamhuri ya Kiislamu.

Serikali ya Iran imelaumu machafuko ya hivi punde zaidi juu ya ushawishi kama huo kutoka nje.

Familia ya Mahsa Amini nchini Iran, akiwemo babake na mjombake, wamekanusha mara kwa mara kuunga mkono makundi ya upinzani ya Wakurdi, ambayo Iran inashutumu kwa kutaka kujitenga.

Tunapozungumza kwenye kivuli cha milima, anatumia jina lake la Kikurdi - Zhina - ambalo marafiki zake na familia walimwita kila siku.

Mahsa ni jina lake rasmi la Kiirani, ambalo wazazi wake walilazimika kulitumia kwenye nyaraka kwa sababu baadhi ya majina ya Kikurdi yamepigwa marufuku nchini Iran.

"Zhina alikuwa mtu wa kawaida, hakuwa wa kisiasa," Erfan anasisitiza.

"Utawala umekuwa ukitengeneza matukio na taarifa potofu - ukisema kwamba Zhina alikuwa akiwasiliana nami na nilimfundisha na kumrudisha Iran kufanya shughuli fulani, wakati ukweli huu hauna msingi kabisa."

Anasema vitisho ambavyo wanafamilia wake wamepokea vimewafanya kutilia shaka usalama wao.

"Wako chini ya mateso ya Jamhuri ya Kiislamu," aalimwambia mwandishi wetu.

"Maafisa wa serikali wametutishia kupitia Instagram kwa akaunti feki, na kuwaambia wanafamilia nchini Iran kwamba ikiwa watahusika katika maandamano, wanaweza kuuawa."

"Mimi mwenyewe, nimekuwa nikipokea vitisho vingi kupitia simu, [ vikisema] kwamba wakiniona mjini, wataniteka nyara na kuniua."

Erfan alishiriki nami video ambazo hazijaonekana hapo awali na zinaonyesha utofauti wa kuhuzunisha.

Ya kwanza ni Mahsa akicheza dansi kwenye arusi, akipunga shela za rangi na kutazama kamera kwa haya.

Ya pili inaonyesha familia yake ikiwa imekusanyika kwenye kaburi, kuashiria siku yake ya kuzaliwa ya 23.

Keki iliyopambwa kwa uso wake imewekwa kwa uangalifu kwenye kaburi lake.

Kuna kelele za hasira na machozi mengi.

Nilisafiri hadi kwenye mpaka wa milimani kati ya Iran na Iraq, ambako kuna barabara zenye vumbi na miinuko na wakulima wanapanda punda wakichunga ng'ombe wao.

Hapa ni moja wapo ya maeneo machache unaweza kusikia hadithi moja kwa moja kutoka kwa Wairani.

Ninakutana na familia ambayo imetoka Sanandaj, magharibi mwa Iran, iliyopakiwa kwenye basi dogo. Wanasema wameondoka kwa muda mfupi tu kutembelea familia.

Muhimu zaidi, wanaogopa kuzungumza hadharani. Ingawa wana hamu ya kuzungumza na kushiriki ujumbe wa kusambaza kwa ulimwengu wa nje, wanajua kwamba kuonekana kwenye kamera au kufichua majina yao kunawaweka hatarini sana.

"Tungeuawa na ujasusi wa Irani," wananiambia. Lakini wanatamani mabadiliko. Wanazungumzia ufisadi na ukandamizaji, wa masuala mengi zaidi ya hijabu tu. Ni zaidi ya mfumo mzima kwamba kuvunja roho zao, wao kueleza. Iran ni nchi wanayoipenda, lakini wanaogopa kuishi.

Kumekuwa na maandamano nchini Iran hapo awali, lakini utawala huo umesimama kidete. Ndiyo maana ni vigumu sana kutabiri kitakachofuata. Huku maandamano ya hivi punde yakifikia miji mipya, binamu wa Mahsa Erfan anaamini kuwa kasi hiyo inaweza kuwa na athari ya kudumu.

"Hatupaswi kusahau watu wa Iran wamekuwa katika upinzani na maandamano dhidi ya utawala kwa miaka mingi, lakini watu sasa ni wanamapinduzi," anasema.

"Hao ni wanawake, wafanyakazi, walimu, wanamichezo, wasanii, wanaoingia mitaani na kuchanganya sauti zao za kutofautiana na familia ya Zhina. Kwa maoni yangu, maandamano haya yataendelea na yatamalizika kwa kuanguka kwa Jamhuri ya Kiislamu."