China inadhibiti madini adimu ambayo ulimwengu hununua..je, mikataba mipya ya Trump inaweza kubadilisha hilo?

Muda wa kusoma: Dakika 4

Rais wa Marekani Donald Trump amesaini mikataba mingi katika ziara yake ya Asia ili kuhakikisha usambazaji wa madini adimu, sekta muhimu ambayo China imekuwa ikiitawala kwa muda mrefu.

Mikataba na Japan, Malaysia, Thailand, Vietnam na Cambodia hutofautiana kwa ukubwa na dutu na ni mapema mno kutathmini athari zake zinazoonekana. Lakini yote yanajumuisha juhudi za kutofautisha upatikanaji wa madini ambayo yamekuwa muhimu kwa utengenezaji wa bidhaa wa hali ya juu, kuanzia magari ya umeme hadi simu za kisasa.

Mikataba hiyo, ambayo inalenga kuwafunga washirika katika biashara na Marekani, ni juhudi dhahiri ya kupunguza utegemezi kwa China, kabla ya mkutano muhimu na kiongozi wake Xi Jinping.

Hatimaye inaweza kupinga umiliki wa Beijing juu ya madini adimu, lakini wataalam wanasema itakuwa mchakato wa gharama kubwa ambao utachukua miaka mingi.

"Kujenga migodi mipya, vituo vya kusafisha, na viwanda vya usindikaji katika maeneo kama vile Australia, Marekani, na Ulaya kunakuja na gharama kubwa zaidi za mtaji, kanuni kali za mazingira, na pembejeo ghali zaidi za nguvu kazi na nishati [ikilinganishwa na China]," Patrick Schroder, mtafiti mkuu katika Kituo cha Mazingira na Jamii katika Chatham House aliandika katika tahariri wiki hii.

Haijabainika wazi bado kama uwekezaji wa dola bilioni 550 wa Marekani ambao Japan ilikubali hapo awali utakuwa sehemu ya makubaliano ya 'rare earths'. Waziri wa Biashara wa Marekani Howard Lutnick anatarajiwa kufafanua maelezo hayo na makampuni ya Japan wakati wa ziara yake ijayo.

Lakini ni hatua muhimu katika ushindani kati ya Marekani na China.

Unaweza kusoma

Beijing inadhibiti usindikaji wa karibu madini yote adimu duniani, jambo ambalo limempa Xi nguvu kubwa katika vita vya kibiashara vinavyoendelea na Washington.

Udhibiti wa mauzo ya nje wa China umezuia usambazaji wa madini adimu hivi karibuni huku nchi hizo mbili zikijaribu kusuluhisha makubaliano yanayohusisha masuala mbalimbali, kuanzia ushuru hadi uuzaji wa shughuli za TikTok nchini Marekani.

Udhibiti huo pia umeibua wasiwasi unaojulikana katika vituo vya utengenezaji nchini Marekani, Ulaya na Asia, ukumbusho wa jinsi minyororo ya usambazaji wa kimataifa ilivyo hatarini kwa uhusiano mgumu wa Marekani na China.

Kabla hata Trump hajasafiri kwenda Asia wiki hii, alifikia makubaliano ya dola bilioni 8.5 na Australia, akiahidi ushirikiano wa viwanda na uwekezaji wa pamoja ili kujenga uwezo wa usindikaji wa madini adimu nje ya China.

Akizungumza wakati huo, wakati wa ziara ya Waziri Mkuu wa Australia Anthony Albanese katika Ikulu ya White House, Trump alisema kwamba "katika takribani mwaka mmoja kuanzia sasa tutakuwa na madini mengi muhimu na madini adimu kiasi kwamba hutajua la kufanya nayo", akiongeza kwamba "yatakuwa na thamani ya dola 2", akimaanisha kwamba bei zitashuka kadiri usambazaji unavyoongezeka.

Muda na bei hazieleweki, lakini Australia hakika ni mshirika muhimu katika harakati za Marekani za kutafuta madini muhimu.

Kampuni kadhaa tayari zinajenga viwanda vya kusafisha, ikiwa ni pamoja na Iluka Resources, ambayo iliiambia BBC mapema mwaka huu kwamba itakuwa vigumu kifedha bila msaada wa serikali.

Mikataba na uchumi mdogo wa Kusini Mashariki mwa Asia ni midogo sana katika maelezo. Malaysia, Thailand, Vietnam na Cambodia zote zilikubaliana kuongeza ufikiaji wa Marekani kwa madini adimu na sheria za usafirishaji ambazo zingewapendelea wanunuzi wa Marekani kuliko makampuni ya Kichina.

Pia zinajumuisha ahadi kwamba hazitazuia usafirishaji kwenda Marekani, na zingehimiza usindikaji na uwekezaji wa ndani na makampuni yasiyo ya Kichina.

Lakini mikataba na Malaysia na Thailand ni makubaliano yasiyofungamana, au kile tunachokiita "Memorandum of Understanding" (MOU). Je, yatastahimili mabadiliko ya kisiasa katika nchi hizi?

Swali jingine kubwa ambalo halijashughulikiwa ni kanuni, hasa kutokana na uharibifu unaoweza kutokea wa mazingira. Kwa madini adimu, si uchimbaji tu bali hata usindikaji ambao ni biashara chafu.

Unahusisha uchimbaji, uchujaji na usafishaji, ambayo yote hutoa mionzi. Athari nchini China imethibitishwa vyema, ambayo imemaanisha kuwa si sekta ambayo nchi nyingine zimekumbatia kwa urahisi.

Mtoaji mkuu zaidi wa madini adimu duniani nje ya China ni kampuni ya Australia ya Lynas Rare Earths. Inategemea Malaysia kwa sehemu ya uboreshaji wake lakini imekabiliwa na vikwazo kadhaa vya udhibiti huko kwa miaka mingi.

Kwa kuwafunga mataifa makubwa ya kikanda kama Japan na Australia katika mikataba ya uwekezaji ambayo inaweza kuipa Marekani udhibiti zaidi juu ya usambazaji wa madini adimu, Trump ataingia katika mazungumzo ya Alhamisi yenye umuhimu mkubwa na Xi kwa msingi imara.

Lakini ukweli ni kwamba China bado inadhibiti karibu 70% ya usindikaji wa madini adimu. Na kuifikia kunahitaji kiasi kikubwa cha mtaji, sheria kali za mazingira na utaalamu wa kiufundi. Kujenga kiwanda kimoja cha usindikaji kunaweza kuchukua miaka kutoka kwa muundo hadi uzalishaji kamili.

Australia imekuwa ikizingatia kuongeza uzalishaji wa madini adimu kwa muda mrefu sasa, lakini mitambo yake bado haijaanza kufanya kazi.

Na China si mtazamaji kimya katika eneo hili, biashara na uchumi wa pili kwa ukubwa duniani ni muhimu kwa nchi hizi zote, ikiwa ni pamoja na Japan. Kwa hivyo Washington haiwezi kupuuza ushawishi unaotumiwa na Beijing, haswa Kusini Mashariki mwa Asia.