Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Wanawake wa Afrika na siri ya kubeba mizigo mizito karibu mara mbili zaidi ya uzito wao
- Author, Molly Gorman
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Wakulima kutoka maeneo mengi duniani hasa vijijini, huonekana kila siku wakibeba mizigo mizito iliyosokotwa kwenye fito, wengine kwenye kamba, na kuwekwa kichwani kwa umbali wa hadi maili kadhaa kwa miguu.
Vitu vikubwa na vizito kutoka mashambani, zana au vifaa mara nyingi vina uzito mkubwa zaidi kuliko uzito wa mwili wao wenyewe, lakini wanaonekana kuhimili mizigo hiyo kwa urahisi.
Hii ni kazi ambayo wengi wetu tungeshindwa kuimudu. Ni changamaoto kubeba kitu kizito kuliko mwili wako na ikiwa unabeba mzigo huo kwa masafa marefu changamoto inakuwa kubwa zaidi.
Wanwake wengi Afrika ndiyo watendaji wakuu wa shughuli za familia, kuanzia shambani mpaka nyumbani. Nchi za Magharibi, Afrika ya kati na Afrika Mashariki, kukuta wanawake na mizigo mikubwa wakitoka shambani, wakienda sokoni, wakienda mashineni nakadhalika ni kitu cha kawaida sana.
Katika Afrika Mashariki, wanawake mara nyingi hubeba mizigo inayolingana na asilimia 70% ya uzito wa miili yao au zaudu, juu ya vichwa vyao kwa masaa kadhaa.
Utafiti unaonyesha miili yao imebuni mbinu ya kuhifadhi nishati wanapotembea ili kupunguza nguvu za misuli zinazohitajika kubeba mizigo hiyo.
Makala hii inangazia kwa ujumla wanawake hawa wa Afrika Mashariki na wengine duniani linapokuja suala la kubeba vitu vizit kichwani.
Jamii ya Sherpa kutoka Himalaya mara kwa mara hubeba mizigo katika mabega na vichwani, ambapo mzigo unawekwa mgongoni na kusaidiwa na kamba ya kutegemea katika paji la uso. Mizigo wanayobeba mara nyingi inazidi uzito wa miili yao.
Wabeba mizigo katika eneo hilo wanaweza kubeba mizigo hii kwa safari zinazochukua siku kadhaa, wakitembea umbali wa kilomita 100 na kupanda milima ya hadi futi 26,000 (8,000m).
Lakini wakulima wa vijiji vya Vietnam kama ilivyo kwa wanawake wa Afrika Mashariki nwana silaha ya siri. Wa afrika Mashariki wanatumia kamba kama ilivyo wamasai, wengine wanaweka mizigo kichwani kama ilivyo, wengine hutumia kanga, lakini haa wa Vietnam wanatumia fito za mianzi imara. Hufunga mizigo pande mbili za muanzi, ili wakati wa kutembea mzigo huo utikisike huku wakipiga hatua.
Hilo hupunguza nguvu zinazohitajika kuinua uzito huo kwa kila hatua kwa takribani asilimia 18%, kulingana na utafiti mmoja uliochunguza uwezo wa wakulima hawa wa kubeba mizigo mizito.
Hata hivyo, licha ya uwezo huo wa kubeba vitu vizito, hakuna shaka kwamba wakulima hawa pia wana nguvu kubwa baada ya miaka mingi ya kubeba mizigo mizito.
Wengi wetu ambao hatufanyi kazi zinazohusisha kubeba vitu vizito, tunaweza pia kufaidika na kuwa na nguvu zaidi. Kipi kinachohitajika kujenga aina hii ya nguvu?
Kujenga mwili wenye nguvu
Hakuna shaka wanadamu wanapenda kuwa watu wenye nguvu. Michezo ya kuinua uzito huvutia watazamaji kwa zaidi ya miaka 4,000 na ilifanyika Misri ya kale, Ugiriki na China.
Maandishi, sanamu na vitu vya kale kama vile mawe makubwa ya kutupa huko Ugiriki ya kale vinaonyesha kwamba mashindano yanayohusisha kuinua vifaa vizito yalikuwa maarufu tangu mwaka 557 KK.
Mazoezi ya kuongeza nguvu kwa kuinua vitu vizito kama chuma, huleta faida kwa afya. Husaidia kujenga afya ya mwili na kupunguza vifo kutokana na magonjwa kama saratani na magonjwa ya moyo.
Baadhi ya tafiti zinapendekeza, mazoezi ya kutumia nguvu yana manufaa kwa afya ya akili pia. Mbali na ile faida ya kujenga misuli ya mwili.
Wataalamu wanasema kabla ya kuanza kubebe vitu vizito, kwanza uanze kunyanyua vitu ambavyo sio vizito sana unavyovihimili, kisha ndio unyanyue vitu ambavyo ni vizito zaidi.
Baadhi ya tafiti zinaonyesha unaweza kupata faida sawa ya kiafya kwa kuinua uzito mwepesi na kurudia mara nyingi kama vile kuinua uzito mzito na kurudia mara kidogo.
Tafiti nyingine zinapendekeza kuunganisha uzito mkubwa na mwepesi katika mazoezi ili kuboresha nguvu zako. Na inapendekezwa kuinua uzito kwa dakika mbili hadi tano kisha kupumzika na kuendelea, hilo huleta faida kubwa zaidi.
Ingawa wataalamu wengi wanapendekeza mbinu ya kuchuchumaa wakati kuinua vyuma vizito, kuna mjadala kuhusu kama hii ni njia bora kwa afya ya mgongo au la.
Ubebaji wa migizo mizito
Hata hivyo, kuna njia nyingine za kuongeza uwezo wa kubeba mizigo bila kutumia mbinua ya kuinua vyuma katika ukumbi wa michezo ya mazoezi ya viungo.
Kama wakulima wa Vietnam, baadhi ya jamii zimeendeleza mbinu za kubeba mizigo mizito kwa umbali mrefu.
Kwa mfano, katika karne ya 20, wachuuzi wa sokoni huko Covent Garden, London, walibeba vikapu vya matunda na mboga juu ya vichwa vyao.
Mbinu za jadi za kubeba mizigo bado ni za kawaida leo, hasa katika nchi zinazoendelea.
Kaskazini-mashariki mwa India, kubeba mizigo kwa mikono hutumika sana wakati wa kusafirisha bidhaa na vifaa kwa umbali mrefu katika maeneo magumu, hasa kutokana na kukosekana kwa miundombinu ya usafiri katika maeneo ya milima, lakini pia kwa sababu za kiuchumi.
Utafiti unaonyesha kuwa msaada kama kamba za kiuno na mabega hupunguza mapigo ya moyo na matumizi ya oksijeni, na kusaidia kubeba mizigo kwa muda mrefu au umbali mrefu.
Uwezo wa kubeba mizigo unategemea mambo kama umri, nguvu za misuli, na mazingira.
Wanajeshi hutumia nguvu nyingi kubeba mizigo inayozidi kilogramu 45, na mafanikio yao hutegemea uwezo wa kusonga mbele kwa haraka wakiwa wanabeba mizigo hii.
Kituo cha Kudhibiti Magonjwa cha Marekani kinashauri kufanya mazoezi ya kubeba vitu vizito mara mbili kwa wiki kama sehemu ya ratiba yako ya mazoezi.
Hilo ni muhimu hasa kwa kuzingatia ongezeko la watu wenye umri mkubwa – ifikapo mwaka 2030, 20% ya Wamarekani watakuwa na umri wa miaka 65 au zaidi.
Kadri watu wanavyozeeka, hupoteza uzito wa misuli na nguvu, lakini mazoezi ya kuinua vitu vizito mara nyingi yanaweza kusaidia kudumisha uzito wa mifupa, kupunguza hatari ya ugonjwa wa mifupa na kuboresha afya ya viungo, usingizi na kujiamini.
Pengine hutahitaji kubeba mzigo kwenye milima au kuwa na hamu ya kuvunja rekodi za dunia kama mashindano ya Olimpiki, lakini nguvu za ajabu za watu hawa zinaweza kukuhamasisha kuchukua chuma chenye uzito kwa ajili ya mazoezi ya viungo.
Imetafsiriwa na Mariam Mjahid na kuhaririwa na Yusuph Mazimu