Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Kwa nini baadhi ya Waghana wanajiunga na waasi kupigana Burkina Faso?
- Author, Ed Butler
- Nafasi, BBC
- Muda wa kusoma: Dakika 6
Raia watatu wa Ghana wameieleza BBC juu ya kuhusika kwao katika mapigano kati ya wapiganaji wa Kiislamu na wanajeshi katika nchi jirani ya Burkina Faso.
"Siku zote tuko pamoja na maiti. Katika baadhi ya matukio, nimeona watu 40, 50 au 100 waliokufa," amesema mmoja wa wanaume wao.
Watatu hao, wote wakiwa na umri wa miaka ya mwisho ya thelathini au mapema arobaini, wanasema wamepigana nchini Burkina Faso mara nyingi tangu 2018. Walivuka mpaka wa urefu wa kilomita 550 (maili 340) kati ya nchi hizo mbili, bila kugunduliwa na vikosi vya usalama.
Wamekanusha kuchochewa na dini au kufunzwa na wanajihadi, wanasema walikwenda kupigana ili kutetea jamii ambayo wana uhusiano nayo kifamilia na kikabila.
"Ndugu yangu mkubwa, mke wake na watoto wote waliuawa na jeshi la [Burkinabe]. Inaniuma sana. Wanajeshi walikuja kwenye jamii yao msituni. Waliwaua wote, kaya nzima, ikiwa ni pamoja na watu 29," amesema mmoja wa watu hao.
Lakini mmoja katika watatu hao ameeleza sababu za kidini, akisema: "Ikiwa utakufa wakati unapigana na wanajihadi, basi unakwenda Jannah (neno la Kiislamu la peponi), njia ya watu wema."
Walipoulizwa ikiwa walishiriki katika mashambulizi dhidi ya raia, watu hao waligawanyika. Mmoja alikana kufanya hivyo, lakini mwingine alikubali kwamba alifanya hivyo.
"Baadhi ya wenyeji wanaunga mkono jeshi kutushambulia, ndiyo maana inatubidi kuwaua pia," amesema.
"Unajua sifurahii kupigana hivi. Idadi ya watu tunaowaua, watu wanaouawa na wanajeshi, ni kubwa sana. Lakini mapambano haya yameingia kwenye damu yetu," aliongeza.
Wote watatu walizungumza kwa sharti la kutotajwa majina.
BBC haikuweza kuthibitisha madai yao lakini walituonyesha picha za silaha, wakaeleza eneo la migogoro na kuwataja makamanda wa kijihadi nchini Burkina Faso.
BBC iliwasiliana na wanaume hao katika soko la mifugo kaskazini mwa Ghana, ambapo makundi ya wanajihadi yanadaiwa kuwasajili wapiganaji.
Kuajiri wapiganaji
Mwaka 2022, shirika lisilo la kiserikali lenye makao yake makuu nchini Ufaransa, Promediation, lilisema utafiti wake unaonyesha wanajihadi waliajiri vijana kati ya 200 na 300 kutoka Ghana.
Na Taasisi ya Uhusiano wa Kimataifa ya Uholanzi, katika ripoti iliyotolewa Julai iliyopita, inasema wanajihadi walipata "mafanikio madogo" katika kuajiri wapiganaji nchini Ghana.
Hata hivyo, wanaume hao walitoa mtazamo tofauti, katika madai ambayo hayakuweza kuthibitishwa, wanasema watu kutoka "sehemu zote za Ghana" na kutoka makabila mengi wamejiunga na uasi nchini Burkina Faso.
"Wengine wanapigania jihad. Wengine wanapigana kwa ajili ya biashara," amesema mmoja wao.
Malipo ya kifedha yanakuja kwa njia ya mifugo ambayo wanajihadi huiba kutoka katika jamii zilizofukuzwa katika vijiji vyao.
"Tunaposhambulia jamii, tunachukua wanyama wao; wakati mwingine 50, wakati mwingine 100," BBC iliambiwa na mmoja wa wanaume hao.
Wanaeleza kuwa ng'ombe hao huletwa kaskazini mwa Ghana, na kuuzwa sokoni. Usafirishaji haramu huo katika mpaka ulithibitishwa na BBC kupitia wafanyabiashara wa mifugo.
Inaaminika kuwa hiyo ndio njia kuu ya mapato kwa vikundi kama vile Jama'at Nusrat ul-Islam wa al-Muslimin (JNIM), mshirika wa al-Qaeda, kikundi cha jihadi kinachofanya kazi zaidi nchini Burkina Faso. Vilevile kipo nchini Niger na Mali.
Umoja wa Mataifa ulieleza mwaka jana kuwa, Ukanda ya Afrika Magharibi ni kitovu cha ghasia za wanajihadi duniani.
Maelfu wameuawa
Mashirika ya misaada yanasema katika muongo mmoja uliopita, watu milioni mbili wamekimbia makazi yao kutokana na waasi nchini Burkina Faso na maelfu wameuawa.
Ninpoa Nasuri ni mmoja wa maelfu waliokimbilia Ghana kuepuka ghasia, ameiambia BBC, mume wake aliuawa mbele yake mwaka 2024 wakati wa uvamizi katika kijiji chao mashariki mwa Burkina Faso na wapiganaji kutoka JNIM.
"Waliwakamata wanaume, na wakawapiga hadi kuwaua. Mume wangu alikuwa mkulima. Hakuwa na uhusiano wowote na wanamgambo wa serikali au mzozo huo," aliambia BBC.
Wakimbizi wengine wameelezea vitendo kama hivyo vya ghasia vilivyofanywa na jeshi la Burkinab.
"Baadhi ya watu waliokuwa wakiwaua walikuwa na umri wa miaka 80, wenye umri wa miaka 90. Watu hawa hawawezi kushika bunduki, hawawezi kupigana na mtu yeyote. Waliwaua bila sababu," anasema Saafiya Karim.
Ghana hadi sasa bado haijaguswa na uasi huo, ingawa kuna mashambulizi yamefanyika katika nchi jirani za Togo na Ivory Coast.
Katika taarifa ya hivi karibuni kwa mwandishi wa habari wa Ghana, Mohammed Eliasu Tanko, mtu anayejiita mwakilishi wa JNIM, amesema kundi hilo halina nia ya kuanzisha mashambulizi nchini Ghana.
"Wao (wapiganaji wa JNIM) hawaruhusiwi kuchukua hatua yoyote dhidi ya Ghana. Hii ni kauli ya wazi na ya uhakika. JNIM haitafuti vita na Ghana," mtu huyo anayejulikana kwa jina la Ansari alisema katika taarifa hiyo.
Hata hivyo kuongezeka kwa ghasia za kijamii katika sehemu ya kaskazini mwa Ghana, kumeibua wasiwasi kwamba wanajihadi huenda wakatumia mzozo huo kwa manufaa yao.
Migogoro ya kikabila
Mji wa Bawku uko katika vurugu za miongo kadhaa kati ya makabila tofauti kwa ajili ya udhibiti wa uchifu wa eneo hilo. Zaidi ya watu 100 wanaaminika wameuawa katika mapigano tangu mapigano yalipozidi mwezi Oktoba mwaka uliopita.
"Ikifika jioni huko Bawku ni milio ya risasi na majibizano ya bunduki. Watu wanatumia AK47, M16, na kila aina ya bunduki," mkazi mmoja ameiambia BBC.
Wasafirishaji haramu wa silaha kutoka JNIM wanatuhumiwa kuuza silaha pande zote mbili za mapigano.
"Tunaelewa kuwa wanasambaza silaha ambazo wamezichukua kutoka kwa wanajeshi nchini Burkina Faso. Wanafanya hivyo kwa kutumia lori zinazosafiri hadi Niger, nyuma zikiwa zimebeba vitunguu. Wanaficha silaha ndani ya malori hayo," anasema Tanko.
"Afisa mmoja wa ujasusi alinithibitishia kuwa hii ndiyo njia mpya wanayotumia kusambaza bunduki. Na maafisa wa usalama wa Ghana hawana vifaa vya kutosha kuweza kugundua magari haya, na hilo linaiweka Ghana katika hali mbaya sana," amesema.
Waziri wa Ulinzi wa Ghana Edward Omane Boamah hakujibu ombi la BBC la kutaka maoni yake.
Rais John Mahama, aliyeingia madarakani mwezi Januari baada ya kushinda uchaguzi wa rais mwezi Disemba, alitembelea huko Bawku mwezi uliopita katika juhudi za kukuza amani kati ya makundi hasimu. Hata hivyo, mapigano ya bunduki yanaendelea kuripotiwa.
Msemaji wa chama tawala cha Ghana Sammy Gyamfi aliiambia BBC, kukomesha ghasia huko Bawku ni "kipaumbele namba moja" cha serikali.
"Vurugu tayari zinaenea na ikiwa uangalifu hautachukuliwa kuna uwezekano waasi wanaweza kuchukua fursa ya mzozo huo," amesema.
Wanaume watatu ambao BBC ilizungumza nao wanasema hawaondoi uwezekano wa kuenea kwa uasi.
"Uasi unaweza kwenda sehemu yoyote, au nchi yoyote. Haukuwepo Togo lakini sasa mashambulizi yanatokea huko. Ikiwa wanaweza kwenda Togo, wanaweza kufika Ghana," amesema mmoja wao.
Lakini mwingine alikuwa na mtazamo tofauti, akisema waasi nchini Burkina Faso hawafanyi tena "mapambano ya Kiislamu."
"Wanaua tu watu, na kuiba mifugo yao. Kinachofanyika sio jihadi na hivyo sipendi," amesema.