Hadithi ya mapenzi ya mtandaoni ya raia wa India na Pakistani iliyoishia gerezani

Polisi wanasema Iqra na Mulayam walikutana mtandaoni mnamo 2020 wakati wa janga la Covid

Chanzo cha picha, BANGALORE POLICE

Mnamo Januari, mwanaume mmoja wa nchini India alikamatwa kwa kumsaidia mwanamke wa Pakistani kuingia nchini kinyume cha sheria na kupata kitambulisho ghushi.

Aliyemsaidia alikuwa mke wake.

Mulayam Singh Yadav, 21, kutoka India na Iqra Jeewani, 19, kutoka Pakistani walikutana na kupendana mtandaoni miaka mitatu iliyopita, walipokuwa wakicheza mchezo wa Ludo. Lakini walijua itakuwa vigumu kwao kuwa pamoja.

India na Pakistan zina uhusiano mbaya, majirani wamepigana vita tatu tangu 1947, wakati India iligawanywa na Pakistan kuundwa. Hii inaweza kufanya iwe vigumu kwa watu kupata visa kusafiri ili kuonana.

Kwa hivyo Septemba mwaka jana, Mulayam na Iqra walisafiri kwenda Nepal, ambapo walifunga ndoa. Kisha walisafiri hadi mji wa India wa Bangalore mji mkuu wa jimbo la Karnataka na kuishi pamoja.

Lakini maisha yao ya furaha yaligeuka kuwa ya kusikitisha mnamo Januari Bi Jeewani alikamatwa kwa kosa la kuingia India kinyume cha sheria huku Bw Yadav akikamatwa na kufunguliwa mashtaka ya ulaghai, kughushi na kutoa hifadhi kwa raia wa kigeni bila hati sahihi.

Alifukuzwa nchini Pakistan wiki iliyopita, wakati Bw Yadav akisalia jela huko Bangalore.

Wanafamilia wa Bw Yadav, wanaoishi katika jimbo la kaskazini mwa India la Uttar Pradesh, wamesikitishwa na kukamatwa kwa watu hao. Wanasema hadithi ya wanandoa ni moja tu ya upendo.

"Tunawataka warudi nyumbani," kaka yake Jeetlal anasema. "Tunaelewa hali kati ya India na Pakistan. Lakini walichokifanya ni kupendana."

Hata polisi wanaonekana kukubaliana nao.

"Mbali na kuingia kinyume cha sheria na kughushi, inaonekana kama hadithi ya mapenzi," afisa mkuu wa polisi wa Bangalore alisema kwa sharti la kutotajwa jina.

Wawili hao walifunga ndoa huko Nepal mwaka jana lakini muda wao wa kuwa pamoja ulikuwa mfupi

Chanzo cha picha, JEET LAL YADAV

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Hadithi hiyo ya mapenzi ilianza mnamo 2020, wakati wa kufungwa kwa Covid.

Bw Yadav alifanya kazi kama mlinzi wa kampuni ya IT mjini Bangalore huku Bi Jeewani akiwa mwanafunzi katika mji wa Hyderabad nchini Pakistan.

Wawili hao walianza uhusiano wa masafa marefu baada ya kukutana mtandaoni. Lakini Bi Jeewani alikuwa chini ya shinikizo kubwa kutoka kwa familia yake kuolewa.

Kwa pendekezo la Bw Yadav, aliondoka Pakistani na kusafiri hadi Nepal kupitia Dubai kukutana naye. Polisi wanasema wawili hao walifunga ndoa katika sherehe ya Kihindu katika hekalu moja huko na kuja India.

Lakini Bi Jeewani hakuwa na hati zinazohitajika kusalia India, kwa hivyo polisi wanasema Bw Yadav alipanga kadi bandia ya Aadhaar hati ya utambulisho wa Kihindi kwa ajili yake.

Kulingana na polisi, Bw Yadav alikuwa akitoka kila siku kwenda kazini huku Bi Jeewani akisalia nyumbani.

Lakini mara kwa mara alipiga simu kwa WhatsApp kwa mama yake huko Pakistani, ambayo iliwaongoza polisi kwake.

Maafisa wa polisi wa Bangalore wanasema walikuwa katika hali ya tahadhari mwezi uliopita kwa sababu matukio mawili makubwa ya kimataifa yalipaswa kufanyika katika jiji hilo mwezi Februari: onyesho la anga la Aero India na mkutano wa mawaziri wa fedha wa G20.

Baada ya uchunguzi zaidi, Bi Jeewani alikamatwa kwa kuingia kinyume cha sheria na alikabidhiwa kwa Ofisi ya Usajili wa Wageni Kanda tarehe 20 Januari. Alifukuzwa nchini Pakistan mwezi Februari.

"Kufikia sasa, hakuna kosa aliloshtakiwa nalo zaidi ya kuingia nchini kinyume cha sheria," S Girish, naibu kamishna wa polisi katika wilaya ya Whitefield ya Bangalore, aliiambia BBC. "Lakini uchunguzi unaendelea."

BBC haikuweza kumfikia Bi Jeewani au familia yake nchini Pakistan kwa ajili ya kupata maoni yake. Mapema wiki hii, shirika la habari la PTI liliripoti kwamba baba yake alikuwa amethibitisha kuwa amefika nyumbani, na kwamba hawakutaka "kuzungumza kuhusu suala hili".

Mama yake Bw Yadav Shanti Devi anasema anatumai serikali za nchi zote mbili zinaweza kusaidia kuwaunganisha tena.

"Hatujali kama yeye ni Muislamu au Mpakistani, ni binti, mkwe wetu. Tutamtunza vyema."