Masaibu ya kutekwa nyara na kubakwa na mwendesha bodaboda

Na Anne Ngugi

BBC News Swahili

Shyro Ogolla ni mwanamke mwenye umri wa miaka 28 kutoka nchini Kenya, kwa miaka aliyonayo amekumbana na matukio mengi ya dhiki katika maisha yake, na sasa ameamua atumie fursa hii kama njia ya kuielimisha jamii na pia kutoa nasaha hasa kwa vijana wa kike wa Kiafrika .

Mazingira yake ya kuzaliwa na kukua yamekuwa na masaibu mengi kuanzia utotoni lakini amejipiga moyo konde na kuendelea na maisha yake kama watu wengine .

Ila tukio moja ambalo hajasahau katika maisha yake ni dhuluma ya kingono ambayo aliyotendewa na muendeshaji bodaboda (pikipiki) ambaye anasema alikuwa na uhusiano wa kibiashara na yeye, ila siku moja aligeuka kutoka kondoo na kuwa mbwa mwitu.

Matukio ya Kisa cha kutekwa nyara na dhuluma za kingono

Shyro anasema kuwa hawezi kusahau tarehe 2 mwezi Oktoba mwaka wa 2016 , akiwa msanii alikuwa anategemea siku hiyo angetumia muda mwingi katika studio moja ya mjini Nairobi kama ilivyokuwa ada yake .

”Nakumbuka siku hiyo nilimuita jamaa aliyekuwa ananibeba kutoka nyumbani hadi studio , alifika na kunichukua katika mlango mkuu wa nyumbani kwetu.

Ila wakati huu alichukua njia tofauti , nilipomuuliza alinieleza kuwa alikuwa anachukua kitu kimoja mahali kisha tuanze safari yetu”, anakumbuka Shyro.

Lakini hatua yake ya kutumia njiani tofauti ndio uliokuwa mwanzo wa matukio ya dhuluma yaliokuwa mbele yake.

Mwanadada huyu anasema kuwa pindi walipofika katika lango moja kuu mwendesha pikipiki huyo alinyanyuka na kumzaba kofi ghafla na kumuamrisha ashuke kutoka kwenye pikipiki .

Mwanamke huyu anasema kuwa hakuwa na wakati wa kufikiria yaliyokuwa yakifanyika kwa kuwa alikuwa akimfahamu mwendesha pikipiki huyo katika pilkapilka zake za kutafuta usafiri wa boda boda kutoka eneo moja hadi jingine .

Shyro anasema kuwa tukio hilo lilifanyika mapema asubuhi saa tatu ambapo mhudumu huyo wa bodaboda alimshurutisha kumfuata huku akiwa amemshikia kisu shingoni , hadi walipofika nyumba moja ya mabati .

”Nakumbuka mhudumu huyo aliingia ndani ya nyumba na akaongeza sauti ya muziki uliokuwa unacheza kwa sauti ya juu sana kwa kiasi kuwa hakuna ambaye angehisi akiwa ndani ya nyumba kulikuwa na matatizo yeyote yanaendelea,”anakumbuka Shyro.

Mwanamke huyu anasema kuwa alipitia masaibu ya kubakwa na kushurutishwa kushiriki ngono baada ya kupokea kichapo kibaya, ambacho kilimtia uwoga wa kufanya lolote .

”Anaongezea kwamba kila mara baada ya kunibaka aligeukia msokoto wa bhangi ambao aliuwasha kuvuta kisha kuanza kulia mwenyewe huku akisema kuwa hakuna mtu anayempenda ikiwemo mimi, ni tukio ambalo lilinipa wasiwasi na hofu nisijue kwamba ningetoka katika chumba hicho nikiwa hai au la”,anasema.

Anakumbuka kwamba baada ya vuta nikuvute hiyo kati yake na mhudumu wa bodaboda , simu ya mkononi ya mwanadada huyo ilianza kulia kila mara hasa kwa sababu alikuwa anasubiriwa kwenye studio na masaa yalikuwa yamesonga mno .

Mwanadada huyu alipata ujasiri wa kuzungumza na mshambuliaji wake huku akimweleza kuwa iwapo ataendelea kumshika huenda watu wakaanza kumtafuta kwani hakuwa anapokea simu na tayari walifahamu kuwa alikuwa njiani kuelekea huko .

Mhudumu wa boda aliamua kumwachilia masaa ya jioni huku akimsindikiza hadi katika kituo cha kusubiri magari ambapo alichukua gari la uchukuzi.

Masaibu ya kutafuta haki baada ya dhuluma ya kingono

Kuanzia mwaka wa 2016 Shyro anasema kuwa alianza kutafuta haki , ila kesi yenyewe ilikumbwa na changamoto moja baada ya nyengine.

Wakati huo huo Shyro anasema kuwa kutokana na dhuluma hizo alijipata ameanza kunywa pombe kupindukia kama njia nyepesi ya kuponesha vidonda vya moyoni baada ya tukio hilo ambalo hadi sasa anasema ni gumu kusahau.

Hali hiyo ilimfanya kuwa mraibu wa kileo hicho kwa muda mrefu na kuamua kukata tamaa ya kuifuatilia kesi hiyo baada ya kugundua kwamba mshukiwa wa kitendo hicho aliachiliwa muda mfupi baada ya kukamatwa .

Je ni ushauri upi ambao Shyro anautoa kwa watu wanaotumia pikipiki kama usafiri wao?

“Kuna mengi ningeweza kusema hasa kuhusiana na mteja kuwa na uzoefu na muhudumu wa boda boda kwani kuna baadhi yao ambao huwa hawana nia nzuri licha ya kuwa wanatoa huduma ya usafiri kwa watu “

Mwanadada huyu anasema ni muhimu sana kwa wanawake kuwa waangalifu na kufanya mazoea ya utambuzi wa mtu anayewabeba katika bodaboda. Ni vyema pia kuwa muangalifu na mawasiliano ya mwili, wanavyozungumza na mtu .

“ Kama kwangu nilipuuza kuwa mwendesha pikipiki wangu alichukulia ukarimu wangu na uzuri wangu kwake kama fursa ya kuwa na uhusiano wa kimapenzi nami , ila hicho ni kitu nilimueleza hakiwezekani , laiti ningekuwa macho zaidi linapokuja suala la tabia yake akiwa karibu na mimi ningeona hitaji la kukatisha huduma yake mara moja.”Shyro anasema.

Aidha Shyro anasema kuwa sio vizuri kuwaruhusu watu kama wahudumu wa bodaboda kufika karibu sana na nyumbani kwako au hata kwa watu wa karibu sana na wewe kwani anasema mazoea yana taabu.