'Bomu chafu': Bomu gani hili na kwanini Urusi inalihofia?

Waziri wa ulinzi wa Urusi amedai kuwa huenda Ukraine ikatumia "bomu chafu" - kifaa chenye mionzi ya pamoja na vilipuzi vya milipuko ya kawaida.

Hajatoa ushahidi wowote, na Ukraine - pamoja na Ufaransa, Uingereza na Marekani - imetupilia mbali madai hayo.

Urusi imesema nini?

Sergei Shoigu alimwambia waziri wa ulinzi wa Uingereza, Ben Wallace, kwamba "anajali kuhusu uwezekano wa uchochezi wa Kyiv unaohusisha matumizi ya bomu chafu".

Pia amezungumza na mawaziri wa ulinzi nchini Marekani, Ufaransa na Uturuki, akitoa maoni sawa.

Katika majibu yao ya pamoja Ufaransa, Uingereza na Marekani zimesema serikali zao " zote zinakanusha madai ya uongo wa wazi ya Urusi kwamba Ukraine inajiandaa kutumia bomu chafu katika mipaka yake".

Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, alikanusha madai hayo na kuishutumu Urusi kuwa "chanzo cha kila kitu kichafu ambacho kinaweza kufikiriwa katika vita hivi".

'Bomu chafu' ama la mionzi ni nini? na linafafanaje?

Ni bomu ambalo lina nyenzo za mionzi, ambayo hutawanyika hewani wakati linapolipuliwa.

Haihitaji kuwa na nyenzo za mionzi iliyosafishwa sana, kama inavyotumiwa katika bomu la nyuklia.

Badala yake, inaweza kutumia nyenzo za mionzi kutoka hospitalini, vinu vya nguvu za nyuklia au maabara za utafiti.

Hii inazifanya kuwa nafuu zaidi na haraka kutengenezwa kuliko silaha za nyuklia. Ni rahisi kubebeka na yanaweza pia kubebwa hata nyuma ya gari.

Kwa sababu ya mionzi yake inayosambaa umbalii mrefu kunaweza kusababisha magonjwa makubwa, kama vile saratani. Ni bomu linaloweza kusababisha hofu kati ya watu wanaolengwa.

Eneo pana kuzunguka eneo la mlipuko pia lingelazimisha watu kuhamishwa ili kukwepa kuathiriwa kutokana na mabaki ya mionzi, eneo hilo limechafuliwa, na pengine litalazimika kuachwa kabisa.

Shirikisho la Wanasayansi wa Marekani limekadiria kwamba ikiwa bomu lililokuwa na gramu 9 (0.3oz) ya cobalt-60 na kilo 5 ya TNT lingelipuliwa kwenye ncha ya Manhattan, huko New York, itafanya eneo lote la jiji lisiwe na makazi kwa miongo kadha.

Kwa sababu hii, mabomu machafu yanajulikana kama silaha zenye usumbufu mkubwa. Hata hivyo, kama silaha, haziaminiki sana.

Ili nyenzo ya mionzi iliyo kwenye bomu chafu isambae katika eneo linalolengwa, inabidi ipunguzwe kuwa poda.

Lakini ikiwa chembe hizo ni laini sana au zimeachiliwa kwenye upepo mkali, zinaweza kutatawanyika sana ina kuleta madhara mengi.

Kwanini Urusi inatoa madai haya sasa?

Taasisi ya Marekani ya Utafiti wa Vita (ISW) imesema waziri wa ulinzi wa Urusi "huenda alitaka kupunguza au kusimamisha misaada ya kijeshi ya nchi za Magharibi kwenda Ukraine na pengine kudhoofisha muungano wa Nato katika wito wa kutishia".

Pia kumekuwa na uvumi kwamba Urusi inapanga kulipua bomu chafu nchini Ukraine na imeamua kuvitupia lawama vikosi vya Ukraine katika shambulio la kutafuta kisingizio cha kuzidisha mzozo huo.

Hata hivyo, wachambuzi wengi wa masuala ya kijeshi wanasema Urusi haitakuwa mjinga kiasi hiki, kutokana na uharibifu ambao bomu chafu linaweza kufanya kwa wanajeshi wake na eneo lililo chini ya udhibiti wake.

ISW yenyewe imesema: "Kremlin haiwezekani kuandaa shambulio chafu la bomu la bendera ya uwongo."

Bomu chafu lishawahi kutumika duniani?

Bado hakujawa na shambulio la bomu chafu lililofanikiwa popote ulimwenguni.

Hata hivyo, kumekuwa na majaribio. Mnamo 1996, waasi kutoka Chechnya walitega bomu lililokuwa na baruti na caesium-137 katika Hifadhi ya Izmailovo ya Moscow.

Cesium ilikuwa imetolewa kutoka kwa vifaa vya kutibu saratani. Watu wa usalama waligundua lilipo na kulisambaratisha.

Mnamo 1998, idara ya ujasusi ya Chechnya ilitegua bomu chafu ambalo lilikuwa limewekwa karibu na njia ya reli huko Chechyna.

Mwaka 2002, Jose Padilla, raia wa Marekani ambaye alikuwa na mawasiliano na al-Qaeda, alikamatwa mjini Chicago kwa tuhuma za kupanga shambulio la chafu la bomu. Alihukumiwa kifungo cha miaka 21 jela.

Miaka miwili baadaye, Dhiren Barot, raia wa Uingereza na mwanachama wa al-Qaeda, alikamatwa London na baadaye kufungwa jela miaka 30 kwa kupanga mashambulizi ya kigaidi nchini Marekani na Uingereza ambayo yangejumuisha matumizi ya bomu chafu.

Hata hivyo, si Padilla wala Barot waliokuwa wameanza kukusanya mabomu yao kabla ya kukamatwa.