Vympel: Kikosi cha siri kinachotumiwa na Kremlin kuwaangamiza maadui wa Putin nje ya Urusi

Hatua ya hivi karibuni ya rais wa Urusi Vladmir Putin kutaka kuachiliwa kwa mshukiwa wa mauaji Vadim Krasikov ambaye anatumikia kifungo cha jela nchini Ujerumani imefungua mwanya kuhusu kikosi cha siri FSB ambacho watu wengi hawajui shughuli zake na operesheni zake zimeghubikwa katika usiri mkubwa .

Kwanza lazima ujue kinachofungua mwanya wa kuelewa hatua ya Putin ya kutaka kubadilishana wafungwa wanaozuiliwa Urusi na Krasikov.

Ni mwaka mmoja sasa tangu mwanahabari wa Marekani Evan Gershkovich azuiliwe katika safari yake ya kuripoti nchini Urusi. Tumaini lake bora la kuachiliwa linaweza kuwa Vadim Krasikov, ambaye anazuiliwa katika jela ya Ujerumani, aliyehukumiwa kwa mauaji ambayo yaliamriwa na Kremlin.

Katika msimu wa joto wa 2013, mmiliki wa mgahawa wa Moscow alipigwa risasi katika mji mkuu wa Urusi. Mwanamume aliyevalia kofia aliruka kutoka kwenye baiskeli na kumpiga risasi mara mbili kabla ya kukimbia.

Miaka sita baadaye, kamanda wa Chechnya aliyekimbilia uhamishoni Zelimkhan Khangoshvili, aliuawa katika bustani ya Berlin yenye shughuli nyingi katika hali kama hiyo ya kutisha, akipigwa risasi na mtu aliyekuwa kwenye baiskeli kutumia bastola ya Glock 26 mchana peupe.

Mshambulizi huyo alikamatwa baada ya kutupa bastola na wigi kwenye mto Spree karibu na Reichstag, jengo la bunge la Ujerumani.

Pasipoti iliyo na jina "Vadim Sokolov" ilipatikana kwa muuaji wa Berlin, lakini viongozi waligundua haraka kuwa hilo halikuwa jina lake.

Mwanamume mwenye kipara, waliyemkamata alikuwa ni Vadim Krasikov, raia wa Urusi ambaye ana uhusiano na FSB, idara ya usalama ya Urusi - na mshukiwa mkuu wa mauaji ya 2013 huko Moscow.

Katika mahojiano ya hivi majuzi na mtangazaji wa Marekani Tucker Carlson, Rais wa Urusi Vladimir Putin alionekana kuthibitisha ripoti kwamba nchi yake ilikuwa inataka kuachiliwa kwa "mzalendo" Krasikov kubadilishana na mwandishi wa habari wa Marekani Evan Gershkovich.

Mwezi huu umetimia mwaka mmoja tangu Bw Gershkovich, ripota wa Wall Street Journal, kuzuiliwa nchini Urusi kwa tuhuma za ujasusi ambazo zinakanushwa na yeye, gazeti lake na serikali ya Marekani.

Bwana Gershkovich sio Mmarekani pekee katika jela ya Urusi ambaye hatima yake inaweza kuunganishwa na ya Krasikov. Mwanajeshi wa zamani wa Marekani Paul Whelan na raia wa Marekani-Urusi Alsu Kurmasheva pia wanazuiliwa nchini Urusi kwa mashtaka yanayotazamwa na wengi kuwa ya kisiasa.

Maadui wa Kremlin

Mwathiriwa wake, Zelimkhan Khangoshvili, alikuwa kamanda wa waasi wa Chechnya kati ya 2000 na 2004, wakati Chechnya ilikuwa inapigana vita vya uhuru dhidi ya Urusi.

Kwa waangalizi wa Magharibi, Bw Khangoshvili alionekana kuwa sehemu ya msururu wa mauaji yaliyoamriwa na Moscow ya watu waliotoroka Chechen kwenda huko Ulaya na Mashariki ya Kati.

Kremlin ilikanusha kupanga mauaji ya Berlin, na kutupilia mbali hukumu dhidi ya Krasikov kama "iliyochochewa kisiasa".

Hata hivyo, katika mahojiano yake na Tucker Carlson, Rais Putin alionekana kukiri pale aliposema mazungumzo yanaendelea kwa ajili ya mabadilishano yanayomhusisha "mzalendo" wa Urusi ambaye "aliyemwondoa jambazi" katika mji mkuu wa Ulaya.

Ulrich Lechte, ambaye yuko katika kamati ya maswala ya kigeni ya serikali ya Ujerumani, aliiambia BBC kwamba nia ya Rais Putin kumrejesha Krasikov "ni kukiri wazi kuwa na hatia na inaonyesha jinsi Urusi ilivyoweza kuchukua hatua katika nchi yetu kwa udhalimu na bila kupingwa".

Uhusiano wa Vadim Krasikov na kikosi cha Vympel

Vadim Krasikov alikuwa wa kitengo cha siri cha 'Vympel' cha huduma ya siri ya Urusi, FSB, kulingana na waendesha mashtaka katika kesi yake.

"Majukumu yake rasmi ni operesheni za kukabiliana na ugaidi nyumbani, lakini kwa njia nyingi imerejea kwenye mizizi yake ya awali, kama kitengo kilichopewa jukumu la "kazi-nyevu" - hujuma na mauaji - nje ya nchi," anasema mwanahistoria wa Putin na mtaalamu wa usalama wa Urusi Mark Galeotti .

Krasikov binafsi alikutana na Putin kwenye safu ya kulenga shabaha alipokuwa akihudumu na Vympel, akimiliki BMW na Porsche, na alisafiri kwenda kazini mara kwa mara, kulingana na mahojiano ambayo shemeji yake alitoa The Insider.

Ushirikiano kati ya Krasikov na FSB unatoa maelezo ya kwa nini Vladimir Putin, afisa wa zamani wa ujasusi wa kigeni mwenyewe, atakuwa tayari kumkabidhi mfungwa wa thamani ya Evan Gershkovich.

Historia ya kikosi cha Vympel

Chimbuko kamili la Vympel halijulikani lakini kitengo hicho kiliundwa mnamo 1981 na Jenerali wa KGB Drozdov ndani ya Kurugenzi Kuu ya Kwanza ya KGB, kama kitengo cha kujitolea cha spetsnaz kilichobobea katika kupenya kwa kina, hujuma, hatua za moja kwa moja na za siri, ulinzi wa Balozi za Soviet na uanzishaji wa seli za ujasusi katika visa vya vita. Wengi wa wahudumu Vympel walijua lugha mbili au tatu za kigeni kwa vile walikusudiwa kuhudumu katika nchi za kigeni, kwa siri bila kutambuliwa na adui .

Vympel haraka ilipata sifa ya kuwa kati ya vitengo bora zaidi vya vikosi maalum vya Soviet, kuwazidi wenzao wa GRU na MVD. Hata hivyo, baada ya kuanguka kwa USSR, Vympel ilivunjwa .Iliwekwa chini ya uangalizi wa Wizara ya Usalama kabla ya kurejeshwa kwa GUO (taasisi hizo mbili muda mfupi kuwa sehemu ya KGB ya zamani wakati wa enzi ya Boris Yeltsin) na hatimaye kupitishwa kwa MVD (Wizara ya Mambo ya Ndani).

Sehemu kubwa ya maafisa wa Vympel hawakuweza kustahimili aibu ya kuwa chini ya polisi, na walijiuzulu .Kati ya maafisa 278, ni 57 tu waliochagua kubaki ndani ya MVD. Kitengo hicho kilipewa jina la "Vega."

Mnamo 1995, Kituo cha Uendeshaji Maalum cha FSB (TSSN FSB) kilipewa udhibiti wa Vympel. Kikundi hicho kilirejeshewa tena jina lake asili na kuunganishwa tena katika miundo ya Huduma ya Ujasusi. Msisitizo ulihama kutoka kwa shughuli za hujuma za siri na hadi kukabiliana na ugaidi na utekelezaji wa usalama wa nyuklia.

Wahudumu katika kikosi cha Vympel hupitia mafunzo maalum yanayohusiana na vifaa vilivyoboreshwa au maalum vya vilipuzi, vinavyowaruhusu kutumia mbinu "kama za kigaidi" kutekeleza shughuli zao.

Mafunzo ya kimwili yanajumuisha mapigano ya kutukia mikono, mafunzo ya parachuti, kupiga mbizi, mbinu za kupambana chini ya maji, kukwea milima,na mbinu nyinginezo. Vikundi vya kikanda vya Vympel vilitumwa katika miji yenye vifaa muhimu vya nyuklia.

Vympel (yaani Kurugenzi "V" ya TsSN FSB) bado ni kitengo kilichoaratibiwa kama cha siri. Kilishiriki katika kampeni za Chechen za Urusi na kuvamia jengo kuu la Soviet wakati wa mzozo wa kikatiba wa 1993 wa Urusi.Machache yanajulikana kuhusu operesheni na shughuli zake za sasa, isipokuwa ni kutekwa kwa kiongozi wa wanamgambo wa Chechnya Salman Raduyev mnamo Machi 2000 na shambulio la shule huko Beslan mnamo Septemba 2004.

Tafsiri , taarifa ya ziada na maelezo ya kihistoria yameongezwa na Yusuf Jumah