Kwanini Trump anazuru tena mataifa ya Ghuba?

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
- Author, Amir Rawash
- Nafasi, BBC News Arabic
- Muda wa kusoma: Dakika 7
Mahali ambapo Rais wa Marekani anaamua kuzuru katika ziara yake ya kwanza ya nje ya nchi uamuzi muhimu, na mara nyingi huonekana kama mwongozo wa vipaumbele vya sera za kigeni.
Mnamo Mei 2017, Donald Trump alienda kinyume na desturi ya marais wa kisasa wa Marekani, ambao kwa kawaida huchagua kuzuru Canada, Mexico au Ulaya kwanza.
Badala yake, aliamua kutembelea Saudi Arabia yenye utajiri wa mafuta katika safari ya kwanza ya kigeni katika muhula wake wa kwanza kama rais, na baada ya kurejea kwa mara ya pili katika Ikulu ya White House, Trump anarejea tena katika eneo la Ghuba wiki hii (13 - 16 Mei).
Mataifa ya Saudi Arabia, Qatar na Umoja wa Falme za Kiarabu, ziko katika orodha ya kwanza ya ziara ya kigeni ya Trump katika muhula wake wa pili, lakini alifanya safari isiyotarajiwa Vatican mwezi uliopita kuhudhuria mazishi ya Papa Francis.
Hatua ya Trump kuanzia ziara yake katika eneo la Ghuba inatoa ufahamu wa mawazo yake.
Trump anatambua kwamba kukuza uhusiano thabiti na viongozi wa Ghuba kutaleta manufaa makubwa ya kisiasa na kiuchumi, kutokana na ushawishi wao wa kikanda na kimataifa na uwezo wa kusukuma uwekezaji mkubwa nchini Marekani, Profesa Abdullah Baabood, mtafiti wa Oman aliyebobea katika masuala ya Ghuba, aliiambia BBC.
Biashara kubwa
Alipotangaza mpango wake wa awali mnamo mwezi Machi, Trump aliweka bayana kuwa kufikia mikataba ya kiuchumi na nchi tajiri za Kiarabu ni jambo lililopewa kipaumbele, akisema uamuzi huo ulifanywa baada ya kuahidiwa "mabilioni ya dola" na "makampuni ya Kimarekani ambayo yatakuwa yakitengenezea vifaa kwa kwa ajili ya Saudi Arabia na maeneo mengine ya Mashariki ya Kati".
"Kutokana na akiba zao za kifedha, fedha za utajiri huru, na uwezekano mkubwa wa uwekezaji, mataifa ya Ghuba yana jukumu muhimu katika uchumi wa dunia," Profesa Baabood alisema.
Kwa kuzingatia changamoto za kiuchumi nyumbani, Trump anatambua faida za uhusiano wake na mataifa tajiri ya Ghuba, aliongeza.

Chanzo cha picha, Getty Images
Mnamo 2017, Trump alijivunia mikataba yenye thamani ya zaidi ya $450bn - ikiwa ni pamoja na uuzaji wa vifaa vya kijeshi vya thamani ya $ 110bn.
Wakati huu, amekuwa akigonga vichwa vya habari kwa ahadi za mikataba yenye faida kubwa zaidi, akitumai kupata kama dola trilioni moja ($1tn) kupitia uwekezaji na Saudi Arabia.
Ikulu ya Marekani aidha inasema kuwa UAE imejitolea kuweka mfumo wa uwekezaji wa dola trilioni 1.4 ($1.4tn) nchini Marekani kwa zaidi ya miaka 10.
Trump anataka kuonyesha "mafanikio ya haraka" kutokana na ziara hiyo, Hassan Mneimneh, mchambuzi wa Washington anayebobea katika masuala ya Mashariki ya Kati na Marekani, aliiambia BBC.
Rais wa Marekani angependa kupata ahadi hizo za uwekezaji mkubwa - hasa mikataba ya kijeshi - kuzingatiwa haraka iwezekanavyo, alisema, ili aweze kuziwasilisha kama ushahidi wa mafanikio ya sera zake za biashara na nchi nyingine.
Hali tete Mashariki ya Kati
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Mipango ya baada ya vita kwa ajili ya Gaza na mazungumzo ya nyuklia ambayo hayajakamilika na Iran ni miongoni mwa vipaumbele vya sera zakigeni za Marekani, na washirika wa Ghuba pia watanufaika nayo.
Katika siku za kwanza za muhula wake mpya, Trump alishangaza ulimwengu, akisema kuwa nchi yake inataka kuichukua Gaza ili kuigeuza kuwa "Eneo lake la Mashariki ya Kati".
Pendekezo lake lilihusisha kuhamishwa kwa watu milioni 2.1 wa eneo hilo katika hatua ambayo alisema inaweza kugharamiwa na "nchi jirani zenye utajiri mkubwa".
Mpango huo ulikosolewa vikali duniani kote, na mpango mbadala ya Waarabu kujenga upya Ukanda wa Gaza baada ya vita ulikataliwa na Marekani na Israel.
Katika ziara hii, Trump huenda akatafuta fedha kutoka kwa nchi za Ghuba kwa ajili ya juhudi zozote za ujenzi mpya wa eneo hilo lililokumbwa na vita, Prof Baabood alisema, lakini huenda akaangazia masuala ya haraka zaidi.
"Kwa sasa, Trump anatarajiwa kuwahimiza washirika wa Ghuba kusaidia kwanza kukamilisha mpango wa kuachiliwa kwa mateka waliosalia huko Gaza," Prof Baabood anaamini.
Ni lengo ambalo tayari wanashughulikia: Qatar, ni makao ya kituo kikubwa zaidi cha jeshi la anga la Marekani katika eneo la Mashariki ya Kati, imekuwa kiungo muhimu katika mpango wa usitishaji mapigano kati ya Israel na Hamas.

Chanzo cha picha, Getty Images

Chanzo cha picha, Getty Images
Ushawishi wa Ghuba katika migogoro ya kimataifa
Hivi majuzi Marekani imeongeza vikosi vyake katika Mashariki ya Kati huku ikishambulia kwa mabomu kundi la wanamgambo wa Kihouthi nchini Yemen ili kuwazuia kushambulia meli za Bahari ya Shamu.
Wiki moja kabla ya ziara ya Trump, Oman ilianzisha mpango wa upatanishi kati ya Washington na Wahouthi.
Bw Mneimneh anaamini kwamba huenda Riyadh ilihimiza Marekani kusitisha mashambulizi yake ya angani kabla ya ziara yake.
Trump pia ametishia kuishambulia Iran ikiwa haitafanya makubaliano ya nyuklia.
"Kuna njia mbili Iran inaweza kushughulikiwa - kijeshi, au ufanye makubaliano," Trump aliiambia Fox News mwezi Machi, na kuongeza kwamba angependelea "kufanya makubaliano".
Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ilisema katika taarifa tarehe 30 Aprili: "Utawala wa Iran unaendelea kuchochea migogoro katika Mashariki ya Kati, kuendeleza mpango wake wa nyuklia, na kuunga mkono washirika wake wa kigaidi na washirika."
Hata hivyo, pande zote mbili zinaonekana kukwepa vita, huku Oman ikiwa katika mpango wa mazungumzo kati ya Iran na Marekani kuhusu mpango wa nyuklia wa Tehran.
Saudi Arabia imechukua jukumu la kuwa mpatanishi mkuu kati ya Marekani, Urusi na Ukraine.
Mwezi Februari, mkutano wa ngazi ya juu kati ya Marekani na Urusi mjini Riyadh ulijadili mazungumzo ya kumaliza vita vya Ukraine - bila uwepo wa Ukraine. Mkutano huo ulikuwa wa kwanza tangu uvamizi wa Urusi mnamo 2022, na uliashiria mwisho wa juhudi za mataifa ya Magharibi kuitenga Moscow.
Mnamo mwezi Machi ufalme huo ulikaribisha wajumbe kutoka nchi zote tatu katika duru tofauti za mazungumzo kuhusu mzozo wa Ukraine.
Mazungumzo kati ya Marekani na Ukraine mjini Jeddah yalikuwa ya kwanza baada ya majibizano makali kushuhudiwa kwenye moja kwa kwenye televisheni kati ya Trump na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky katika Ikulu ya Marekani mwishoni mwa Februari, na mazungumzo zaidi mjini Riyadh - yaliyotajwa kuwa "ya tija" na Ukraine - yanaweza kusaidia kuboresha uhusiano.
Saudi Arabia na UAE pia zimesaidia kufikia makubaliano ya kubadilishana wafungwa wa kivita wa Urusi na Ukraine.
Mataifa ya Ghuba yamepata "ushawishi mkubwa wa kiuchumi na kisiasa kutokana na jukumu lao katika (mazungumzo kuhusu) migogoro ya kikanda na kimataifa, pamoja na uwezo wao wa kifedha na hifadhi kubwa ya mafuta na gesi asilia," Prof Baabood alisema.
China ambayo ni wapinzani mwingine wa Marekani inatambua umuhimu wa kimkakati wa Ghuba, na hivyo Washington inapenda kudumisha uhusiano imara na washirika wake wa kikanda, aliongeza.
Uwezekano wa kurejeshwa kwa uhusiano kati ya Saudia na Israel
Wakati wa muhula wake wa kwanza, Trump alipata mafanikio ya kihistoria kwa kuwa mpatanishi kati ya Israel na nchi nne za Kiarabu: UAE, Bahrain, Morocco na Sudan.
Vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan vitakatiza mchakato huo, lakini nchi nyingine tatu zilijiunga na Misri na Jordan kama nchi pekee za Kiarabu kuwa na uhusiano wa kidiplomasia na Israel.
Saudi Arabia, ambayo ni kiongozi mkuu katika ulimwengu wa Kiarabu na Kiislamu, bado haijaitambua Israel rasmi.
Afisa wa ngazi ya juu wa Saudia aliiambia BBC mwaka jana kwamba makubaliano yalikuwa "karibu kufikiwa" kabla ya mashambulizi mabaya ya Hamas dhidi ya Israel tarehe 7 Oktoba 2023.
Lakini baada ya Trump hivi majuzi kupendekeza kwamba Saudi Arabia inaweza kusaidai kuanzishwa kwa taifa huru la Palestina kama sharti la makubaliano, ufalme huo ulikariri kuwa "hakutakuwa na uhusiano wa kidiplomasia na Israeli bila" uwepo wa taifa huru la Palestina.
Wachambuzi wanaamini kuwa kurejesha uhusiano na Israel kumezidi kuwa na utata kwa Riyadh.
Huku vita vya Gaza vikiwa bado vinaendelea, Saudi Arabia haionekani kuwa tayari kujadili suala hili wakati wa ziara hiyo, Profesa Baabood alisema.
Trump anatarajiwa kuendelea kutekeleza mikataba ya kurejesha uhusiano kati ya Israel na nchi za ziada za Ghuba, aliongeza, lakini makubaliano yoyote ya baadaye kati ya Israel na Saudi Arabia yataashiria hatua muhimu zaidi.
Imetafsiriwa na Ambia Hirsi












