Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
'Natumai Assad atalipa', asema mama ambaye kifo cha mwanawe kilichochea mapinduzi ya Syria 2011
Msukumo wa kumwondoa Bashar al-Assad madarakani ulizaliwa huko Deraa, mji mdogo nchini Syria karibu na mpaka wa Jordan.
Tarehe 21 Mei 2011, mwili ulioteswa na kukatwa viungo vya Hamza al-Khatib mwenye umri wa miaka 13 ulifikishwa kwa familia yake wiki kadhaa baada ya kukamatwa katika maandamano ya kuipinga serikali.
Kifo chake, na kuteswa kwa vijana wengine wa eneo hilo kwa kuandika maandishi ya kumpinga Assad, kulizua maandamano makubwa na ukandamizaji mkali wa vikosi vya serikali.
Ikiwa mtu yeyote katika Deraa anapaswa kusherehekea kuanguka kwa utawala wa Assad, ni familia ya Khatib.
Lakini tulipotembelea leo, hakuna mtu katika nyumba hiyo aliyekuwa akisherehekea.
Walikuwa wametumwa tu picha za skrini za hati zilizopatikana katika gereza maarufu la Saydnaya zilizothibitisha kwamba kakake Hamza Omar, ambaye pia alikamatwa na polisi mnamo 2019, alikufa kizuizini.
Mama wa wavulana, Samira, akitetemeka kwa huzuni, aliniambia alikuwa akimngoja Omar atoke gerezani.
"Nilikuwa nikifikiria labda atakuja leo au kesho," alisema. "Leo, nimepata habari."
Akiwa amevalia mavazi meusi, na tayari akimuomboleza mumewe, ambaye alifariki chini ya miezi mitatu iliyopita, alimwomba Rais wa zamani Bashar al-Assad mwenyewe ayapitie kama aliyoyapitia kwenye maisha yake.
"Natumai atalipa ," alisema. "Na kwamba Mungu atamlipizia kisasi yeye na watoto wake."
Mpwa wake, Hossam al-Khatib, alisema nyaraka hizo zilichapishwa kwenye mitandao ya kijamii, na watu waliokuwa wakimsaka Saydnaya ili kupata taarifa kuhusu jamaa zao. Walilikuta faili la Omar na kulisambaza mtandaoni huku wakijua kuwa ni kaka yake Hamza.
Kuanguka kwa Assad kumeondoa ukandamizaji wa miongo kadhaa nchini Syria, na sehemu kubwa ya watu wa Deraa walikuwa mitaani siku ya Jumapili, ikiwa na furaha kubwa, wakati wapiganaji wa waasi wapoliteka mji mkuu Damascus na Assad kukimbia.
Picha za simu za mkononi zinaonesha umati wa wanaume wakikimbia kuzunguka uwanja wa Deraa wakiwa katika furaha tele, wakipiga kelele na kurusha silaha angani.
Eneo hili lilikuwa kitovu kikuu cha upinzani wakati wa utawala wa Assad, vita vikali vimekita katika shule na nyumba hapa, kijiji baada ya kijiji kilichoharibiwa na mizinga na milio ya risasi.
Upinzani katika eneo hili la kusini mwa Syria ni tofauti na muungano unaoongozwa na kundi la wanamgambo wa Kiislamu Hayat Tahrir al-Sham (HTS), ambao ulienea kutoka kaskazini na kuchukua mji mkuu wiki iliyopita. Lakini wote wawili walikutana kwenye mji mkuu siku ya Jumapili.
Jeshi Huru la Syria (FSA) lilianza mapigano hapa mwaka 2011, wakati ukandamizaji mkali wa serikali baada ya kifo cha Hamza ulipowashawishi baadhi ya maafisa wa jeshi la Assad kuasi na kuunda kikosi cha waasi.
Mmoja wao alikuwa Ahmed al-Awda, mshairi ambaye alisoma fasihi ya Kiingereza katika chuo kikuu kabla ya kuwa afisa wa jeshi, na kisha kiongozi wa waasi, sasa kiongozi wa wanamgambo wa Mkoa wa Deraa.
"Huwezi kufikiria jinsi tulivyo na furaha," aliniambia katika mji wa karibu wa Busra.
"Tumekuwa tukilia kwa siku nyingi. Huwezi kufikiria tunachohisi. Kila mtu hapa Syria alipoteza familia. Kila mtu alikuwa akiteseka."
Bw Awda alisema alikuwa miongoni mwa watu wa kwanza kuingia Damascus siku ya Jumapili, pamoja na HTS.
Jambo la kwanza alilofanya, aliongeza, ni kwenda kwenye balozi na majengo ya serikali, ili kuwalinda watu waliokuwa ndani.
"Tulipeleka vijana wengi wa serikali ya kiraia kwenye hoteli ya Four Seasons, na kuweka kikosi kikubwa sana huko kuwalinda," alisema.
Lakini anasema hatamsamehe Assad kirahisi hivyo.
"Nitajitahidi niwezavyo kumpeleka kwenye hukumu mahakamani, kwa sababu hatutasahau alichowafanyia watu wa Syria, na jinsi alivyoiangamiza Syria."
Kuna wasiwasi kwamba Syria inaweza kufuata njia ya Iraq na Libya na kugawanyika katika machafuko.
"Tuliona kilichotokea Iraq na tunakataa," Bw Awda alisema.
Vikosi vya Assad sio pekee vilivyokuwa vikipigana hapa katika miaka michache iliyopita. Washirika wa kundi la Islamic State (IS), ambao bado wametawanyika mashariki mwa nchi, pia walikuwa tishio.
Bw Awda anasema alipigana nao, na kumuua kiongozi mkuu wa IS, Abu Ibrahim al-Qurayshi, miaka miwili iliyopita.
Sasa anataka uchaguzi huru, akiamini kwamba watu wa Syria hawatamchagua tena mtu yeyote ambaye atakuwa dikteta.
Katika makaburi ya Deraa, bamba kwenye kaburi la Hamza liko vipande vipande - lililovunjwa na shambulizi la vikosi vya serikali wakati wa mapigano na vikosi vya waasi hapa, familia ilisema.
"Waliendelea kumpiga hata alipokuwa amekufa," binamu mmoja alisema.
Majirani walitazama kwa ukimya wakati bendera ya upinzani ya Syria ikifungwa kwenye jiwe la kichwa la Hamza.
Nyuma yake, makaburi yanasimulia hadithi ya miaka 13 ya mapigano: shambulio la anga, vita, familia nzima iliyouawa nyumbani kwao.
Vita na Assad vimeisha lakini amani nchini Syria bado haijapatikana.
Imetafsiriwa na Lizzy Masinga