'Maswali ni mengi uhaba wa pombe Zanzibar'

FD
    • Author, Alfred Lasteck
    • Nafasi, BBC Swahil

”Kuna matatizo yanayoweza kutokea na matatizo hayo wala si lazima usababishe wewe na pale ambapo hukubaliani na Serikali sema, na kuwa muwazi tutakuheshimu zaidi, kama una baa watu wamezuia pombe sema mimi nina baa inaingiliana na maslahi yangu, kuwa muwazi,” alisema Rais wa Zanzibar, Dkt. Hussein Mwinyi.

Hali hii inakuja ikiwa ni mwaka jana tu, tangu kisiwa hicho chenye mamlaka ya ndani, kilipoorodheshwa na majarida mbalimbali kuwa kati ya vivutio 10 bora vya utalii barani Afrika.

Watalii wengi hufika visiwani huko kwaajili ya mapumziko na sasa wengi huenda wakakumbana na uhaba wa pombe katika mahoteli, migahawa na sehemu za starehe.

Akizungumza jana wakati wa uapisho wa wateule, Rais Mwinyi alikosoa hatua wanazochukua viongozi pale wanapotaka kujiuzulu katika nyadhifa zao.

Alizungumza hayo baada ya aliyekuwa Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale, Simai Mohammed Said kurekodi video fupi akitangaza kujiuzulu nafasi yake ya Uwaziri, akisema mazingira ya kutekeleza jukumu hilo yamekuwa magumu.

Kujiuzulu kwake kulikuja zikiwa zimepita siku kadhaa tangu alipoviambia vyombo vya habari kuwa kuna sintofahamu zimeanza kujitokeza na athari zake zinarudisha nyuma biashara ya Utalii Zanzibar, baada ya uwepo wa uhaba wa pombe katika Hoteli na Migahawa.

Pia Unaweza Kusoma

Upatikanaji wa Pombe

Upatikani wa Pombe visiwani humo bado ni changamoto huku ukitishia sekta ya utalii. Uhaba huo huenda ukaathiri shughuli za kitalii kwani wageni wengi hufika visiwani humo mara kwa mara.

Utalii huingiza takribani 90% ya mapato yatokayo nje lakini kwasasa bei ya bia imepanda kwa karibu 100% baada ya kusitishwa kwa leseni kwa kampuni zilizokuwa zikingiza vinjwaji kwenye visiwa hivyo.

Wamiliki wa hoteli wanaonya kwamba mabadiliko ya ghafla ya kampuni za uingizaji pombe yanaweza kufanya kisiwa hicho kupoteza baadhi ya watalii.

Hata hivyo, upungufu wa pombe unatajwa kusababishwa na maamuzi ya mamlaka ya kudhibiti vileo visiwani Zanzibar (ZLCB), ya kutotoa leseni kwa kampuni tatu za uingizaji pombe ambazo ni - One Stop, Scotch Store na ZMMI.

Kwanini leseni hazikutolewa?

SX

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES

Haijabainika ni kwa nini leseni zkwa makampuni hayo matatu, ambayo yalikuwa yakisambaza pombe kisiwani humo kwa zaidi ya miongo miwili hazijatolewa.

BBC ilitafuta mamlaka husika kuthibitisha sababu za kutopewa leseni lakini viongozi husika hawakuwa tayari kuzungumza.

Ifahamike kuwa ili muingizaji pombe apewe leseni, ni lazima mmiliki awe Mzanzibari mkazi, mwenye rekodi safi ya ulipaji kodi na miundombinu tosheleza ya kufanya shughuli hiyo.

Zaidi ya hayo, waagizaji ili kupewa leseni mpya lazima pia walipe ada ya kila mwaka ya dola za kimarekani 12,000 kwa bodi ya udhibiti.

Kampuni mpya ni zipi?

Mwezi uliopita, ZLCB ilitoa leseni kwa makampuni matatu mapya - Kifaru, Bevko na Zanzi Imports - lakini wamiliki wa hoteli wanasema bado hawajaweza kuwafikia.

Makampuni hayo mapya yanaripotiwa kuwa hayajajipanga na kwamba itawachukua muda kuweza kukidhi mahitai ya pombe visiwani humo.

Na yale makampuni ambayo hayajapata leseni, yanadai kukata rufaa huku wakieleza kuwa hali ni mbaya kwenye soko

"Tunahitaji hatua za haraka za serikali kabla ya maduka yetu kuwa matupu. Uhaba umesababisha kupanda bei ya bia," Arvind Asawla, Mkurugenzi Mkuu wa Scotch Store Limited, aliiambia tovuti ya serikali ya Daily News.

Uhaba uko wapi zaidi?

D

Uhaba mkubwa unaripotiwa kuwa katika hoteli za kitalii katika mkoa wa Unguja Kaskazini na Kusini na baadhi ya maeneo ya Mjini Magharibi.

"Kuna uhaba wa pombe Zanzibar na tayari tumeziarifu mamlaka kuhusu hali ya sekta ya utalii," Rahim Mbarouk, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Uwekezaji wa Utalii Zanzibar aliiambia BBC.

Neema Meena anasema, “bei ya bia imepanda kutoka Tsh 2,500 (1$) hadi Sh5,000 (dola 2). Baadhi ya bia kama Safari, Kilimanjaro zimeadimika na kama ukizipata basi ni kwa bei ya juu.”

Vilio kila kona

Katibu wa Umoja wa Wafanyabiashara ya vileo eneo la Amani, Frank Kahamu amesema vileo ni shida na vimekuwa adimu.

Kahamu alisema kuwa atalazimika kuwaachisha kazi zaidi ya wafanyakazi 3,000 iwapo hali hiyo itaendelea. Alisema alilieleza gazeti la ‘The Citizen’ kuwa, "hatuwezi kuendelea kulipa mishahara kwa hali hii."

Hata hivyo Mwenyekiti wa Bodi ya Vileo visiwani humo, Juma Chum alikataa kujibu hali ilivyo wakati BBC ilipomtafuta kufahamu hali ya mambo.

Tatizo lilipoanzia

C

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Waziri wa zamani wa Utalii, Simai Mohammed Said aliyejiuzulu siku kadhaa zilizopita, alitaja sababu kuwa ni “mazingira yasiyo rafiki katika kazi.”

Katika mkutano na waandishi wa habari aliishutumu hadharani ZLCB kwa kusimamia vibaya jukumu la vileo.

Alisema, "tukishindwa kupanga, ikiwa ni pamoja na kuwa na akiba ya kutosha ya vileo, tunakatisha tamaa wageni wetu," alisema wakati wa mkutano huo na waandishi wa habari.

Lakini wakati akimuapisha waziri mpya wa utalii siku ya Alhamisi, Rais Mwinyi alimshutumu Said kwa mgongano wa kimaslahi, alipokuwa akihudumu katika wizara hiyo.

“Kama una baa, ukagundua mamlaka haijatoa huduma ya pombe kwenye baa yako, basi uwe muwazi na uwaambie wananchi kuwa kuna mgongano wa kimaslahi,” alisema Rais Mwinyi.

Mgogoro huo unakuja huku kukiwa na ongezeko la watalii wanaowasili katika kisiwa hicho. Mwaka jana, Zanzibar ilishuhudia ongezeko la watalii kutoka mataifa ya kigeni kwa asilimia 16, huku idadi ikifikia watalii zaidi ya 630,000.