Msumbiji: Je, unazijua mbinu zinazotumika kukabiliana na vimbunga?

Chanzo cha picha, Nomsa Maseko/BBC
- Author, Nomsa Maseko
- Nafasi, BBC
Mjenzi wa Msumbiji, José Joaquim amedhamiria kutoiweka tena familia yake katika hofu wakati wa kimbunga katika nyumba iliyochoka.
Wakati kimbunga Idai kilipopiga kwenye ufuo wa Msumbiji miaka mitano iliyopita, alikuwa akiishi na mke wake na mtoto mchanga katika mji wa Beira.
"Upepo ulipokuwa mkali, tulikuwa ndani. Kwa sababu ya kelele hatukujua nini kinaendelea nje. Lakini ghafla upande mmoja wa paa uliezuliwa," Joaquim aliambia BBC.
"Na kisha mlango wetu ulipasuka katikati kwa sababu ya upepo. Tuligundua sasa tunapaswa kuondoka."
Walihangaika katika upepo mkali uliokuwa ukiwaangusha hadi wakafika katika kituo cha kuhifadhi watu katika shule. Kwa usalama watu walikaa chumba kimoja kilichokuwa na dari imara hadi upepo ulipopungua.
"Kama baba nilihisi jukumu la kumlinda mtoto wangu na mama yake, na namshukuru Mungu! Nilifanya uamuzi wa busara kuondoka na kutelekeza nyumba ili niweze kuokoa familia yangu," kijana huyo wa miaka 27 anasema.
Idai ilisababisha uharibifu mkubwa na hasara. Watu 1,500 walifariki na wengine milioni tatu waliathiriwa katika nchi tatu.
Tangu wakati huo dhoruba zingine zimepiga eneo hilo na kwa mabadiliko ya hali ya hewa, wanasayansi wanatabiri dhoruba zitakuwa na nguvu na hatari zaidi.
Hili linaweza kuwa tatizo kwa nchi hiyo yenye ufuo wa tatu kwa urefu katika Bahari ya Hindi.
Nyumba za Kukabiliana na Vimbunga

Chanzo cha picha, Nomsa Maseko/BBC
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Wakati wowote mawingu yanapokusanyika, watu katika eneo hili hupata wasiwasi kuhusu uwezekano wa mafuriko mabaya yanayoletwa na vimbunga vya kitropiki.
Hilo limewalazimu watu, kama Joaquim, kujenga nyumba imara na kujifunza mbinu za kujiokoa.
Alikuwa akisomea uhandisi wa ujenzi wakati wa Idai, lakini baada ya kunusurika na kimbunga hicho, Joaquim alijiunga na kozi ya ujenzi imara iliyotolewa na chuo kiitwacho Young Africa.
Amehitimu lakini amerudi chuoni kufundisha wanafunzi wapya. Kundi la wanafunzi wa ujenzi waliovalia nguo za usalama wamekusanyika karibu na nyumba ndogo.
Wanajifunza jinsi ya kujenga paa ambayo imeundwa mahususi kustahimili upepo mkali na mvua kubwa inayotokana na vimbunga.
"Kwa sababu ya hatari ya paa kuezuliwa, tunatumia vyuma ili kuimarisha paa," Joaquim anasema.
"Kwa mbinu hizi za ujenzi, tunaamini itaweza kuhimili nguvu ya upepo na mvua kubwa kama ya wakati wa Kimbunga Idai."
Kama sehemu ya kozi yake, Joaquim aliisaidia Young Africa kujenga zaidi ya nyumba 130 katika maeneo mawili, zote zimejengwa kutoa ulinzi wakati wa kimbunga kikali. Nyumba hizi ni kwa watu waliopoteza nyumba zao wakati wa kimbunga.

Chanzo cha picha, Nomsa Maseko/BBC
Joaquim sasa anatumia ujuzi wake, kujenga nyumba za watu wengine katika jamii yake na familia yake mwenyewe. Alinionyesha nyumba yake ambayo anatarajia kuikamilisha kabla ya msimu ujao wa kimbunga.
"Mimi na familia yangu tutakuwa salama," ananiambia.
Nyumba hutoa ulinzi lakini baadhi ya maeneo karibu na mji wa pwani wa Beira - watu huhitajika kuhama wakati kimbunga kikali kinapotabiriwa.
Halmashauri ya mtaa imeunda kamati za mitaa za ushughulikiaji maafa. Ni watu wa kujitolea ambao hufanya kazi mwaka mzima ili kuandaa jamii inapokuja dharura na kuwasaidia kuhama kwa usalama.
Upandaji wa Mikoko

Chanzo cha picha, Nomsa Maseko/BBC
Katika mji wa Praia Nova, kitongoji cha wavuvi karibu na bahari. Nilikutana na mmoja wa wafanyakazi wa kujitolea ambaye husaidia uokoaji wakati wa matukio ya dhoruba.
"Tunafanya kazi pamoja wakati wowote kunapotokea dharura. Hasa vimbunga vinapotokea ghafla, tuko katika jamii tukifanya," anasema Liria Charomar.
Anajua umuhimu wa uhamishaji watu. Niliona kovu kwenye mguu wake - anasema amelipata wakati kuwavuusha watu kwenye maji mengi wakati wa Kimbunga Idai.
"Kulikuwa na mabati mengi chini ya maji lakini sikuweza kuyaona, na wakati nainua mguu, bati moja lilinikata," anaeleza.
Njia moja ya kuweka ulinzi katika maeneo hatarishi ya pwani ni kupanda miti ya mikoko ambayo imekatwa kwa miaka mingi kwa ajili ya ujenzi na kuni.

Chanzo cha picha, Nomsa Maseko/BBC
Kati ya kijiji cha Nhangau, takribani saa moja kwa gari kutoka pwani ya Beira tunakutana na Alberto Santos anaefanya kazi na watu wengine wa kujitolea kupanda miti upya.
"Mikoko hutumika kama kizuizi cha upepo," anasema Santos.
"Upepo mkali hutoka baharini, kwa sababu vimbunga vyenyewe vinatoka baharini lakini msitu wa mikoko huzuia upepo mkali."
Chama chake cha upandaji miti kimepanda hekta 1,300 (ekari 3,212) ya mikoko katika kipindi cha miaka 15 iliyopita.
Mabadiliko ya Tabia Nchi

Chanzo cha picha, Nomsa Maseko/BBC
Ukweli ni kuwa Msumbiji imezalisha kiasi kidogo tu cha gesi chafu inayosababisha mabadiliko ya tabia nchi na mabadiliko ya hali ya hewa.
“Wakazi wa Beira hawafurahishwi na hali hii inayosababishwa na mataifa mengine,” anasema Bi Charoma.
“Hapa Msumbiji tayari tuko kwenye matatizo, tuna matatizo makubwa kama vimbunga vikali na nchi hizo bado zinafanya mambo yasiyofaa. Haisaidii kwa yeyote. Wanapaswa kutuacha tuishi kama tulivyokuwa tukiishi zamani."
Watu wa Beira wataendelea kufanya wawezalo kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi, kujianda na siku za usoni zisizo na uhakika.
"Siku zote kuna utashi wa kutafuta suluhu. Kwa hivyo, kuwa sehemu ya suluhisho ni muhimu kwangu, na nadhani ni muhimu kwa watu wengine pia," anasema Joaquim.
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Ambia Hirsi












