Wasyria watafuta miili ya wapendwa wao wawazike baada ya miaka 50 ya udikteta wa Assad

- Author, Jeremy Bowen
- Nafasi, BBC World Affairs Editor
- Muda wa kusoma: Dakika 7
Katika ukuta wa nje ya Hospitali ya Al-Mujtahid huko Damascus, picha za nyuso za wanaume waliokufa zimebandikwa.
Umati kutoka maeneo tofauti tofauti unamiminika hapa kuchunguza na kukagua picha hizi, jua likiwa utosini huku wakiwa na matumaini watapata miili ya wapendwa wao.
Miili hiyo ambayo imehifadhiwa kwa sasa ikiletwa katikati mwa jiji kutambuliwa na familia zao.
Madaktari wanasema kuwa wote waliokufa walikuwa ni wafungwa katika gereza la seydanaya.
Makundi ya watu wakiwa wamejawa na huzuni nyusoni mwao wanamiminika katika hospitali hii wakitafuta taarifa za wapendwa wao waliopotea katika hali tatanishi, huku wengine wakijipanga kuchukua miili ya wapendwa wao wakawazike.
Waking'ang'ania kufikia orodha iliyobandikwa ukutani wengine wanapiga picha ili warudi nyumbani wakapate uhakika kamili kuwa ni mpendwa wao.
Ni mchakato wa kusikitisha na kuchosha.
Baadhi ya wanaume wanaonekana walifariki muda mrefu uliopita, kulingana na picha za nyuso zao ambazo hazitambuliki kwa haraka.
Wakitoka katika ukuta huo uliobandikwa picha za walioaga wanaelekea katika makafani kutambua mwili ili wauchukue.

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Hospitali ya Al-Mujtahid ilipokea miili 35, idadi kubwa ambayo ilisababisha chumba cha maiti kujaa pomoni na chumba kilichotengwa kwa miili kilizidi uwezo wake kwa kujaa magari yaliyobeba maiti.
Ndani ya chumba cha maiti, miili ililazwa kwenye sakafu kwa mabomba ya friji ili kuhifadhi miili hiyo.
Baadhi ya miili ilikuwa imefunikwa kwa sanda zinazozidi kufunguka na kuning'inia na kufichua nyuso, michoro ya chale au makovu ambayo inaweza kuwatambulisha waliofariki.
Kati ya maiti zilizofikishwa katika hospitali hii mmoja wao alikuwa amevaa nepi, na mwingine alikuwa na utepe kwenye kifua chake ikiwa imeandikwa nambari.
Hata baada ya kuuawa, waangalizi wa magereza hawakubandika jina lake ili atambuliwe kiurahisi.
Miili yote ilikuwa imedhoofika.
Madaktari ambao walikagua miili hiyo wanasema ilikuwa na alama za kuadhibiwa na kuvunjwa mifupa.
Kulingana na Raghad Attar, mtaalam wa meno, amekuwa akikagua rekodi zilizotolewa na familia ili kutambua waliofariki kupitia mpangilio wa meno ambao huwa sawia katika familia.
Anasema amekuwa akikusanya ushahidi ambao ungetumika katika mchakato wa kutambua miili kupitia msimbojeni, na nilipomuuliza kuhusu hisia kutokana na kile anachokifanya alianza kububujikwa na machozi.
''ilikuwa ni kawaida kusikia wafungwa wamepotea kwa muda mrefu, pindi unapowaona unaskia uchungu mwingi'', anasema Raghad.
''Nilikuja hapa jana, ilikuwa hali ya kusikitisha. Tunatumai kuwa siku zijazo zitakuwa bora, lakini hii ni ngumu sana. Najisikia huzuni sana kwa familia hizi,'' anaongezea.
Machozi yalianza kumtiririka nilipomuuliza iwapo Syria itaweza kupona baada ya miaka 50 ya utawala wa familia ya Assad.
"Sijui," alisema, "lakini natumai itatokea. Nahisi tutakuwa na siku bora, lakini nataka kuomba nchi zote kutusaidia."
"Chochote cha kutusaidia. Chochote, chochote…"
Familia na marafiki wanaingia polepole katika makafani haya, wakitembea kimya kimya kutoka kwa mwili mmoja hadi mwingine kwa matumaini watafarijika tangu kuwapoteza wapendwa wao waliochukuliwa na kuingizwa katika gereza la Assad.
Mwanamke kwa jina Nour, aliyevaa barakoa kuficha uso wake, alisema nduguye alikamatwa mwaka 2012 akiwa na miaka 28.
Walichokijua kumuhusu kaka yake ni kupitia mtandao wa Facebook ambao ulieleza amezuiliwa katika gereza la Saydnaya ambalo lilikuwa chini ya ulinzi wa wanajeshi wa Assad.
''Hali nii inahuzunisha.''Nour anasema.
''Wakati huo huo pia tuna matumaini. Hata kama tutampata ni miongoni mwa waliofariki. Ilimradi asikosekane. Tunataka tujue alichokipitia, na hali yake angalau roho zetu zitulie.
Kwa upande mwingine, familia hii ilimuelezea daktari kuwa kijana wao alikamatwa baada ya kukataa kufungua tarakilishi ichunguzwe na mamlaka.
''Ilikuwa ni miaka 12 iliyopita. Tangu siku hiyo hatujasikia chochote kumhusu na pia kutoka kwake'', familia inasema.
Kwa miaka mingi ambayo nimekuwa nikiripoti matukio nchini Syria, taarifa kama hizi zimejitokeza kwa wingi.
Katika simu yangu, nina picha ya uso wa mwanamke niliyemkuta mwezi Julai 2018 kwenye kambi ya wakimbizi, baada ya waasi kujisalimisha katika ngome yao ya Douma pembezoni mwa Damascus.
Mtoto wake mdogo alikosekana baada ya kukamatwa kwenye kizuizi cha huduma za ujasusi.
Zaidi ya miaka 50 ya utawala wa familia ya Assad inamaanisha miaka 50 ya kupotea usijulikane uliko, kifungo, na mauaji.
Inamaanisha pia ukatili usio na huruma kwa wafungwa, kwa familia zinazojitahidi kuwaona, na kwa watu wa Syria ambao walikuwa hawana ukuruba na familia ya Assad.
Katika ukuta uliobandikwa picha katika ua la makafani ya hospitali ya Al-mujtahid, watu walijaa kujua kilichowasibu wapendwa wao.
Walitaka kujua hali ya wapendwa wao na kikubwa zaidi ni miili ya wapendwa wao waliopotea.
Wengi wana hasira huku wengine wakitaka kulipiza kisasi.
Waliosimama kwa vikundi walipiga moyo konde wakiwa na matumaini wataishi bila uoga maisha ya usoni.
Kasri la Rais

Dereva wetu wa BBC pia alikusanya ushahidi wake wa video.
Alitoa simu yake na kuanza kurekodi videowakati gari lilipokuwa likielekea kwenye lango refu la kasri la kifalme.
Wakati wa utawala wa serikali hii, Wasyria walikuwa waangalifu kutokupunguza kasi ya magari yao karibu na milango ya kifalme kwa hofu ya kukamatwa na kutupwa gerezani ikiwa mamlaka zingedhani wanawakilisha tishio kwa rais.
Simu za mkononi hupoteza intaneti na kukosa kufanya kazi wanapokaribia eneo la usalama la kasri la kifalme.
Kasri hiyo inatazama Damascus na inaweza kuonekana kutoka sehemu kubwa za jiji.
Ikiwa na jazanda kuwa familia ya Assad imekuwepo na inawapiga darubini kupitia mtandao wa huduma za ujasusi wa utawala.
Mfumo huu ulianzishwa na Hafez, rais wa kwanza wa familia ya Assad. Polisi wake wa siri walikuwa wakichunguza kila raia nchini humo.
Mjasiriamali mmoja ninayemjua huko Homs aliniambia kuwa kuna wakati idara ya ujasusi ilimjia alipokuwa akijenga hoteli, na walimwomba michoro ya hoteli mapema katika mradi ili waweze kuingiza vifaa vya kusikilizia walivyohitaji katika vyumba.
Walimwambia kuwa hii ingekuwa rahisi kuliko kuweka vifaa hivi baada ya ujenzi kumalizika.
Familia ya Assad haikuwahi kuishi kwenye kasri la kifalme.
Ilikuwa imehifadhiwa kwa sherehe rasmi, na kulikuwa na baadhi ya ofisi kwenye ghorofa za juu kwa ajili ya biashara za kila siku.
Nilikwenda mara nyingi huko mwaka 2015, ili kujadiliana masharti ya mahojiano na Bashar al-Assad. Nilikutana naye mara mbili kabla ya mapinduzi dhidi yake kuanza mwaka 2011.
Wakati huo, alikuwa bado akiwasimulia mikakati ya mwamko mpya kwa Wasyria, ambayo yaligeuka kuwa ni hadaa.
Aliongoza viongozi wa Magharibi kuamini kuwa angeweza kuvunja uhusiano na Iran, na kama asingeliungana kikamilifu na mataifa ya Magharibi, wangeweza kumshawishi kuwa ni kwa faida yake kutokupinga.
Marekani, Israel na mataifa ya uarabuni walikuwa wakijaribu kumshawishi aachane na Iran ndani ya wiki kabla hajalazimika kutoroka hadi Moscow.
Kuondoka kwa Assad, kunanikumbusha eneo nililolitembelea katika kasri hili la kifalme ili kumfanyia mahojiano Bashar al- Assad.
Kasri hilo ambalo ni la kifahari kando na kuwa kasri ya rais pia ilikuwa imejengwa na madhumuni ya kuwa makaazi ya familia ya Assad.
Familia ya Assad imeitawala Syria kama mali yake tangu vizazi vyake vya awali, ikijitajirisha na kununua uaminifu wa wafuasi wake kwa gharama ya Wasyria ambao wangeweza kufungwa au kuuawa ikiwa hawangekubaliana na utawala wa Assad, au hata kama hawakufanya hivyo.
Kulipiza kisasi

Chanzo cha picha, Getty Images
Mpiganaji kwa jina Ahmed, aliyechukua silaha dhidi ya utawala wa Assad mwaka 2011, alikwepa kushindwa kwa waasi huko Damascus, na kisha alijikuta akirudi kutoka Idlib akiwa na wanamgambo wa Hayat Tahrir al-Sham, akifikiria maisha ya familia ya Assad, akiwa na ndugu zake watatu, wote wakiwa wapiganaji wa kundi la waasi.
"Watu walikuwa wakiishi maisha duni huku Bashir akiogelea kwa ubwenyenye na ukasi wa kupitiliza,''alisema Ahmed kwa sauti ya chini.
"Hakuwa na haja ya kujali kilichokuwa kinawasibu raia wake. Aliwafanya kuishi kwa hofu, njaa na aibu. Hata baada ya sisi kuingia Damascus, watu walikuwa wakitunong'onezea wakiwa bado na hofu," aliongeza.
Nilipitia nyumba ya wageni iliyopambwa kwa marumaru, na kufunguliwa milango ya kifahari ambapo nilikutana na Assad wakati utawala uliponea chupuchupu kuondolewa mamlakani mwezi Februari mwaka 2015.
Jambo kubwa zaidi kuhusu mahojiano hayo lilikuwa kukataa kwake mara kwa mara kwamba vikosi vyake vilikuwa vikiua raia. Alijaribu hata kutania kuhusu hilo.
Sasa, wapiganaji wa upinzani wanasimama mlangoni na kutembea kwenye ushoroba wa kasri hilo. Baadhi ya vitabu vilikuwa vimeanguka kutoka kwenye rafu za maktaba, lakini jengo liko salama.
Nilitembea hadi chumba cha kusubiri ambapo Assad alikuwa akitoa mazungumzo ya dakika 10 au 15 kabla ya mahojiano.
Alikuwa daima mkarimu, mwenye huruma, akiniuliza kuhusu familia yangu, na safari yangu kwenda Syria.
Tabia ya Bashar al-Assad kuonekana mpole imesababisha baadhi ya waangalizi wa Magharibi kuamini kuwa yeye ni mtu dhaifu ambaye anaweza kunyenyekea.
Kwa siri, nilimwona akiwa na kujiamini hadi kiwango cha majivuno, akijua kila kitu lililola siri na wazi katika mtandao wa Mashariki ya Kati, akifuatilia nia mbaya za maadui zake na tayari kufanya shambulizi.
Imetafsiriwa na Mariam Mjahid












