Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Trump apinga mpango wa Israel wa kunyakua maeneo ya Palestina
Afisa wa Ikulu ya White House amethibitisha kwamba Rais wa Marekani Donald Trump anapinga mpango wa Israel wa kunyakua maeneo ya Palestina katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu.
Afisa huyo alisema Jumatatu jioni: "Utulivu katika Ukingo wa Magharibi unadumisha usalama wa Israeli na unaendana na lengo la utawala huu la kufikia amani katika eneo hilo."
Rais wa Mamlaka ya Palestina Mahmoud Abbas amemtaka Rais Trump "kuthibitisha tena kutounga mkono unyakuzi huo" siku moja baada ya Israeli kutangaza maamuzi mapya yanayolenga "kuimarisha unyakuzi wa ardhi katika Ukingo wa Magharibi."
Wakati wa mkutano wake na Mfalme Abdullah wa Pili wa Jordan huko Amman, Abbas alionya kuhusu "uzito wa maamuzi haya na athari zake kwa usalama na utulivu katika eneo hilo, hasa kutokana na kulengwa kwa maeneo matakatifu ya Kiislamu na Kikristo, na mwezi mtukufu wa Ramadhani unapokaribia," kulingana na Shirika la Habari la Palestina "WAFA."
Abbas alisema anamwomba rais wa Marekani "kuthibitisha tena ahadi ya kuzuia unyakuzi, ahadi iliyotolewa na Marekani Septemba iliyopita wakati wa majadiliano ya mpango wa Rais Trump kuhusu Gaza na viongozi wa nchi za Kiarabu na Kiislamu huko New York.
Tangazo la hatua hizo za Israeli linakuja siku chache kabla ya ziara ya Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu nchini Marekani wiki hii.
Kulingana na shirika la habari la Palestina WAFA, Abbas na Mfalme Abdullah walilaani vikali maamuzi ya hivi karibuni ya baraza la mawaziri la utawala wa Israel yanayolenga kuimarisha unyakuzi katika Ukingo wa Magharibi na kupanua makazi.
Pande zote mbili zilithibitisha kwamba hatua hizi "ni ukiukaji mkubwa wa sheria za kimataifa, na zinalenga kudhoofisha taifa la Palestina na suluhisho la mataifa mawili."
Hatua mpya za Israel
Siku ya Jumapili, Baraza la Mawaziri la Usalama la Israe liliidhinisha hatua zinazolenga kuimarisha udhibiti wa Ukingo wa Magharibi, na hivyo kufungua njia ya "upanuzi zaidi wa makazi" katika maeneo ya Palestina.
Hatua zilizotangazwa na Waziri wa Fedha Bezalel Smotrich na Waziri wa Ulinzi Israel Katz ni pamoja na kuondoa sheria za muda mrefu zinazowazuia Wayahudi kununua ardhi katika Ukingo wa Magharibi.
Hatua hizo pia zinajumuisha kuhamisha mamlaka ya kutoa vibali vya ujenzi wa makazi katika sehemu za miji ya Palestina, ikiwemo Hebron, kutoka manispaa ya Mamlaka ya Palestina hadi Israeli, jambo ambalo linaonekana kuwa ni juhudi za kurahisisha shughuli za makazi katika eneo hilo, kulingana na vyombo vya habari vya Israel.
Tovuti ya Times of Israel iliripoti kwamba sera ya ujenzi hapo awali ilihitaji idhini kutoka kwa manispaa ya eneo hilo na mamlaka ya Israeli. Chini ya taratibu mpya, ujenzi utahitaji idhini ya Israeli pekee.
Katz aliongeza katika taarifa hiyo, "tumejitolea kuondoa vikwazo, kuanzisha uhakika wa kisheria na kiraia, na kuwaruhusu walowezi kuishi na kujenga.”
Taarifa hiyo iliongeza kuwa hatua hizi pia zitaruhusu mamlaka ya Israeli kusimamia baadhi ya maeneo ya kidini hata kama yapo katika maeneo yaliyo chini ya udhibiti wa Mamlaka ya Palestina.
Israeli imechukua Ukingo wa Magharibi tangu 1967, ambao unatakiwa kuwa sehemu ya taifa la Palestina la baadaye, lakini walowezi wanaiona kuwa ni ardhi ya Israeli.
Jumuiya ya Kimataifa
Uingereza imelaani vikali hatua hiyo ya Israel na kuitaka Israel ibadilishe uamuzi huo, ikisema: "jaribio lolote la upande mmoja la kubadilisha muundo wa kijiografia au idadi ya watu wa Palestina halikubaliki kabisa na ni kinyume cha sheria za kimataifa."
Msemaji wa Umoja wa Ulaya Anwar Al-Anouni aliwaambia waandishi wa habari, "Umoja wa Ulaya unalaani maamuzi yaliyochukuliwa na Baraza la Mawaziri la Usalama la Israel ili kupanua udhibiti wa Israel juu ya Ukingo wa Magharibi.”
Wakati huo huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameonyesha "wasiwasi mkubwa" kuhusu hatua mpya zilizochukuliwa na Israeli katika Ukingo wa Magharibi.
Msemaji wake, Stephane Dujarric, amesema "Katibu Mkuu ana wasiwasi mkubwa na uamuzi uliotangazwa wa Baraza la Mawaziri la Usalama la Israeli wa kuidhinisha hatua za kiutawala na utekelezaji katika Maeneo A na B ya Ukingo wa Magharibi," akibainisha kwamba mwelekeo huu unadhoofisha matarajio ya suluhisho la mataifa mawili."
Shirika lisilo la kiserikali la Israeli la Peace Now lilisema uamuzi wa serikali unatishia kuiweka kando Mamlaka ya Palestina, na kufuta makubaliano na kuanzisha unyang'anyi wa kidikteta.
Kwa upande mwingine, Baraza la Yesha, shirika linalowakilisha walowezi wengi katika Ukingo wa Magharibi, lilisifu hatua hizo, likisema "serikali ya Israeli imetangaza leo, kwamba Ardhi ya Israel ni ya Wayahudi."
Mbali na Jerusalemu Mashariki, ambayo Israeli iliiteka, zaidi ya Waisraeli 500,000 wanaishi katika makazi na vituo ambavyo ni kinyume cha sheria chini ya sheria za kimataifa, pamoja na Wapalestina milioni tatu, kote Ukingo wa Magharibi.
Mwaka 2025, upanuzi wa makazi ulifikia kiwango cha juu zaidi tangu 2017, kulingana na ripoti ya hivi karibuni ya Umoja wa Mataifa.
Hatua za Palestina
Rais wa Mamlaka ya Palestina ametoa wito wa "mikutano ya haraka ya Baraza la Umoja wa Kiarabu, Taasisi ya Ushirikiano wa Kiislamu na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa".
Mwakilishi wa Kudumu wa Palestina katika Umoja wa Mataifa, Balozi Muhannad Al-Aklouk, alitangaza kwamba "nchi ya Palestina imewasilisha ombi la dharura la kufanyika kikao cha cha Baraza la Umoja wa Mataifa ili kujadili njia za kukabiliana na maamuzi ya hivi karibuni ya serikali ya Israel."
Katika taarifa ya pamoja, mawaziri wa mambo ya nje wa Misri, Jordan, Falme za Kiarabu, Indonesia, Pakistan, Uturuki, Saudi Arabia, na Qatar wamelaani vikali maamuzi na vitendo vya Israeli.
Imetafsiriwa na Rashid Abdllah na kuhaririwa na Ambia Hirsi