Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Wafahamu wabunge saba wa Kenya waliouawa mitaani
- Author, Mariam Mjahid
- Nafasi, BBC Swahili
- Akiripoti kutoka, Nairobi
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Katika historia ya taifa la Kenya, vifo vya viongozi mashuhuri wa kisiasa vinavyotokea kwa njia ya kutatanisha vimeacha makovu ya kudumu kwenye dhamira ya wananchi.
Mauaji haya mara nyingi hutokea nyakati za misukosuko ya kisiasa, yakihusisha siasa za kiimla, uhasama wa uongozi, na migawanyiko ya kitaifa.
Matukio haya ya kikatili yaliwafanya wananchi kutokuwa na imani na serikali zilizokuwa madarakani, huku yakiibua majonzi, hasira, na hofu iliyoenea miongoni mwa wananchi.
Kila tukio la mauaji halikubaki kama tukio la kipekee bali liliibua athari za kina kuimarisha migawanyiko ya kisiasa, mianya ya usalama na wito wa uwajibikaji hasa katika idara za kijasusi.
Wabunge waliopigwa risasi na kuuawa katika mazingira tatanishi baadhi walihusishwa na maono ya mabadiliko au msimamo wa wazi dhidi ya mifumo ya utawala, huku wengine wakionekana kuangukia mikononi mwa wahalifu.
Katika taarifa hii tuwaangazia wabunge saba ambao walifariki ghafla baada ya kumiminiwa risasi wakiwa katika shughuli zao za kawaida mitaani.
1. Charles Ogondo - Mbunge wa Kasipul
Kisa cha hivi punde ni cha mauaji ya Mbunge wa eneo bunge la Kasipul katika jimbo la Homa Bay Charles Ong'ondo.
Mbunge huyu alikuwa ametoka bungeni muda mchache tu kabla ya kushambuliwa akiwa ndani ya gari lake kwenye barabara iiliyo na shughuli nyingi mjini Nairobi.
Polisi wamesema gari la Mbunge Charles Ong'ondo liliandamwa na watu wawili waliokuwa wakiendesha pikipiki kisha mmoja wao akasimama na kumfyatulia risasi kadhaa.
Dereva wake alinusurika shambulio hilo.
Marehemu ni mbunge wa chama cha Orange Democratic Movement(ODM) kinachoongozwa na mwanasiasa mkongwe Raila Odinga.
Polisi wangali wanachunguza kisa hicho huku waliotenda uhalifu huo wakiwa bado hawajakamatwa na chanzo ya mauaji hayo hakijabainika mara moja.
Dereva wa gari na abiria wa kiume, ambao hawakujeruhiwa walifanikiwa kumkimbiza mbunge huyo katika Hospitali ya Nairobi, ambapo alithibitishwa kuwa amefariki wakati anawasilishwa.
Katika taarifa iliyotolewa na Msemaji wa Polisi Muchiri Nyaga, alithibitisha kwamba Mbunge huyo aliuawa kwa kupigwa risasi Jumatano jioni kando ya Barabara ya Ngong karibu na mzunguko wa chumba cha kuhifadhi maiti cha City na mtu aliyekuwa na bunduki.
"Kuna uwezekano marehemu alilengwa na mauaji yake yalipangwa," Msemaji wa Polisi aliongezea.
Muchiri alisema makamanda wakuu wa polisi na wapelelezi walitembelea eneo hilo kuchunguza kilichotokea.
Huduma ya Polisi ililaani kitendo hicho cha ufyatuaji risasi na kukitaja kama "uhalifu mbaya na usio na maana" na kuhakikishia umma kwamba hakuna kitakachozuia uchunguzi.
2. George Muchai - Mbunge wa Kabete
Tarehe 7 mwezi Februari mwaka 2015, Mbunge George Muchai eneo bunge la Kabete alipigwa risasi na kuuawa pamoja na walinzi wake wawili na dereva wao katikati ya jiji la Nairobi.
Sanduku na bunduki mbili za walinzi ziliibiwa katika tukio hilo.
Muchai ambaye alikuwa mbunge wa chama cha Jubilee alikuwa amehudumu kwa miaka miwili tangu achaguliwe kwa mara ya kwanza.
Wakati huo, alikuwa akirudi baada ya chakula chajio na familia yake.
Familia yake ilikuwa mbele yao katika gari jingine ambapo binti yake alieleza walikuwa wametoka eneo la Westlands.
Mbunge huyo alikuwa amenusurika jaribio lingine la mauaji mnamo mwaka 2011, jambo lililoonyesha wazi kulikuwa na njama ya kumuangamiza.
3.Mugabe Were - Mbunge wa Embakasi
Melitus Mugabe Were, mbunge wa Embakasi kupitia chama cha kisiasa cha ODM, aliuawa mwezi Januari 29, 2008 katikati ya ghasia za baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2007.
Alipigwa risasi nje ya makazi yake katika mtaa wa Woodley, Nairobi.
Mauaji ya Mugabe Were yalishtua taifa lote na kuwa mfano wa hatari ya siasa za chuki.
Baada ya kesi iliyodumu miaka saba, mahakama iliwahukumu James Omondi (Castro), Wycliffe Simiyu (Zimbo), na Paul Omondi (Papa) kunyongwa kwa kosa hilo la mauaji.
5. David Kimutai Too - Mbunge wa Ainamoi
Aliyekuwa mbunge wa Ainamoi, David Too, aliuawa kwa kupigwa risasi Januari 2008 huko Eldoret, eneo la West Indies, Kaunti ya Uasin Gishu.
David Too alikuwa mwanachama wa chama cha ODM, aliuawa siku chache tu baada ya mwenzake wa Embakasi Melitus Were kupigwa risasi na kuuawa nje ya nyumba yake jijini Nairobi.
Too aliuawa pamoja na afisa wa polisi wa trafiki wa kike, na hivyo kuchochea madai kwamba kifo chake kinaweza kuwa ni masuala ya wivu wa mapenzi.
Kifo cha Too kilizua hali ya wasiwasi kote nchini huku wafuasi wa upinzani wakidai njama fiche kutokana na mauaji hayo mawili yenye utata yaliyotokea wiki moja.
Mshukiwa mkuu wa mauaji hayo Andrew Moeche Omwenga, afisa wa polisi, alidai alijitetea baada ya kushambuliwa na Kimutai pamoja na afisa mwenzake Eunice Chepkwony.
Moeche alihusishwa kimapenzi na Chepkwony, ambaye alikuwa mjane wa askari mwingine.
6. Tony Ndilinge - Mbunge wa Kilome
Mnamo mwaka 2001, aliyekuwa Mbunge wa Kilome, Tony Ndilinge, aliuawa kwa kupigwa risasi mara mbili kichwani nje ya baa moja eneo la Githurai viungani mwa jiji la Nairobi.
Wakati huo, Ndilinge alikuwa mkosoaji mkubwa wa utawala wa Rais wa zamani Daniel arap Moi.
Mauaji hayo yalitafsiriwa na wengi kama njama ya kisiasa iliyofanyika katika mazingira ya siri na taharuki.
7. Tom Mboya - Mwanasiasa
Mnamo Julai 5, 1969, Tom Mboya mwanasiasa mahiri na miongoni mwa vinara wa harakati za uhuru nchini Kenya aliuawa kwa kupigwa risasi katikati ya jiji la Nairobi.
Wakati huo akiwa Waziri wa Mipango ya Kiuchumi, Mboya alikuwa na umri wa miaka 39 pekee.
Kifo chake kilisababisha mshtuko wa kitaifa, huku wengi wakikitafsiri kama njama ya kisiasa dhidi ya ushawishi wake mkubwa.
Alizikwa kwa heshima katika jumba la kumbukumbu lililojengwa kwenye Kisiwa cha Rusinga.
Sio tu Kenya ambayo imeshuhudia mauaji ya wabunge mitaani baadhi ya mataifa ya bara la Afrika yameshuhudia viongozi wa ngazi juu waliouawa kwa njia tatanishi.