Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Boniface Mwangi: Mfahamu mwanaharakati wa Kenya mwenye utata
- Author, Abdalla Seif Dzungu
- Nafasi, BBC Swahili
- Akiripoti kutoka, Nairobi Kenya
- Muda wa kusoma: Dakika 4
Mwanaharakati wa Kenya Boniface Mwangi hatimaye ameachiliwa huru na serikali ya Tanzania, mkurugenzi mtendaji wa shirika la Haki Afrika ameambia BBC.
Hussein Khalid alithibitisha kuwa alikuwa pamoja na Mwangi wakiwa njiani kutoka kutoka kaunti ya Kwale karibu na mpaka wa Tanzania na Kenya ambako alikuwa amewachwa na sasa wanaelekea Nairobi.
Mwanaharakati Boniface Mwangi na Agather Atuhaire wa Uganda walikamatwa nchini Tanzania mapema wiki hii, ambako walikuwa wameenda kuhudhuria kesi ya kiongozi wa CHADEMA Tundu Lissu.
Rais Samia Suluhu Hassan alionya kwamba hataruhusu wanaharakati kutoka nchi jirani "kuingilia" masuala ya nchi yake na kusababisha "machafuko".
lakini je, Boniface mwangi ni nani haswa?
Mfahamu Mwanaharakati wa Kenya Boniface Mwangi
Boniface Mwangi alizaliwa Julai 10, 1983 na ni mwanahabari wa Kenya, mwanasiasa na mwanaharakati aliyejihusisha na harakati za kijamii na kisiasa.
Kulingana na Mtandao wa Wikipedia, anajulikana kwa taswira zake za ghasia za baada ya uchaguzi zilizokumba Kenya mwaka wa 2007 na 2008.
Amemuoa Hellen Njeri Mwangi, ambaye anafanya kazi naye katika shirika lake la Pawa 254. Wana watoto watatu
Mwangi alitajwa kuwa miongoni mwa Waafrika 100 bora wenye ushawishi mkubwa na jarida la New African mwaka 2020.
Maisha yake ya utotoni na elimu ya msingi
Mwangi alizaliwa katika kaunti ya Taveta, nchini Kenya, kwenye mpaka na Tanzania. Mama yake alikuwa mfanyabiashara aliyevuka mpaka. Mwangi alianza kuishi na babu yake huko Nyeri, Mkoa wa Kati wa Kenya, alipokuwa na umri wa miaka sita.
Baadaye alihamia na mamake katika kitongoji cha watu wa kipato cha chini cha Nairobi cha Ngara, kisha eneo la Majengo, Githurai 45, kabla ya kuishia Pangani. Mwangi aliacha shule katika kipindi hiki na kumsaidia mamake kuuza vitabu.
Uanahabari
Mama yake alipofariki mwaka wa 2000, Mwangi, ambaye wakati huo alikuwa na umri wa miaka 17, aliamua kubadilika ili kunusurika. Alijiunga na shule ya Biblia kwa nia ya kuwa mchungaji, na kupata diploma katika masomo ya Biblia.
Akiwa shuleni alipendezwa na upigaji picha. Alishawishiwa na mpiga picha wa Kenya Mohamed Amin.
Licha ya kutokuwa na elimu ya shule ya upili, Mwangi alifanikiwa kupata nafasi katika shule ya kibinafsi ya uandishi wa habari. Ili kufadhili masomo yake ilimbidi aendelee kuuza vitabu mitaani, lakini akaanza kupata uzoefu kama mwandishi wa picha. Alichapisha picha katika gazeti la kitaifa la The Standard, na mwaka wa 2005 alishinda tuzo zake za kwanza za upigaji picha.
Ndani ya miaka mitatu alipata kutambuliwa kimataifa kama mmoja wa wapiga picha wa Afrika walio na vipaji.
Alitunukiwa Tuzo ya Mpigapicha Bora wa Mwaka wa 2008 na 2010 wa CNN Afrika. Hata hivyo, aliwacha kazi yake ya upigaji picha, ili kuingia katika uwanaharakati.
Uwanaharakati
Mwangi aliacha uandishi wa habari baada ya kushuhudia na kupiga picha ghasia za baada ya uchaguzi nchini Kenya mwaka wa 2007 kama mpiga picha wa magazeti.
Alipata mfadhaiko baada ya kuathiriwa moja wakati watu wa jamii yake walipotishiwa
Aliathirika zaidi baada ya kulazimika kuwaangazia wanasiasa walewale waliochochea ghasia bila kuadhibiwa.
Mpango wake wa kwanza ulikuwa mradi wa Picha Mtaani, kwa Kiswahili "picha mtaani", ukionyesha picha za ghasia za mwaka 2007 baada ya uchaguzi wa kitaifa, kati ya makabila mbalimbali.
Maonyesho haya ya mitaani yalionyeshwa kote nchini kwa watu kujadili upatanisho. Na kukuza
uponyaji wa kitaifa
Zaidi ya watu 600,000 waliona maonyesho hayo. Hii ilikamilishwa baadaye na filamu ya Heal the Nation, ambayo ilionyeshwa zaidi katika maeneo ya vitongoji duni.
Kufuatia hatua hii Mwangi alianza kukuza msimamo thabiti zaidi wa haki za kibinadamu katika makabiliano yake ya kisiasa kupitia kuzungumza dhidi ya uongozi mbaya na mbovu wa kisiasa, na kutangaza ujumbe wa amani kwa uchaguzi uliopangwa kufanyika 2013 kwa mipango inayoitwa MaVulture na Team Courage.
Team Courage ni kundi la wanaharakati wenye lengo la kushawishi raia wazalendo kuchukua hatua za kijasiri na madhubuti katika kujenga Kenya mpya.
Mpango wake wa hivi punde zaidi ni Pawa 254 ambao ulizinduliwa mwaka wa 2011, kituo na nafasi kwa wasanii na wanaharakati kufanya kazi pamoja kuelekea mabadiliko ya kijamii na kuendeleza haki za Kibinadamu nchini Kenya.
Mwanaharakati mwenye utata
Mwangi alikamatwa na polisi Mei 2019 kwa madai ya kuandaa mapinduzi nchini Kenya
Maafisa wa upelelezi walikuwa wamemkamata Bw Mwangi nyumbani kwake na kumpeleka katika Kituo Kikuu cha Polisi ambako alirekodi taarifa.
Aliachiliwa muda mfupi baada ya taarifa inayoelezea mashtaka ambayo huenda akakabiliwa nayo kusambaa kwenye mitandao ya kijamii.
Mwaka 2024 Kuzuiliwa kwake kulikuja baada ya kuitisha maandamano dhidi ya serikali katika mbio za marathon katika mji mkuu, Nairobi.
Polisi walikuwa wamethibitisha kuwa Bw Mwangi alikuwa kizuizini lakini hawakutoa maelezo zaidi.
Kuzuiliwa kwake kulizua hasira miongoni mwa wafuasi wake, waliotaka aachiliwe.
Alikuwa akikusanya watu kwenye X (zamani Twitter) kumtaka Rais William Ruto ajiuzulu, akitumia neno #RutoMustGo na #OccupyStanChart,
Aliwataka watu kuvalia rangi za bendera ya taifa, kuvaa kanga zenye ujumbe "RutoMustGo" na kushiriki maandamano mtandaoni.