Unapata uchovu? Fahamu mbinu 5 za kukabiliana nao

    • Author, Ousmane Badiane
    • Nafasi, BBC
  • Muda wa kusoma: Dakika 3

Uchovu, usingizi, maumivu ya misuli, kupoteza motisha, ni miongoni mwa matatizo yanayohusiana na kazi na mara nyingi hupunguza ufanisi kazini.

Utafiti wa Chama cha Wanasaikolojia wa Senegal (2021) unakadiria kuwa mfanyakazi 1 kati ya 3 huko Dakar, huonyesha dalili za mfadhaiko wa kisaikolojia unaohusiana na kazi. Nyuma ya uso wa tabasamu na mwonekano wa mafanikio, maisha yanaporomoka kimya kimya.

Kulingana na utafiti wa Taasisi ya Wafanyakazi, zaidi ya 60% ya wafanyakazi wa Senegal wanaripoti kukabiliwa na mfadhaiko mkubwa unaohusiana na kazi, lakini chini ya 10% wanawasiliana na mtaalamu wa afya ya akili.

Meneja wa Utumishi, katika mji mkuu wa Dakar, Senegal, Amsatou Ndiaye anatoa ushauri muhimu ili kuepuka kukosekana kwa ufanisi kazini.

Weka mipaka

Kufanya kazi kupita kiasi, ni moja wapo ya sababu ya uchovu. Ili kuzuia uchovu huu, Amsa anapendekeza kujifunza kuweka malengo ya kazi yanayowezekana, yaani malengo yanayoweza kufikiwa, na kuamua kupumzika pale unapochoka.

Mafunzo ya usimamizi wa muda yanaweza kuimarisha uwezo wa kujipanga.

Nyoosha mwili

Shughuli za kimwili huzuia uchovu wa mwili. Matembezi madogo, kunyoosha mikono na miguu, haya yanaweza kupunguza sana uchovu wa akili na mwili.

Katika mahali pa kazi, hili linaweza kufanyika kwa kuchukua mapumziko au kujishughulisha na mambo ambayo yanapumzisha mwili.

Mtindo wa maisha

Kulala vizuri, kula vizuri, na kunywa maji ya kutosha: Vitendo hivi vina athari chanya ya moja kwa moja kuzuia uchovu. Amsa anasisitiza haja ya kampeni za uhamasishaji wa kupata lishe nzuri na usingizi, mambo ambayo mara nyingi hupuuzwa katika mazingira ya kazi.

Tafakuri

Kupumzika na kudhibiti hisia, ni silaha yenye nguvu dhidi ya uchovu sugu. Fanya tafakuri katika maisha ya kila siku. Katika eneo lako la biashara, tengeneza eneo la utulivu au hudhuria mafunzo kuhusu udhibiti wa hisia. Hilo linaweza kuchangia mazingira ya kazi yenye amani.

Omba msaada

Uchovu mara nyingi hutokea kimya kimya. Kwa hivyo ni muhimu kujenga utamaduni wa kuaminiana na kujieleza. "Kuzungumzia matatizo yako sio ishara ya udhaifu, lakini ni ishara ya ufahamu," anasisitiza Amsa.

Kuanzisha vituo vya kusikiliza matatizo ya watu, washauri wa afya, au vikundi vya majadiliano – haya yanaweza kusaidia kuhimiza majadiliano ya wazi na kugundua dalili za mapema.

Kulingana na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO), uchovu unahusisha mambo matatu: hisia ya uchovu, kujitenga kiakili na kazi, na kushuka kwa utendaji wa kazi.

Uchovu hautambuliwi kama ugonjwa wa kazi. Kwa maneno mengine, sio ugonjwa wa akili.

WHO inapendekeza kwamba mataifa yaimarishe sera za afya kazini, kuhakikisha uwiano wa maisha na kazi, na kuiweka afya ya akili katika huduma za afya.