Glasi moja ya maziwa hupunguza hatari ya kupata saratani ya utumbo - utafiti

    • Author, Philippa Roxby
    • Nafasi, BBC
  • Muda wa kusoma: Dakika 3

Utafiti uliofanyika Uingereza umepata ushahidi kwamba watu wanao kula kalsiamu zaidi katika milo yao - inaweza kuwasaidia kupunguza hatari ya kupata saratani ya utumbo.

Watafiti walichambua milo ya wanawake zaidi ya nusu milioni kwa zaidi ya miaka 16 na kugundua kuwa maziwa ya wanyama au vyakula vya jamii ya (soya, karanga, mbegu, lozi, kunde, mchele, shayiri, nazi, korosho, katani na macadamia) - vina kalsiamu ambayo ni kinga.

Pia walipata ushahidi zaidi kwamba unywaji wa pombe kupita kiasi na nyama iliyochakatwa kiwandani vina athari na huongeza hatari ya kupata saratani.

Madaktari wanasema lishe bora, kuwa na uzito wa kiasi na kuacha kuvuta sigara ni njia bora za kupunguza hatari ya kupata saratani ya utumbo.

Utafiti unasemaje?

Utafiti huo, kutoka Chuo Kikuu cha Oxford na Kituo cha Utafiti wa Saratani Uingereza, unasema kalsiamu, kutoka katika maziwa ya wanyama au vyakula vya jamii ya kunde, mbegu, karanga n.k, hupambana na saratani.

Miligramu 300 ya kalsiamu kwa siku katika mlo, au glasi kubwa ya maziwa, hupunguza hatari ya kupata saratani kwa 17%

Kula nyama iliyosindikwa kupita kiasi na nyama nyekundu na pombe kunaweza kuongeza hatari yako ya kupata saratani ya utumbo.

Kunywa glasi kubwa ya pombe kwa siku huongeza hatari ya saratani kwa 15%. Kula gramu 28 ya nyama iliyosindikwa au nyama nyekundu, kwa siku huongeza hatari ya saratani kwa 8%.

Kalsiamu hufanya kazi gani?

Calcium (Kalsiamu) ni madini muhimu kuimarisha mifupa na kuweka meno yako katika afya njema, lakini ushahidi unaonyesha hutoa kinga dhidi ya baadhi ya saratani.

Kuna kalsiamu nyingi katika maziwa, mtindi na jibini. Vyakula vyenye tuwi la maziwa pia ni moja wapo ya vyanzo vikuu vya kalsiamu.

Inapatikana pia katika vyakula vingine kama vile soya na vinywaji vya mchele, mkate mweupe, njugu, mbegu na matunda kama vile tini zilizokaushwa, mboga aina ya kale na samaki wa kwenye makopo, na pia iko kwenye maziwa yaliyoondoshwa sukari.

Utafiti huo unasema kalsiamu inaweza kukulinda dhidi ya saratani ya utumbo "kwa sababu ina uwezo wa kuingiliana na asidi ya bile na molukule ya free fatty acids kwenye utumbo mpana, na kupunguza athari zao katika kusababisha kansa."

Dalili ya saratani ya utumbo

Kuna takriban visa 44,000 vya saratani ya utumbo kila mwaka nchini Uingereza, na kuifanya kuwa saratani ya nne kwa wingi wa watu.

Ingawa kesi nyingi ni za wazee, lakini viwango vya saratani vinaongezeka kwa watu wa chini ya miaka 50. Wataalamu wanasema lishe duni na kunenepa kupita kiasi vinaweza kuwa miongoni mwa mambo yanayohusika.

Dalili za saratani ya utumbo ni pamoja na:

  • Mabadiliko ya kwenda haja, kama vile kuharisha, kwenda chooni mara nyingi zaidi au kutopata choo vizuri.
  • Kutokwa na damu kwenye shimo la haja kubwa au kukuta damu kwenye kinyesi chako
  • Kupoteza uzito bila ya sababu inayoeleweka
  • Uchovu usio na sababu au kushindwa kupumua vizuri

Zungumza na daktari wako ikiwa utagundua hali yoyote kati hizo.

Dk Lisa Wilde, kutoka shirika Bowel Cancer UK, anasema, mtu mmoja hugunduliwa na saratani ya utumbo "kila dakika 12" na nusu ya saratani zote za utumbo zinaweza kuzuiwa kwa kuwa na mtindo bora katika maisha.

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah imehaririwa na Ambia Hirsi