Putin: Tunaweza kujenga kituo kikubwa zaidi cha gesi kwa Ulaya nchini Uturuki

Putin

Chanzo cha picha, Getty Images

Rais wa Urusi Vladimir Putin amesema kuwa wanaweza kuanzisha kituo kikubwa zaidi cha kusambaza gesi kwa Ulaya nchini Uturuki.

Akikumbusha kwamba Bomba la Nord Stream 1, ambalo limetumika kuhamisha gesi hadi Ulaya hadi leo, limezimwa, Putin alisema kuwa wanaweza kuhamisha gesi hadi Ulaya kupitia Uturuki badala yake.

Putin aliongeza kuwa hili linaweza kudhihirika iwapo pande zote zitakuwa tayari.

Akizungumza katika hafla ya Wiki ya Nishati ya Urusi, Naibu Waziri Mkuu wa Urusi Aleksandr Novak alisema kwamba mabomba mapya yanaweza kuongezwa kwenye Bomba la Kusambaza Kituruki la Moscow, kulingana na habari za shirika la Reuters, "Hii ni moja ya chaguzi ambazo tutachunguza. Tunapaswa kulifanyia kazi,” alisema.

Akijibu kauli ya Putin, Waziri wa Nishati na Maliasili Fatih Dönmez alisema, "Hii ni mara ya kwanza tunasikia kauli za Putin kuhusu usafirishaji wa gesi kutoka njia mbadala." Dönmez alisema, "Ni mapema sana kuzungumza juu ya hili," na "Kwa miradi kama hii ya kimataifa, upembuzi yakinifu unahitajika, na upande wa kibiashara unapaswa kujadiliwa."

Rais wa Urusi Vladimir Putin, kwa upande mwingine, alisema kuwa inawezekana kutengeneza njia ya Nord Stream 1 na 2, ambapo milipuko ilifanyika mwezi uliopita, lakini kwamba mustakabali wa njia hizi inapaswa kuamuliwa pamoja na Ulaya. "Bomba katika North Stream 2 haionekani kuharibika.

Lakini mpira uko katika mahakama ya Umoja wa Ulaya kuhusu suala hili," Putin alisema. Ujenzi wa Nord Stream 2 ulikamilika kabla ya uvamizi wa Urusi nchini Ukraine mnamo Februari 24, lakini Ujerumani ilikuwa imeamua kutofungua njia hiyo kutokana na uvamizi huo.

Gesi iliyotumwa kutoka Nord Stream 1 ilikatwa na Urusi wakati wa kiangazi, huku Urusi ikidai kuwa haiwezi kutengeneza mitambo iliyoharibika kutokana na vikwazo hivyo, huku nchi za Magharibi zikisisitiza kuwa huo ni uamuzi wa kisiasa. Kutokana na matatizo katika mtiririko wa gesi kutoka Urusi, vikwazo vya taa na joto vilitangazwa katika nchi nyingi za EU.

Katika hotuba yake hii leo, Putin alitangaza kuwa nchi yake inalenga kuweka mauzo ya mafuta katika kiwango cha sasa hadi 2025, na pia alipongeza uamuzi wa kundi la OPEC+, ambalo liliamua kupunguza uzalishaji wiki iliyopita ili kuweka bei ya mafuta kuwa juu.