Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Unalijua eneo lisilo na mwenyewe duniani? kulifikia unahitaji siku 11
Ulimwengu umejaa sehemu za kustaajabisha, lakini bado kuna sehemu nyingi za mbali za dunia ambazo watu wachache hupata kuona. Katika kitabu kinachoitwa Remote Experiences: Extraordinary Travels from North to South, Mpiga picha David De Vleeschauwer na mwandishi wa habari za usafiri Debbie Pappyn walisafiri kuyafikia maeneo 12 yaliyofichika zaidi, yasiyotambulika na ya mbali zaidi ambayo hayajaguswa na utalii.
Kwa kwenda mahali ambapo watu wengi hawendi, wawili hao wanatumai kuwahimiza wengine kusafiri kuyafikia na kwa malengo zaidi, na kutunza vyema sayari tunayoishi sote.
Hakuna mtu anayemiliki, eneo hili la ncha ya kaskazini ni kama karatasi ya barafu inayobadilika kila wakati inayoelea katikati ya Bahari ya Aktiki.
Meli kubwa zaidi duniani na yenye nguvu zaidi ya kuvunja barafu inayotumia nyuklia, 50 Let Pobedy, husafiri kila msimu wa joto linalofikia hadi nyuzi joto 90° kaskazini ikiwa na abiria 100, wote wakiwa na shauku kubwa ya kukanyaga eneo hili muhimu la kijiografia.
Kwa wengi wao, wakati huu ni zaidi ya kuongeza orodha tu ya kufika katika maeneo fulani.
Meli inayopasua barafu yenye unene wa 3m ikielekea huko, imeindwa jina kwa kirusi linalomaanisha "Miaka 50 ya Ushindi", kama kumbukumbu ya miaka 50 ya ushindi wa Umoja wa Kisovyeti katika Vita Kuu ya Pili.
Ili kuadhimisha uzinduzi wake, meli hiyo ilibeba mwenge wa Olimpiki hadi kwenye North Pole mnamo 2013 wakati wa maandalizi ya Olimpiki ya Majira ya baridi ya Sochi.
Ikiendeshwa na vinu vya nyuklia vya megawati 171 na jenereta mbili za megawati 27.6, meli hiyo inayovunja barafu yenye urefu wa karibu mita 160 inaweza kukimbia karibu kilomita 40 kwa saa - na kusafiri bila kusimama kwa karibu miaka sita bila kurejea nchi kavu kwa ajili ya kujaza mafuta.
Kukiwa na vinu vya nyuklia, vituo vya kusimama jwa ajili ya kuweka mafuta vinakaribia kuwa historia.
Hii si safari ya kawaida ya baharini ndani ya meli ya kifahari.
Njia ya kuelekea sehemu ya eneo hilo la kaskazini kabisa ya sayari, ambapo mhimili wa mzunguko wa Dunia hukutana na uso wake, huchukua siku 11, kwa mwendo wa kawaida uzioidi 20km kwa saa wakati wa kupasuka kupitia barafu.
Katika ulimwengu huu wa barafu, mwanadamu si mfalme. Wasafiri huchukua safari hii si tu kukanyaga ardhi ya pembe ya dunia lakini pia kupata uzoefu wa uzuri wa eneo hili la Aktiki.
Kutazama sehemu kubwa ya barafu ya bahari kunalevya. Jua halitui kamwe katika majira ya kiangazi ya Aktiki na bado mwanga hubadilika kila mara, ukiakisi barafu nyeupe na ng'aavu. Wakati mwingine hali ya hewa ni ya baridi, na hali mbaya na isiyo na utulivu, na yenye ukungu mnene. Hilo halijalishi kama uko nje au unatazama kupitia matundu kwenye tumbo lenye joto la meli.
Baada ya siku kadhaa kusafiri, unapofika kwenye eneo hili la ncha ya Kaskazini, abiria huwana bashasha na baadhi wanaielezea kama hisia ya mwanzo mpya.
North Pole imejificha. Ni eneo dogo lililobaki kwenye latitudo kamili ya nyuzi 90 ° kaskazini.
Katika Kisiwa cha Hooker, boti za Zodiac hubeba abiria kwenye barafu karibu na Rubini Rock ili kushuhudia miamba yenye kuvutia.
Abiria wanaalikwa kujiunga na miamba hii inayoelea katika eneo hili ili kufahamu ukubwa halisi wa jangwa hili lililoganda. Wakati helikopta inapopaa kutoka kwenye meli, meli kubwa ya chuma inayoelea hubadilika na kuwa chembe ndogo nyekundu katika bahari yenye rangi nyeupe inayometa, na njia zake kwenye barafu zikiwa bado zinaonekana kama mshipa katika bahari ya Aktiki yenye giza na baridi.
Helikopta huzunguka meli, na kuruhusu abiria kufahamu - mazingira haya. Kabla ya safari hii, hakuna mtu ambaye angeweza kutambua kwamba mandhari hii inapatikana hadi pale kwenye Ncha ya Kaskazini isiyoweza kufikiwa.
Sasa, baada ya kukanyaga eneo hili, wasafiri hawa hatimaye wanaelewa ukubwa na barafu nyeupe linalotandaza sehemu ya juu kabisa ya dunia yetu.
Makala hii ilichukuliwa kutoka kwa kitabu Remote Experiences: Extraordinary Travels from North to South, kilichochapishwa na Taschen.