Tutakula nini kwenye safari za kwenda angani?

    • Author, Laura Hall
    • Nafasi, BBC

Ushindani wa angani unakuwa kwa kasi. Katika miaka miwili ijayo, Nasa inapanga kuwatuma wanaanga tena Mwezini kupitia programu yake ya Artemis.

Kwani kituo cha Kimataifa cha Anga za Juu (ISS), kilichoundwa kuzunguka kwa miaka 15 - sasa kinafikia mwaka wake wa 26 angani na kitabadilishwa hivi karibuni.

Misheni hizo na ongezeko la miradi ya utalii ya anga za juu ya watu walio na pesa nyingi, inazua swali moja kwa mwandishi wa vyakula kama mimi: Tutakula nini tukifika huko?

Chakula Kisicholiwa Angani

Dkt. Sonja Brungs, naibu kiongozi katika Shirika la Anga za Juu la Ulaya anasema, "chakula bora, chakula kinachofaa chenye virutubisho vingi, kilichotengenezwa kulingana na mahitaji ya wanaanga ni muhimu kwa ajili ya kufanikisha misheni ya anga za juu."

Hivi sasa, wanaanga wanapewa mifuko midogo ya chakula iliyo na milo iliyotayarishwa duniani. Milo hii hutengenezwa na makampuni maalumu ya kuzalisha chakula na kisha kukaushwa, kupunguzwa maji au kupunguzwa vijidudu. Wanaanga huongeza maji kupasha moto au kupoza milo hiyo.

Wanaweza pia kwenda angani na chakula cha nyumbani, lakini mlo huo pia unapaswa kutayarishwa kwa uangalifu na kuondolewa vijidudu.

Kuna baadhi ya vyakula ambavyo havifai; chochote chenye asili ya mkate, hakiwezi kuchukuliwa angani kwani kinaweza kupeperushwa kwa urahisi.

Kumaanisha kinaweza kuingia kwenye hewa na mwanaanga akavuta pumzi kikaingia ndani au kuingia kwenye vifaa vya chombo.

Chumvi haitakiwi sana, kutokana na ukweli kwamba mwili huhifadhi sodiamu kwa namna tofauti katika anga, na inaweza kusababisha ugonjwa wa mifupa. Pombe pia hairuhusiwi kwani inaathiri mfumo wa kuchakata maji taka katika chombo.

Mradi wa Kutengeneza Chakula

Mwaka 2021, Nasa ilizindua shindano la kuunda njia mpya za kutengeneza chakula angani kwa kutumia rasilimali chache zinazozalisha taka kidogo, huku pia zikizalisha chakula salama, chenye lishe na kitamu ambacho kinaweza kutumika kwa kwa muda mrefu katika anga ya juu.

Solar Foods, yenye makao yake mjini Helsinki, ni mojawapo ya makampuni nane ambayo yameingia kwenye shindano hilo. Wanafikiria kutumia taka za angani ili kuunda protini.

"Tunatengeneza chakula kutoka kwenye hewa," anasema Artuu Luukanen, makamu wa rais wa Solar Foods. Kampuni yake iligundua vijidudu vinavyoweza kuliwa katika mashamba ya Finland ambavyo hukua kwa kula mchanganyiko wa kaboni dioksidi, hidrojeni na oksijeni.

Vijidudu hivyo ni chanzo cha protini. Protini inaweza kuchanganywa na aina mbalimbali ya vitu vya ladha ili kuunda chakula chenye lishe bora, kama vile pasta, michi ya protini, nyama mbadala na hata yai mbadala.

"Tulianza kufikiria juu ya chakula cha anga za juu kwa sababu katika mazingira yoyote ya anga, kuna gesi taka mbili muhimu zinazopatikana; hidrojeni na kaboni dioksidi," anasema Luukanen.

"Kwa hivyo tunachozungumza hapa sio tu teknolojia ya utengenezaji wa chakula, lakini ni chakula ambacho kitakuwa sehemu muhimu ya udhibiti wa mazingira na mfumo wa kusaidia maisha."

Protini yao inaweza kugeuzwa kuwa lahamu au unga na kuchanganywa na unga wa kawaida na viungo ili kuunda chakula kilichorutubishwa kwa protini kama vile tambi, miche ya protini na hata chokoleti.

Majaribio yanaendelea ili kugundua ikiwa inaweza kuchanganywa na mafuta na kugeuzwa kuwa chakula chenye umbo la nyama.

Vyakula vya Asili

Chakula cha asili pia kinazingatiwa. Wanaanga wanahitaji vyakula vya asili, na majaribio yanaendelea kuhusu jinsi ya kupanda mboga katika mazingira ya anga za juu. Chombo cha ISS kina bustani yake ndogo ya mboga, ambapo wanaanga hutafiti ukuaji wa mimea.

Maabara ya Interstellar kwenye Kisiwa cha Merritt, Florida, imetengeneza mfumo wa kisasa wa kuzalisha mimea midogo midogo, mboga mboga, uyoga na hata wadudu; kupitia shindano la Nasa.

Kampuni nyingine ni Enigma of the Cosmos huko Melbourne, Australia, inayofanya kazi kukuza mimea midogo midogo kwa mazingira ya angani.

Jambo ambalo linaonekana kuwa na uwezekano ni kwamba siku zijazo chakula cha angani kitajumuisha uyoga. Washindi watatu kati ya sita wa Shindano la Chakula la Nasa wanatafiti uyoga.

Kampuni ya Mycorena wa Gothenburg, kutoka Sweden, ambayo imetengeneza mfumo unaotumia mchanganyiko wa mwani na uyoga kuzalisha aina ya protini kama inayopatikana kwenye uyoga, ambayo mara nyingi hutumiwa kama mbadala wa nyama.

Chakula hiki cha anga za juu kiko katika mfumo wa duara – kina umbo kama vile umbo la minofu ya kuku. Faida ya ziada ni kwamba chanzo chake cha protini yake, kina asidi zote muhimu za amino ambazo mwili wa binadamu unahitaji kufanya kazi.

Biashara ya Chakula

Kadiri fursa zinavyokua kwa kampuni binafsi kuingia kwenye mbio za angani, ndivyo pia fursa kwa wapishi zinavyoibuka.

Mpishi Rasmus Munk kutoka Copenhagn. Hivi karibuni alitangaza kuingia ushirikiano na kampuni ya SpaceVIP.

Ushirikiano huo ni kuhudumia chakula kwenye chombo binafsi cha angaza za juu cha Space Perspective Neptune, ambapo tikiti zinagharimu dola za kimarekani 495,000, kwa kila mtu kwa safari ya saa sita kwenda angani.

Awamu ya tatu ya Shindano la Chakula la NASA, inaendelea msimu huu wa joto na inalenga kupima zaidi jinsi miradi hii inavyoweza kufanya kazi katika mazingira kama ya anga.

Ni jambo la kutazamwa kwa ukaribu; ingawa kuna uhakika kwamba vyakula hivi vipya vitakuwa sehemu ya lishe ya mwaanaanga, pia inaonekana huenda vitaathiri jinsi tunavyokula duniani katika siku zijazo pia.