Jinsi madaktari wa kike wa upasuaji walivyonyanyaswa kingono wakati wa upasuaji

Chanzo cha picha, Getty Images
Madaktari wa upasuaji wa kike wanasema wananyanyaswa kingono, kushambuliwa na katika visa vingine kubakwa na wenzao, uchambuzi mkubwa wa wafanyakazi wa Huduma ya afya ya Uingereza -NHS umegundua.
BBC News imezungumza na wanawake ambao walinyanyaswa kingono katika chumba cha upasuaji wakati upasuaji ukifanyika.
Waandishi wa utafiti huo wanasema kuna mtindo wa wanafunzi wa kike kudhalilishwa na madaktari bingwa wa upasuaji wa kiume, na hii inafanyika sasa, katika hospitali za NHS.
Chuo cha Royal cha Madaktari wa upasuaji kilisema matokeo hayo "yalishtua sana".
Unyanyasaji wa kijinsia, unyanyasaji wa kingono na na ubakaji vimetajwa kuwa siri ya wazi ya upasuaji.
Kuna hadithi ambayo haijaelezewa ya wanawake ambapo wapasuaji wa kiume waliwatomasa na kugusisha sehemu za siri kwenye miili ya wafanyakazi wa kike. Wengine wamejitoa kingono ili kupata fursa za kazi.
Uchambuzi wa Chuo Kikuu cha Exeter, Chuo Kikuu cha Surrey na kitengo cha kinachoshughulikia Utovu wa Kimapenzi katika Upasuaji – vimefanya mahojiano ya kipekee na na BBC News.
Takriban theluthi mbili ya madaktari wa upasuaji wa wanawake waliojibu watafiti hao walisema wamekuwa walengwa wa unyanyasaji wa kijinsia na theluthi moja wamedhulumiwa kingono na wenzao katika miaka mitano iliyopita.
Wanawake wanasema wanahofia kuwa kuripoti matukio kutaharibu kazi zao na hawana imani kuwa NHS itachukua hatua.
'Kwa nini uso wake uko katikati ya matiti yangu?'
Kuna uoga wa kuzungumza kwa uwazi kuhusu suala hili. Judith ambaye aliomba tutumie jina lake la kwanza tu, kwa sasa daktari wa upasuaji mwenye uzoefu na mwenye kipaji anasema.

Chanzo cha picha, CREDIT: JONATHAN SUMBERG
Alishambuliwa kingono mapema katika kazi yake alipokuwa mtu aliyekuwa na uwezo mdogo zaidi katika jumba la upasuaji - na daktari mkuu wa upasuaji wa kiume alikuwa akitokwa na jasho.
"[Yeye] aligeuka tu na kuzika kichwa chake kwenye matiti yangu na nikagundua kuwa alikuwa akisugua uso wake katikati ya matiti yangu.
"Unahisi kuchanganyikiwa na kukosa la kufanya, unajiuliza, 'mbona uso wake upo katikati ya matiti yangu?"
Alipofanya hivyo kwa mara ya pili Judith alijitolea kumletea taulo.
Alimjibu "hapana, hii inanifurahisha zaidi", anasema, "na alikuwa akitabasamu - nilihisi mchafu, nilihisi kudhalilishwa".
Baya zaidi kwake ulikuwa ni ukimya wa wenzake juu ya jambo hili.
"Hakuwa hata mtu mkubwa zaidi katika chumba cha upasuaji, lakini alijua kuwa tabia hiyo ilikuwa sawa na huo ni uozo."
Hii ilitokea kwa Judith katikati ya chumba cha upasuaji, lakini unyanyasaji wa kijinsia na unyanyasaji wa kingono umeenea zaidi ya hospitali.
'Nilimuamini'
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Anne - hatuwezi kufichua jina lake halisi kwa sababu za kisheria - alitaka kuzungumza na BBC kwa sababu anaamini mabadiliko yatatokea tu wakati watu watakapozungumza.
Hachagui kuelezea kilichomtokea kama ubakaji, lakini ni wazi ngono iliyofanyika haikuwa ya maelewano. Ilifanyika katika hafla ya kijamii iliyounganishwa na mkutano kuhusu matibabu - mkutano wa madaktari wenye utaalamu unaofanana.
Kwa mtindo unaofahamika, yeye alikuwa mkufunzi na daktari wa kiume alikuwa mshauri.
"Nilimuamini, nilimtazama," anasema.
Alitumia uaminifu huo akisema hajui watu wengine huko na kwamba hangeweza kuwaamini.
"Kwa hiyo, alinirudisha mahali nilipokuwa nakaa, nilifikiri anataka kuzungumza na bado alinigeuka ghafla na akafanya mapenzi na mimi."
Alisema wakati huo alihisi mwili wake uliganda na anasema "Sikuweza kumzuia".
"Sio kile nilichotaka, haijawahi kuwa kile nilichotaka, haikutarajiwa kabisa."
Alipomwona siku iliyofuata "alikosa amani".
"Sikuhisi ningeweza kufanya fujo, nilihisi kuna utamaduni mkubwa sana wa kuvumilia chochote unachofanyiwa."
Tukio hilo lilikuwa na athari ya kudumu kwake, kwanza lilimuacha akiwa amekufa ganzi kihisia na miaka ya baadaye "kumbukumbu ya tukio hilo ilikuwa ikinijia akilini mwangu kama tukio la kutisha, kama ndoto mbaya" kazini, hata alipokuwa akijiandaa kumfanyia mgonjwa upasuaji.
Kutetereka kwa imani kwa madaktari wa upasuaji
Inakubalika sana kwamba kuna utamaduni wa kukaa kimya dhidi ya tabia hiyo. Mafunzo ya upasuaji yanategemea kujifunza kutoka kwa wafanyakazi wenzako wakuu katika chumba cha upasuaji na wanawake wametuambia ni hatari kusema kuhusu wale ambao wana mamlaka na ushawishi kutokana na kazi zao za baadaye.
Ripoti hiyo, ambayo imechapishwa katika Jarida la Upasuaji la Uingereza, ni jaribio la kwanza la kufahamu kiwango cha tabia hiyo ya unyanyasaji wa kingono.
Madaktari wa upasuaji waliosajiliwa - wanaume na wanawake - walialikwa kushiriki bila kujulikana kabisa na 1,434 walijibu. Nusu walikuwa wanawake:
- 63% ya wanawake walikuwa walengwa wa unyanyasaji wa kijinsia kutoka kwa wenzao
- Asilimia 30 ya wanawake walishambuliwa kingono na wenzao
- 11% ya wanawake waliripoti kulazimishwa kuwasiliana kimwili kuhusiana na nafasi za kazi
- Angalau matukio 11 ya ubakaji yaliripotiwa
- 90% ya wanawake, na 81% ya wanaume, walikuwa wameshuhudia aina fulani ya mienendo mibaya ya kingono
Ingawa ripoti inaonyesha wanaume pia wanakabiliwa kwa kiasi fulani na tabia hii (24% walikuwa wamenyanyaswa kingono), inahitimisha kuwa madaktari wa upasuaji wanaume na wanawake "wanaishi katika uhalisia tofauti".
"Matokeo yetu yanaweza kuyumbisha imani ya umma katika taaluma ya upasuaji," Dkt Christopher Begeny, kutoka Chuo Kikuu cha Exeter alisema.
Wakati huo huo ripoti ya pili - inayoitwa Kuvunja Ukimya: Kushughulikia Utovu wa Kimapenzi katika Huduma ya Afya - inatoa mapendekezo kwa kile kinachohitaji kubadilika.
Ripoti hizo mbili zinashauri uwepo wa idadi ndogo ya madaktari wa upasuaji wanawake (karibu 28%), na kwamba upasuaji ufanyika huku kukiwa na madaktari wa viwango tofauti kwani ukosefu wa utaratibu huu huwapa baadhi ya wanaume nguvu kubwa na ikichanganywa na mazingira ya shinikizo la upasuaji,
"Hiyo inasababisha watu kuwa na tabia ambayo haiadhibiwi na mengi ya haya hayadhibitiwi," Prof Carrie Newlands, mshauri wa upasuaji kutoka Chuo Kikuu cha Surrey.
Alihamasika kukabiliana na tabia kama hiyo baada ya kusikia uzoefu wa wenzake wachanga.
Aliiambia BBC: "Hali ya kawaida ni kwamba mwanafunzi wa kike ananyanyaswa na mhalifu mkuu wa kiume, ambaye mara nyingi ndiye msimamizi wake.
"Na hiyo inasababisha utamaduni wa ukimya ambapo watu wana hofu ya kweli ya maisha yao ya baadaye na kazi zao ikiwa watazungumza."
'Inasikitisha sana'
Mada nyingine iliyojitokeza katika data ilikuwa ukosefu wa imani katika miili kama vile NHS Trusts, Baraza Kuu la Madaktari (ambalo linasimamia sajili ya madaktari walioruhusiwa kufanya mazoezi ya Uingereza) na Vyuo vya Kifalme (ambavyo vinawakilisha utaalamu katika dawa) - kushughulikia tatizo.
"Tunahitaji mabadiliko makubwa katika michakato ya uchunguzi ili wachunguzi wawe wa nje na huru, na kuaminiwa ili huduma ya afya iwe mahali salama pa kufanya kazi," anasema Prof Newlands.
Tim Mitchell, rais wa Chuo cha Royal cha Madaktari wa Upasuaji cha Uingereza, aliiambia BBC kwamba matokeo ya uchunguzi huo "ni ya kushtua sana na yatakuwa chanzo cha aibu kubwa kwa taaluma ya upasuaji".
Alikiri kuwa ni "wazi ni tatizo la kawaida" ambalo halijashughulikiwa.
“Tunatakiwa kuweka utamaduni wa kutovumiliana ili kuhakikisha kunakuwa na taratibu zinazomaanisha watu wanaoathirika wanajiamini wanaweza kujitokeza, kuripoti matukio haya na wawe na uhakika kwamba yatachukuliwa kwa uzito wake,” alisema.
Dk Binta Sultan, kutoka NHS Uingereza, alisema ripoti hiyo ilifanya "tathmini ngumu sana" na kuwasilisha "ushahidi wa wazi" kwamba hatua zaidi zinahitajika ili kufanya hospitali "kuwa salama kwa wote".
Alisema: "Tayari tunachukua hatua muhimu kufanya hili, ikiwa ni pamoja na kupitia ahadi za kutoa usaidizi zaidi na mifumo ya wazi ya kutoa taarifa kwa wale ambao wameteseka kwa unyanyasaji au tabia isiyofaa."
Afisa mkuu mtendaji wake Charlie Massey alisema "kufanya mienendo ya kingono kwa wagonjwa au wenzake haikubaliki" na kwamba "makosa makubwa hayaendani" na kazi ya matibabu nchini Uingereza.
Lakini je, upasuaji ni mahali salama kwa wanawake kufanya kazi leo?
"Sio mara zote. Na hilo ni jambo gumu na baya kulikubali," anasema Judith.















