Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Video na mashahidi wanavyosema kuhusu watu wa Gaza 112 waliouawa
Takribani Wapalestina 112 waliuawa huku umati wa watu ukikimbia kuzunguka lori kuchukua msaada wa chakula uliohitajika sana majira ya Alhamisi asubuhi, kulingana na wizara ya afya inayosimamiwa na Hamas.
Mamia ya watu walishuka kwenye mstari wa magari yalipokuwa yakisafiri gizani kuelekea kaskazini kando ya barabara ya pwani nje kidogo ya Mji wa Gaza, wakisindikizwa na jeshi la Israel.
Mbali na waliofariki, watu 760 walijeruhiwa, wizara hiyo ilisema.
Tukio hilo la kusikitisha limezua madai tofauti kuhusu kilichotokea na nani alihusika na mauaji hayo.
BBC Verify imeangalia habari muhimu, iliibuka lini na kutoka wapi. Tumekagua video za mitandao ya kijamii, picha za satelaiti na picha za droni za IDF ili kuunganisha kile tunachojua na tusichojua kuhusu kile kilichotokea kufikia sasa.
Mamia wanasubiri msaada
Picha hii, iliyochapishwa kwenye Instagram mnamo tarehe 28 Februari, inaonesha baadhi ya mamia ya watu wakiwa wamekusanyika kwenye moto huku wakingojea usafirishaji wa misaada ya kibinadamu.
Umoja wa Mataifa unaonya kuhusu njaa inayokuja kaskazini mwa Gaza, ambapo takribani watu 300,000 wanaishi na chakula kidogo au maji safi, eneo hilo limepata msaada mdogo sana katika wiki za hivi karibuni.
Video hiyo inaonesha watu wamepiga kambi kwenye Mtaa wa al-Rashid, barabara ya pwani kuelekea kusini magharibi mwa Jiji la Gaza.
Ni eneo ambalo limetumika hivi karibuni kama sehemu ya usambazaji wa misaada.
Hapo awali tumethibitisha video katika eneo hilo inayoonesha watu wakikusanyika karibu na lori kudai magunia ya nafaka.
Mahmoud Awadeyah, mwandishi wa habari aliyekuwa katika eneo la tukio, aliiambia BBC: "Kulikuwa na idadi kubwa ya watu wakitafuta chakula''
Msafara unakaribia kambi
Takribani saa 04:00 alfajiri kwa saa za huko siku ya Alhamisi tarehe 29 Februari, msafara wa malori yaliyobeba msaada kutoka Misri unapitia eneo la Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF), ukielekea kaskazini kwenye Mtaa wa al-Rashid.
IDF inasema kulikuwa na malori 30 kwenye msafara huo, huku mtu aliyeshuhudia akiiambia BBC kuwa kulikuwa na 18.
Msemaji mkuu wa IDF, Daniel Hagari, alisema kuwa mwendo wa saa 10:45 malori kwenye msafara huo yalizingirwa na umati wa watu wakati magari hayo yakikaribia mzunguko wa Nabulsi, kwenye ukingo wa kusini-magharibi mwa Jiji la Gaza.
Watu wanayazingira malori
Hii ni picha ya skrini kutoka kwenye picha za droni ya infra-red iliyotolewa na IDF.
Video iliyotolewa na IDF Imehaririwa katika sehemu nne.
Inaonesha matukio katika maeneo mawili, ambayo BBC Verify imeweka kijiografia.
Sehemu mbili za kwanza za video zinaonesha watu wakizunguka malori mawili au zaidi kusini mwa mzunguko wa Nabulsi.
Sehemu nyingine mbili za video zinaonesha matukio karibu mita 500m kusini zaidi.
Zinaonesha takribani malori manne yaliyokuwa yamesimama. Tena, watu wanaweza kuonekana wakiyazunguka, lakini wakati huu inawezekana pia kuona kile kinachoonekana vile visivyo na mwendo vikiwa vimelala chini.
Picha hii ya skrini iliyofafanuliwa ya video ya IDF inaangazia watu hawa kwa miraba nyekundu.
Pia inaonesha kile kinachoonekana kuwa magari ya kijeshi ya Israeli karibu.
BBC Verify imeiomba IDF picha kamili ya tukio hilo.
Milio ya risasi
Tumekagua video ya kipekee ya Al Jazeera iliyorekodiwa karibu na eneo hilo la pili nyuma ya msafara, takribani nusu kilomita kusini mwa mzunguko.
Milio ya risasi inasikika na watu wanaonekana wakihangaika juu ya lori na kurukia nyuma ya magari hayo.
Mahmoud Awadeyah alisema magari hayo ya Israel yameanza kuwafyatulia risasi watu wakati msaada huo ulipowasili.
"Waisraeli waliwafyatulia risasi watu hao kwa makusudi... walikuwa wakijaribu kukaribia malori yaliyokuwa na unga," alisema. "Walifyatuliwa risasi moja kwa moja na kuwazuia watu kuwakaribia waliouawa."
Tumethibitisha picha zaidi zilizorekodiwa eneo ambalo ufyatuaji risasi ulitokea, picha za miili ikichukuliwa kwa mkokoteni kaskazini kuelekea Nabulsi.
Kumekuwa na ripoti za majeruhi kupelekwa katika hospitali kadhaa.
Dkt. Mohamed Salha, meneja wa muda wa hospitali ya al-Awda, ambapo wengi wa waliofariki na waliojeruhiwa walipelekwa, aliiambia BBC: "Hospitali ya Al-Awda ilipokea karibu watu 176 waliojeruhiwa...142 kati yao ni wenye majeraha ya risasi, wengine kutoka kwa mkanyagano na miguu iliyovunjika katika sehemu za juu na chini za mwili."
Ilichosema Israeli
Saa saba na dakika sita saa za huko siku ya Alhamisi, taarifa ya IDF iliyotumwa kwenye Telegram ilisema: "Mapema leo asubuhi, wakati wa kuingia kwa malori ya misaada ya kibinadamu katika Ukanda wa Kaskazini wa Gaza, wakazi wa Gaza walizingira malori, na kupora vifaa vilivyowasilishwa.
"Wakati wa tukio hilo, makumi ya raia wa Gaza walijeruhiwa kutokana na kusukumana na kukanyagwa."
Saa tisa na dakika thelathini na tano, taarifa zaidi ya IDF kwenye X, iliyokuwa Twitter, ilirudia maelezo hayo ya tukio.
Katika maoni zaidi kwa Channel 4 News ya Uingereza, msemaji wa IDF Lt Kanali Peter Lerner alisema "kundi la watu lilivamia msafara huo na kuusimamisha kwa hatua fulani.
"Vifaru vilivyokuwa pale kuulinda msafara huo vinaona Wagaza wakikanyagwa na kwa tahadhari walijaribu kuwatawanya kundi hilo kwa risasi chache za onyo."
Katika taarifa ya video iliyotumwa kwenye X huko Gaza na Israel, Daniel Hagari wa IDF alidai: "Mamia wakawa maelfu na mambo yakaharibika."
Alisema kamanda wa kifaru aliamua kurudi nyuma ili kuzuia kuwadhuru raia na "walikuwa wakizingatia usalama, sio kuufyatulia risasi umati".
Na mapema, katika mahojiano kwenye CNN kati ya saa kumi na mbili kamili jioni na saa moja kamili jioni, mshauri maalum wa waziri mkuu wa Israeli, Mark Regev, alisema Israeli haikuhusika moja kwa moja kwa njia yoyote.
Alisema IDF ilifyatua risasi katika tukio tofauti lisilohusiana na lori, lakini hakutoa ushahidi zaidi.
Bw Regev aliongeza: "Katika tukio la lori kupigwa risasi kulikuwa na milio ya risasi, hayo yalikuwa ni makundi yenye silaha ya Palestina. Hatujui ikiwa ni Hamas au wengine."
Viongozi kote duniani wametaka uchunguzi ufanyike kuhusu kilichotokea.
Inafuatia wasiwasi uliotolewa Jumanne na afisa mkuu wa Umoja wa Mataifa ambaye alionya kwamba zaidi ya watu nusu milioni kote Ukanda wa Gaza wanakabiliwa na janga la uhaba wa chakula.
Imetafsiriwa na Lizzy Masinga.