Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Bola Tinubu - 'godfather' anayetarajiwa kuongoza Nigeria
Bola Tinubu, 70, ametangazwa mshindi wa uchaguzi wenye ushindani mkubwa nchini Nigeria tangu kumalizika kwa utawala wa kijeshi mwaka 1999.
Akiwa bado anasifiwa sana kwa kuunda upya kitovu cha kibiashara cha Nigeria Lagos , Bw Tinubu alikiondoa chama cha upinzani kilichogawanyika na mgombea wa chama cha tatu anayeungwa mkono na vijana na anatazamiwa kuchukua nafasi ya Rais Muhammadu Buhari mwezi Mei, endapo madai ya upinzani ya uchaguzi huo kukumbwa na udanganyifu hayatasababisha kurudiwa kwa kura hiyo.
Nigeria nchi yenye watu wengi zaidi barani Afrika inakabiliwa na uchumi unaoporomoka, ukosefu wa usalama ulioenea na mfumuko mkubwa wa bei. Wengi watataka Bw Tinubu apige hatua atakapochukua mojawapo ya kazi za kuogofya zaidi barani Afrika.
Bw Tinubu ambaye alilazimishwa kikimbilia uhamishoni na mtawala wa kijeshi Sani Abacha, anajua thamani ya uhuru na anaivaa kama nembo kwenye kofia yake iliyotiwa saini - pingu iliyovunjika ambayo inaonekana kama namba nane iliyolazwa upande.
Ni mhasibu lakini shughuli za kundi la Muungano wa Kidemokrasia wa Kitaifa (Nadeco), ambaloo alikuwa mwanachama wake, ndizo zilizomweka kwenye mtafaruku wa Abacha.
Upinzani wa makundi kama Nadeco, na kifo cha Abacha mwaka 1998, ulileta demokrasia ya Nigeria mwaka 1999 na kwa njia nyingi, Bw Tinubu, mtendaji mkuu wa zamani wa mafuta wa Mobil, anahisi kuwa ana haki ya kugombea urais wa Nigeria.
Bw Tinubu, anayejulikana kama "Jagaban" na wafuasi wake, sasa atakuwa akiangalia kuunganisha nchi ambayo inarudi nyuma katika safu za kikanda na kambi za kidini, kama matokeo ya uchaguzi yanavyoonyesha.
Lakini sio kazi inayomsumbua. Ametumia wakati wake kama gavana wa jimbo la Lagos kati ya 1999 na 2007 kuuza ugombea wake kwa Wanigeria.
Chini ya uongozi wake, Lagos ilikuza mapato yake kwa kiasi kikubwa kupitia uwekezaji mkubwa wa kigeni, wakati mpango wa usafiri wa umma ambao uliwezesha kujengwa kwa njia mpya za mabasi ya mwendo kasi ulipunguza msongamano wa magari unaokabiliwa kila siku na wasafiri.
Lakini jiji hilo lenye takriban watu milioni 25 haliendani na sifa yake kama jiji kubwa licha ya madai yake ya kuligeuza.
Miundombinu ya umma kwa kiasi kikubwa iko katika hali mbaya - huduma za kimsingi kama vile maji na makazi ya umma ni duni, wakati mradi wa reli ulioanza wakati wa utawala wake haujakamilika karibu miaka 20 baadaye licha ya utajiri wa serikali.
Pia ameshutumiwa kwa kushikilia fedha za serikali licha ya kuondoka madarakani mwaka wa 2007.
Kila gavana ambaye amemrithi amekuwa mfuasi anayefuata "ramani kuu", huku yule aliyethubutu kutafuta njia yake mwenyewe aliwekwa chini, akisaidiwa na wanachama wenye nguvu wa chama cha usafiri.
Pia kuna madai ya ufisadi dhidi ya Bw Tinubu, ambayo anakanusha.
Miaka miwili iliyopita, Dapo Apara, mhasibu wa Alpha-beta, kampuni ambayo Bw Tinubu anadaiwa kumiliki hisa kupitia kwa mshirika wake, alimshutumu kwa kutumia kampuni hiyo kwa utakatishaji fedha, ulaghai, ukwepaji kodi na vitendo vingine vya ufisadi.
Bw Tinubu alishtakiwa licha ya yeye na Alpha-beta kukana madai hayo lakini pande zote ziliamua kusuluhisha kesi hiyo nje ya mahakama Juni mwaka jana.
Madai hayo, ikiwa ni pamoja na kukabiliwa mara mbili Mahakama ya Maadili ya Nigeria (CCT), kwa madai ya kukiuka maadili ya maafisa wa umma - ambapo aliondolewa - yanawafanya wapinzani kusema Bw Tinubu si mtu sahihi kwa kazi hiyo katika nchi ambayo rushwa imekithiri.
Katika uchaguzi uliopita, onyesho lisilo la kawaida la gari la kivita lililokuwa likitumiwa na benki kupeleka pesa kwenye jumba lake la kifahari katika eneo la Ikoyi, Lagos lilizua tuhuma kwamba alihusika katika ununuzi wa kura, jambo ambalo hakufanya juhudi kubwa kulikana.
"Kama nina pesa, nikitaka, ninawapa watu bila malipo, mradi tu [sio] kununua kura," alisema.
Ni mmoja wa wanasiasa matajiri wa Nigeria lakini utajiri wake unahojiwa.
Mnamo Desemba, aliiambia BBC kwamba alirithi mali isiyohamishika ambayo aliwekeza, lakini huko nyuma pia alisema alikua "milionea wa papo kwa hapo" wakati akifanya kazi kama mkaguzi wa hesabu wa kampuni ya Deloitte and Touche.
Alisema alikuwa amehifadhi dola milioni1.8 (£1.5m) kutoka kwa mishahara yake na marupurupu mengine, karibu kiasi sawa na hicho kilichopatikana katika akaunti zilizohusishwa naye katika mzozo wa 1993 na mamlaka ya Marekani.
Katika hati ambazo zinapatikana hadharani, Idara ya Sheria ya Marekani ilidai kuwa kuanzia mapema mwaka wa 1988, akaunti zilizofunguliwa kwa jina la Bola Tinubu zilikuwa na mapato ya mauzo ya heroini nyeupe.
Kevin Moss, ajenti maalum aliyechunguza oparesheni hiyo, alidai kuwa Bw Tinubu alimfanyia kazi mshukiwa wao mkuu Adegoboyega Akande.
Ingawa mahakama ilithibitisha kwamba ilikuwa na sababu ya kuamini kuwa pesa zilizokuwa kwenye akaunti za benki zilikuwa pesa za ulanguzi wa dawa za kulevya, Bw Tinubu na wenzake walikanusha madai hayo, na mahakama haikutoa amri ya mwisho kuhusu achanzo cha pesa hizo.
Badala yake, Bw Tinubu, ambaye hakushtakiwa binafsi kuhusu pesa hizo, alifikia maafikiano na mamlaka na kupoteza dola 460,000.
Bw Tinubu pia anakabiliwa na maswali kuhusu afya yake, wakati mmoja alizua gumzo mitandaoni alipochapisha video ya sekunde nane akiendesha baiskeli ya mazoezi kama uthibitisho wa uimara wa afya yake.
Wapinzani wanasema umri wake umekwisha na kutumia video mbalimbali za kejeli kwenye mikutano ya kampeni ambapo inaweza kuwa vigumu kuelewa anachosema.
Raia wengi wa Nigeria wanahofia rais mwingine mwenye matatizo ya kiafya baada ya Rais Umaru Yar'Adua kufariki akiwa madarakani mwaka 2010 na rais wa sasa ambaye ametumia muda mrefu kupata matibabu nje ya nchi.
Lakini wafuasi wake wanasema ana nguvu ya kufanya kazi hiyo na hagombei nafasi kwenye mashindano ya Olimpiki.
Wakati wa kampeni, kulikuwa na utata kuhusu uchaguzi wake wa mgombea mwenza.
Bw Tinubu, Muislamu wa kusini, alimchagua gavana wa zamani wa jimbo la Borno Kashim Shettima, Muislamu wa kaskazini, kuwa makamu wake.
Hatua hii ilionekana kuwafurahisha waislamu wengi kaskazini mwa Nigeria ambao wajivunia kuwa na idadi kubwa zaidi ya wapiga kura nchini humo.
Hata hivyo, iliibua hasira za Wakristo wengi wanaosema inakwenda kinyume na mila ya watu wenye imani tofauti kuwania urais.
Alitetea chaguo lake, akisema alianzaia umahiri badala ya masilahi ya awali.
Anaonekana kama "godfather" wa kisiasa wa eneo la kusini-magharibi na mtu wake mwenye ushawishi mkubwa zaidi, ambaye anaamua jinsi nguvu inavyosambazwa kati ya washirika wake wengi.
Mnamo 2015 alijielezea kama "mwindaji wa talanta" ambaye anaweka "talanta ofisini".
Ushawishi wake mkubwa wa kisiasa ulisababisha kuunganishwa kwa vyama vya upinzani mwaka 2013 na hatimaye kushindana na chama tawala cha PDP mwaka 2015 - jambo ambalo ni nadra sana nchini Nigeria ambako viongozi walio madarakani hawashindwi mara kwa mara.
Wakati wa mchujo wa chama chake, ilipoonekana kana kwamba matarajio ya Bw Tinubu yalikuwa yakififia, aliwakumbusha Wanigeria kwamba alihusika pakubwa kumteua Rais Muhammadu Buhari baada ya mtawala huyo wa zamani wa kijeshi kushindwa mara kadhaa kushinda urais.
Washirika wa Bw Buhari tangu wakati huo wamejaribu kupuuza ushawishi wa gavana huyo wa zamani katika uchaguzi wa 2015, lakini kuna uwezekano kwamba rais wa sasa angeibuka, mara mbili, bila kuungwa mkono na Bw Tinubu.
Ndiyo maana wafuasi wake waliona kuwa ni usaliti wakati Makamu wa Rais Yemi Osinbajo, ambaye alifanya kazi na Bw Tinubu kama kamishna mjini Lagos, aliposhindana na bosi wake wa zamani kwa tiketi ya APC.
Baada ya kushinda uchaguzi, atalazimika kushughulikia masuala mengi yaliyoachwa nyuma na Bw Buhari - ukosefu wa usalama ulioenea, ukosefu mkubwa wa ajira, kupanda kwa mfumuko wa bei na nchi iliyogawanyika kwa misingi ya kikabila.
Sio kazi isiyowezekana, lakini kazi iliyo mbele yake ni ngumu.