Maandamano Iran: BBC yatambua watu zaidi waliouawa kwenye maandamano baada ya kifo cha Mahsa Amini

"Nisipotoka nje kuandamana, nani mwingine atafanya hivyo?" Maneno ya mwisho ya Minoo Majidi kwa familia yake kabla hajafa.

Minoo alikuwa na umri wa miaka 62 alipopigwa risasi na vikosi vya usalama katika mitaa ya Kermanshah magharibi mwa Iran.

Kulingana na bintiye, alipigwa risasi zaidi ya 167. Alikufa hospitalini.

Kufuatia kifo cha Minoo, binti yake Roya Piraei alichapisha picha ya Instagram iliyopigwa karibu na kaburi la mamake.

Akiwa amenyolewa nywele, alikuwa ameshika nywele zake mwenyewe kama ishara ya kuomboleza na kukaidi, Ilisambaaa kwa kasi.

"Nilijua singeweza kuongea. Hili tu ndilo jambo ningeweza kufanya kuonyesha jinsi mfumo huu ulivyo katili," Roya aliiambia BBC 100 Women.

Mamake Roya ni mmoja wa mamia ya Wairan ambao wameuawa kote nchini walipokuwa wakiandamana kupinga kifo cha Mahsa Amini akiwa kizuizini.

Mwanamke huyo wa Kikurdi mwenye umri wa miaka 22 alizuiliwa kwa madai ya kutofuata sheria kali ya mavazi ya kufunika kichwa kwa kutumia hijabu ambayo ni ya lazima kwa wanawake.

Maafisa wa serikali wamekiri zaidi ya watu 300 wamekufa wakati wa maandamano hayo, lakini takwimu zao ni pamoja na vikosi vya usalama na watu wanaounga mkono serikali.

Kwa mujibu wa Mashirika ya Kutetea Haki za Kibinadamu nchi Iran, kufikia tarehe 29 mwezi Novemba takriban watu 448 wameuawa na vikosi vya usalama, wakiwemo wanawake 29 na watoto 60.

Mashirika hayo yanaamini kwamba idadi halisi ya watu waliouawa iko "juu zaidi", kwani zinajumuisha visa ambavyo wameweza kuthibitisha na wamepokea ripoti nyingi za vifo, ambazo wanaendelea kuchunguza.

Kutambua wafu

Kwa kutumia mbinu makini za uchunguzi, timu kutoka BBC zimeweza kuthibitisha utambulisho wa zaidi ya 75 ya waliouawa.

Kwa kutpekua rekodi rasmi, tovuti na mitandao ya kijamii tulipata vyeti vya vifo, picha za mazishi na picha za kutisha za marehemu.

Pia tulizungumza na jamaa, wanaharakati na makundi vya kutetea haki za binadamu ili kuthibitisha na kuhakiki taarifa tulizopata.

Utafiti wetu ulithibitisha wengi wa waliofariki ni wanawake, na kwamba idadi kubwa ya waliouawa wanatoka katika makabila madogo yaliyotengwa.

Vifo hivyo ni pamoja na watoto wenye umri wa miaka saba. Pia tulibaini kuwa baadhi ya watu waliouawa walinaswa kwenye machafuko makubwa yanayozunguka maandamano, badala ya kuhusika moja kwa moja katika maandamano wenyewe.

Jamii za wachache zaathiriwa zaidi

"Ninaamini kuwa kinachoendelea Iran si maandamano tena. Yalianza kama maandamano, lakini mapinduzi yanafanyika," anasema Roya.

Roya anatoka katika jamii ya Wakurdi. Utafiti wetu umeonyesha maeneo ya Wakurdi, pamoja na maeneo ya makazi ya makabila mengine madogo - kama vile Baluch katika mkoa wa kusini-mashariki wa Sistan Baluchistan - yameshuhudia idadi kubwa zaidi ya vifo.

32 kati ya majina tuliyothibitisha yalitoka maeneo ya Wakurdi, huku 20 yakitoka mkoa wa Sistan Baluchistan.

Sistan Baluchistan ni mojawapo ya majimbo maskini zaidi ya Iran, na mojawapo ya majimbo ya kihafidhina.

Wengi wa watu wa Baluch ni wa madhehebu ya Sunni walio wachache nchini Iran.

Kulingana na makundi ya kutetea haki za binadamu, wanakabiliwa na ubaguzi kwa misingi ya dini na kabila. Licha ya uhafidhina wake, katika wiki za hivi karibuni wanawake wamejiunga na maandamano katika mji mkuu wa jimbo la Zahedan.

Katika video za mtandaoni, wanawake waliovalia vazi lililofunika mwili mzima - chador - wanaonekana wakiimba, "iwe na hijabu au bila hijabu, na tunaendelea mbele na mapinduzi."

Hasti Narouei mwenye umri wa miaka 7 pia alikuwa wa jamii ya Baluch.

Picha hii inamuonyesha akiwa amevalia vazi la kitamaduni la Baluchi.

Mnamo tarehe 30 Septemba, alikuwa Zahedan pamoja na bibi yake kwenye sala ya Ijumaa.

Picha za mitandao ya kijamii kutoka siku hiyo zinaonyesha vikosi vya usalama vikijibu maandamano kwa kufyatua risasi kwenye umati.

Kulingana na wanaharakati wa eneo hilo, Hasti alipigwa kichwani na mtungi wa gesi ya kutoa machozi. Alikosa hewa.

Alikuwa binti pekee wa wazazi wake. Alikuwa na kaka wawili, na alikuwa amebakisha wiki moja tu kufikia siku yake ya kwanza shuleni.

Shirika la Amnesty International linasema takriban watu 66 waliuawa siku ambayo Hasti alifariki, wakiwemo watoto 10 waliokuwa wa jamii ya wachache ya Baluchi.

Ilikuwa siku mbaya zaidi kuwahi kushuhudiwa tangu maandamano yaanze. Wanaharakati wameipa jina la "Bloody Friday".

Changamoto za uthibitishaji

Ilikuwa changamoto kwa BBC, kugundua utambulisho wa wale waliouawa katika jimbo la Sistan Baluchistan kulikuwa na safu nyingine ya utata.

Kama mojawapo ya majimbo ya kihafidhina nchini Iran, watu kwa kawaida hawako mtandaoni, na karibu hakuna uchapishaji wa kawaida wa mitandao ya kijamii ambao umewezesha utambulisho wa wengine waliokufa kushirikiwa.

Familia ya Hasti, kwa mfano, haijazungumza hadharani kuhusu binti yao isipokuwa kwenye vyombo vya habari vya serikali vinavyodhibitiwa vikali.

Mkoa pia una miundombinu dhaifu ya mtandao, na wachache wanaweza kufikia au kutegemea miunganisho ya mtandao wa nyumbani.

Kati ya watu 20 ambao BBC ilithibitisha kuwa waliuawa katika mkoa wa Sistan Baluchistan, wengi walionekana kutokuwa na mitandao ya kijamii au uwepo mwingine mtandaoni.

Picha zao za baada ya maiti ndiyo rekodi pekee ya kuona ya utambulisho wao tulioweza kupata.

Jukumu la mitandao ya kijamii

Kwingineko nchini, katika maeneo yenye matumizi makubwa ya intaneti, mitandao ya kijamii imewezesha vifo kuangaziwa zaidi.

Fereshteh Ahmadi mwenye umri wa miaka 32, kutoka Mahabad katika jimbo la Azabajani Magharibi, alikuwa mmoja wa wanawake watatu wa Kikurdi tuliowatambua.

Tarehe 26 Oktoba, maandamano yalifanyika kote nchini kuadhimisha siku ya 40 ya maombolezo ya Mahsa Amini.

Fereshteh alifariki baada ya vikosi vya serikali kudaiwa kumpiga risasi kifuani alipokuwa juu ya paa la nyumba yake.

Serikali imekanusha hili. Mamlaka ya upelelezi imeita familia yake kuhojiwa.

Picha kutoka kwa mazishi ya msichana mdogo anayedhaniwa kuwa binti wa Fereshteh, Bawan, akilia huku akiwa ameshikilia kiganja cha udongo kutoka kwenye kaburi la mama yake, ilishirikiwa sana katika majukwaa ya kijamii na kutazamwa mara nyingi zaidi.

Katika Instagram ya BBC Kiajemi pekee, picha hiyo ilitazamwa na zaidi ya watu milioni 2.5 na kupokea zaidi ya likes 198K.

Waandamanaji katika mji wa kaskazini-mashariki wa Mashad hata walianza kutumia picha yake kwenye mabango kuangazia masaibu ya watoto wengine ambao wamepoteza wazazi wao.

Hakuna nafasi ya kuomboleza

Nyuma ya nambari na picha hizo ni familia zilizo katika hali ya mshtuko na huzuni.

Katika hali nyingi, hawawezi kusema kwa sababu ya kuogopa kuadhibiwa.

Kwa usalama sasa akiwa nje ya Iran, Roya anamkumbuka mama yake Minoo.

Anakumbuka hamu yake ya maisha, utulivu wake usio na mwisho na uvumilivu."

Alikuwa mwanamichezo na alipenda kuendesha farasi. Hata alifundisha ping-pong!" anasema."

Lakini sijisikii kama nimepata nafasi ya kuomboleza kifo chake. Haikuwa ya kawaida.

"Matumaini pekee niliyonayo sasa ni kwamba Iran itakuwa huru siku moja. Kwamba wale waliouawa bila ya haki, hawakufa bure.

Watu wa Iran wanastahili kuwa na maisha ya kawaida.

Mbinu

Ramani inayoonyesha maandamano kote Iran iliundwa kwa kutumia data iliyothibitishwa na Mradi wa Vitisho Vikuu (CTP).

Mradi huu unapeana kiwango cha kujiamini (cha juu, cha wastani au cha chini) ili kuwasilisha tathmini yao ya uwezekano kwamba maandamano yalitokea siku mahususi na katika eneo mahususi.

BBC imetumia maandamano yaliyothibitishwa kutoka kwa seti ya data ya juu na ya wastani.

CTP hutumia picha na video za mitandao ya kijamii na kuripoti kutoka vyombo vya habari vya serikali ya Iran kutathmini tarehe, eneo na ukubwa wa maandamano.

CTP, ambao wamekuwa wakifuatilia maandamano tangu 2017, wameweka kizingiti chao cha kuripoti kama mkusanyiko wa watu dazeni.

Uchunguzi wa BBC mwezi Oktoba ulitaja jumla ya wanaume, wanawake na watoto 45 waliofariki katika maandamano ya Iran.

Katika hafla hiyo, wanahabari walitumia mbinu zile zile tulizotumia hapa, kuanzia na utafiti wa chanzo huria na kisha kuendelea na kuwasiliana na vyanzo, makundi vya haki, jamaa, wanaharakati, na BBC Idhaa ya Kiajemi kukusanya na kuchunguza data.

Picha za maiti au picha za mazishi pia zilipatikana katika visa vyote.

Picha hizo zilitolewa kutoka kwa mitandao ya kijamii, mashirika ya haki za binadamu au vyombo vya habari vya ndani.

Ripoti ya Lara Owen, Firouzeh Akbarian na Khosro Kalbasi Isfahani.

Uthibitishaji na Firouzeh Akbarian, Khosro Kalbasi Isfahani, Soroush Pakzad na Nooshin.

Uandishi na Uandishi wa Habari Unaoonekana na Leoni Robertson na Raees Hussain.

Imeandaliwa na Rebecca Skippage.