Afghanistan: Nini kimebadilika mwaka mmoja baada ya Taliban kurudi

Mwaka mmoja uliopita, wapiganaji wa Taliban waliingia katika mji mkuu wa Afghanistan Kabul, huku vikosi vya kigeni vikikamilisha uondokaji wao haraka nchini humo.

Akizungumza kwa niaba ya Taliban wakati huo, Zabihullah Mujahid alitoa ahadi kadhaa kwa ajili ya serikali mpya.

Je utawala huo umetimiza ahadi zake?

'Tutawaruhusu wanawake kufanya kazi na kusoma.... wanawake watakuwa watendaji sana, lakini ndani ya mfumo wa Uislamu.'

Utawala uliopita wa Taliban, katika miaka ya 1990, uliminya kwa kiasi kikubwa uhuru wa wanawake na tangu Taliban walipochukua mamlaka mwaka jana, mfululizo wa vikwazo vimewekwa tena kwa wanawake nchini Afghanistan.

Kanuni za mavazi na sheria za kutoka na kufika katika maeneo ya umma bila kusindikizwa na mwanaume zimetekelezwa.

Mnamo Machi, shule zilifunguliwa tena kwa mwaka mpya wa masomo, lakini Taliban walibatilisha ahadi ya awali na wasichana kwa sasa hawaruhusiwi kuhudhuria shule ya sekondari.

Kundi la Taliban limelaumu ukosefu wa walimu wa kike na haja ya kupanga kutenga vifaa.

Hii imeathiri takriban wanafunzi milioni 1.1, kulingana na UN na imezua ukosoaji mkubwa wa kimataifa.

Elimu ya shule ya msingi kwa wasichana imeruhusiwa.

Baadhi ya vyuo vikuu vya umma vilifunguliwa tena kwa wanaume na wanawake mwezi Februari.

Lakini ushiriki wa wanawake katika nguvu kazi umeshuka tangu Taliban kuchukua mamlaka majira ya joto yaliyopita, kwa mujibu wa Benki ya Dunia.

Ushiriki wa wanawake katika nguvu kazi uliongezeka kutoka 15% hadi 22% katika muda wa muongo mmoja tu, kati ya 1998 na 2019.

Walakini, huku Taliban ikiweka vizuizi zaidi kwa harakati za wanawake nje ya nyumba tangu kurudi kwao madarakani, asilimia ya wanawake wanaofanya kazi nchini Afghanistan ilipungua hadi 15% mwaka 2021.

Ripoti ya Amnesty mwezi Julai ilisema kwamba Taliban "wamepunguza haki za wanawake na watoto" nchini Afghanistan. Iliangazia unyanyasaji na mateso waliyofanyiwa baadhi ya wanawake ambao walikuwa wameshiriki katika maandamano dhidi ya vikwazo vipya vilivyowekwa kwao.

'Tutafanya kazi...ili kufufua uchumi wetu, kwa ujenzi wetu, kwa ustawi wetu.'

Mwezi Juni, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa liliripoti kuwa uchumi wa Afghanistan ulikuwa umepungua kwa wastani wa 30% -40% tangu Talibani kuingia kuchukua madaraka mwezi Agosti mwaka jana.

Tathmini ya chombo rasmi kinachosimamia juhudi za ujenzi mpya unaofadhiliwa na Marekani nchini Afghanistan ilihitimisha kuwa ingawa baadhi ya misaada ya kimataifa inaendelea kuingia nchini humo, hali ya kiuchumi bado ni "mbaya."

Kusitishwa kwa misaada mingi ya kimataifa na kufungiwa kwa upatikanaji wa akiba ya fedha za kigeni nchini Afghanistan kumekuwa na madhara makubwa ya kiuchumi kwa nchi hiyo.

Ili kufidia, Taliban wametaka kuongeza mapato ya kodi, pamoja na kuongeza mauzo ya nje ya makaa ya mawe na kuchukua fursa ya kupanda kwa bei kimataifa.

Bajeti ya miezi mitatu iliyotangazwa Januari mwaka huu ilionyesha Taliban walikuwa wamekusanya karibu dola milioni 400 katika mapato ya ndani kati ya Septemba na Desemba 2021. Lakini wataalam wameibua wasiwasi kuhusu kukosekana kwa uwazi katika jinsi takwimu hizi zilivyokusanywa.

Kukosa usaidizi wa kimataifa, changamoto za kiusalama, masuala yanayohusiana na hali ya hewa na mfumuko wa bei wa chakula duniani vyote vinachangia kuzorota kwa kasi kwa hali ya uchumi.

'Hakutakuwa na uzalishaji wa dawa nchini Afghanistan….tutakomesha uzalishaji wa opium tena.'

Ahadi ya Taliban ya kukabiliana na kilimo cha mimea ya opium inaakisi sera waliyoianzisha kwa mafanikio fulani walipokuwa madarakani zaidi ya miongo miwili iliyopita.

Opium hutumika kutengeneza dawa za kulevya aina ya heroini na Afghanistan imekuwa, hadi sasa, chanzo kikubwa zaidi cha uzalisha wa opium duniani kwa miaka mingi.

Mnamo Aprili mwaka huu, Taliban ilitangaza kupiga marufuku upandaji wa maua ya mimea hiyo.

Hakuna takwimu dhabiti kuhusu jinsi mpango huo wa kukomesha huko umekuwa ukiendelea, ingawa ripoti kutoka kwa baadhi ya maeneo yanayolima opium katika jimbo la Helmand kusini zinaonyesha kuwa Taliban wamekuwa wakiwalazimisha wakulima kuharibu mashamba ya mimea hiyo.

Ripoti rasmi ya Marekani mwezi Julai ilibainisha kuwa ingawa Taliban walijiweka katika hatari ya kupoteza uungwaji mkono kutoka kwa wakulima na wengine wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya, "wanaonekana kujitolea kupiga marufuku mihadarati."

Hata hivyo, Dk David Mansfield, mtaalam wa uchumi wa madawa Afghanistan, anasema zao kuu la opium lilikuwa tayari limevunwa wakati marufuku ilipowekwa.

"Zao la pili [la mwaka] kusini magharibi mwa Afghanistan kwa kawaida ni zao dogo... hivyo uharibifu wake... hautakuwa na madhara makubwa," anasema Dk Mansfield.

Inafaa pia kuzingatia kuwa uzalishaji na utengenezaji wa dawa zingine, kama vile crystal meth, umekuwa ukiongezeka, ingawa Taliban wamepiga marufuku mmea wa porini (ephedra) unaotumiwa kutengeneza.

'Sisi [Wataliban] tumejitolea kuhakikisha usalama.'

Ingawa mzozo uliowaleta Taliban madarakani kwa kiasi kikubwa umekwisha, bado kulikuwa na zaidi ya madhara kwa raia 2,000 (vifo 700 na zaidi ya majeruhi 1,400) vilivyoripotiwa kati ya Agosti mwaka jana hadi katikati ya Juni mwaka huu, kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa.

Hata hivyo, takwimu hizi ziko chini sana ikilinganishwa na miaka ya nyuma wakati mzozo ulikuwa juu.

Takriban 50% ya waathirika tangu Agosti 2021 walihusishwa na vitendo vya kundi la Islamic State-Khorasan (IS-K), tawi la kundi la Islamic State ambalo bado linaendelea nchini Afghanistan.

Katika miezi ya hivi karibuni, mashambulizi kadhaa ya IS-K yamefanyika yakiwalenga raia, haswa katika maeneo ya mijini yenye Waislamu wa Shia au watu wengine walio wachache.

Uwepo wa vikosi vingine vya kupambana na Taliban, kama vile National Resistance Front (NRF) na Afghanistan Freedom Front (AFF), pia umeongezeka.

"Mazingira ya usalama kwa ujumla yanazidi kuwa yasiyotabirika," ilisema Umoja wa Mataifa mwezi Juni, ikitoa mfano wa kuwepo kwa angalau makundi ya wanamgambo kadhaa wanaopinga Taliban ambao wako nchini humo.

Pia kumekuwa na ongezeko kubwa la ukiukaji wa haki za binadamu, ikiwa ni pamoja na mauaji ya kiholela, kuwekwa kizuizini na kuteswa yanayofanywa na kundi la Taliban, kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa.

Kati ya Agosti 2021 na Juni 2022, ilirekodi mauaji yasiyopungua 160 ya maafisa wa zamani wa serikali na kikosi cha usalama.