"Tunaupokea uamuzi wa TCRA hata kama hatukubaliani nao" – JamiiForums

.

Chanzo cha picha, Maxence Melo

Muda wa kusoma: Dakika 4

Muasisi wa JamiiForums, Maxence Melo, amesema jukwaa hilo linalazimika kukubali uamuzi wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kusitisha leseni yake ya maudhui kwa siku 90, japokuwa hawakubaliani nao.

"Tunalazimika kupokea uamuzi wa TCRA hata kama hatukubaliani nao. Tunatii mamlaka za nchi tunakotoa huduma. Hivyo, JamiiForums haipatikani kwa wateja wetu wa Tanzania," Melo maarufu kama Max ameiambia BBC.

Amesema hata hivyo, utekelezaji wa sheria unapaswa kufuata taratibu zilizowekwa na Kanuni. "Kanuni zinataka aliyeathirika na maudhui kuripoti mwenyewe, mtoa huduma achukue hatua; kwetu haikuwa hivyo. Mlalamikaji ni Mamlaka, sio Rostam anayedaiwa kutosikilizwa. Bahati mbaya kuna wenzetu waliompa nafasi Rostam wakamnyima nafasi Polepole, hao hawajaguswa," aliongeza.

TCRA ilitangaza kusitisha leseni ya maudhui ya JamiiForums na kuzuia upatikanaji wake nchini kwa madai ya kukiuka Kanuni za Maudhui Mtandaoni za mwaka 2020 na marekebisho ya 2022. Mamlaka hiyo ilieleza kuwa JamiiForums ilichapisha taarifa "zisizo sahihi, za kukashifu na zenye lugha isiyofaa" dhidi ya Serikali na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kwa mujibu wa taarifa ya TCRA, hatua hiyo imechukuliwa kufuatia machapisho ya JamiiForums yaliyomnukuu mwanasiasa Humphrey Polepole akidai kuwa mfanyabiashara Rostam Aziz anamiliki asilimia 70 ya mgodi wa makaa ya mawe.

Aidha, JamiiForums iliripoti madai yanayohusisha Rais Samia Suluhu Hassan na mfanyabiashara wa Zimbabwe, Wicknell Chivayo, pamoja na kutumia picha ambazo mamlaka inadai hazikuthibitishwa uhalisia wake. TCRA imesema JamiiForums lilishindwa kuwasiliana na msemaji wa Serikali au mamlaka husika ili kupata maoni ya upande wa pili, na hivyo "kuuaminisha umma taarifa za upande mmoja."

Kuhusu madai ya Polepole kwamba mfanyabiashara Rostam aliuziwa hisa za migodi kwa upendeleo na bei ya chini sana, ikiwemo ule wa Ngaka, chini ya kampuni ya TANCOAL, Rostam alijibu katika mahojiano yake na mwandishi mwandamizi Tido Mhando akisema kuwa alinunua kwa mwekezaji (Intra Energy Corporation Limited) "asilimia 70% kwenye soko la hisa la Australia Stock Exchange.

"Ninaposikia kapewa, kanunua bei ya chee , mimi nimenunua hii kampuni kutoka kwa mwekezaji, waliyemuamini wao (Serikali) miaka ya nyuma wakampa Muastralia, nikanunua zile hisa, na zile hisa mpaka hivi leo, hata uzalishaji hatujaanza", anasema Rostam.

s

Chanzo cha picha, The Chanzo

Maelezo ya picha, Humphrey Polepole, ambaye hivi karibuni alijiuzulu ubalozi kwa madai ya kutokukubaliana na mwenendo wa chama chake na utawala wa sasa
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Si mara ya kwanza JamiiForums inakumbwa na hatua za kisheria chini ya kanuni hizo ambazo zimekuwa zikeboreshwa mara kwa mara. Katika miaka iliyopita, jukwaa hilo limewahi kuzuiwa kwa muda kwa sababu zinazohusiana na machapisho yanayotafsiriwa na mamlaka kama ukiukaji wa masharti ya maudhui mtandaoni.

Hata hivyo hatua ya sasa imeendelea kuibua 'makelele' miongoni mwa wadau wa sheria, haki na vyombo vya habari. Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Boniface Mwabukusi, alisema uamuzi huo ni "tishio kwa uhuru wa vyombo vya habari" na unaathiri misingi ya haki na uwajibikaji.

Kanuni za maudhui mtandaoni zinazotumika sasa ni zile zilizotungwa mwaka 2020 chini ya Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta na zimekuwa zikiboreshwa kwa muda.

Wadau akiwemo Legal and Human Rights Cente (LHRC), Tanzania Human Rights Defenders (THRD), Media Council of Tanzania (MCT), Jamii Media, Tanzania Media Women's Association (TAMWA) na Tanzania Editors Forum (TEF) walizipinga Mahakamani. Na mwaka 2018, Mahakama kuu kanda ya Mtwara ilitoa zuio la muda la matumizi ya kanuni hizo ambazo matumizi yake awali yalipaswa kuanza rasmi Mei 5, 2018.

Taasisi hizo katika kesi ya msingi ya mapatio ya kanuni hizo ziliitaka Mahakama kuu kufanya mapitio ya kanuni hizo kwa kigezo kwamba zinakiuka kanuni za usawa na zinapingana na haki ya kujieleza, haki ya kusikilizwa, na haki ya usiri.

Lakini pamoja na maboresho kiasi, zilipitishwa na kuanza kutumia mwaka 2020 ambazo hata hivyo ziliendelea kukosolewa kwamba zinaminya uhuru wa habari na kujieleza.

Melo mwenyewe aliwahi kuonya mapema kupitia ukurasa wake wa Twitter kwamba baadhi ya vipengele vya kanuni hivyo vingewatia hatiani waendeshaji wa mitandao bila kosa la moja kwa moja, na akasisitiza kuwa ni muhimu mamlaka zifanyie marekebisho pale vinapominya uhuru wa kujieleza.

S
Maelezo ya picha, Chapisho la Melo la Julai 30, 2020, muda mfupi baada ya kuanza kutumika kwa kanuni Maudhui Mtandaoni (2020) ambazo sasa zimetumika kulifungia Jukwaa lake la JamiiForums.

Kwa sasa, hatua ya TCRA dhidi ya JamiiForums, jukwaa maarufu la mijadala mtandaoni nchini, inatazamiwa kendela kuibua upya mjadala kuhusu mipaka kati ya udhibiti wa serikali, uhuru wa vyombo vya habari, na wajibu wa majukwaa ya kidijitali nchini Tanzania.