'Huwachukulia kama mbwa': Wakili anayehatarisha kila kitu kuwatetea wapenzi wa jinsi moja Afrika

Muda wa kusoma: Dakika 6

Licha ya kukashifiwa, kutishiwa na kudhalilishwa hadharani, mwanasheria mkongwe wa Cameroon Alice Nkom amedhamiria kutetea haki za watu wanaoshiriki mapenzi ya jinsi moja nchini mwake hadi mwisho wa maisha yake.

Shirika lisilo la kiserikali la haki za binadamu analoliongoza, Redhac, lilisimamishwa kazi hivi majuzi na serikali, na Nkom anatazamiwa kufika mbele ya wachunguzi kujibu mashtaka ya utakatishaji fedha na kufadhili makundi ya kigaidi, madai anayokanusha.

Wakili huyo mwenye umri wa miaka 80 anasema mamlaka inazuia kazi yake na anaamini analengwa kwa ajili ya utetezi wake wa kisheria kwa jumuiya ya LGBT.

"Siku zote nitawatetea wapenzi wa jinsi moja kwasababu kila siku wanahatarisha uhuru wao na wanafungwa kama mbwa," aliambia BBC kwa sauti thabiti, akizungumza katika ofisi yake katika mji wa kusini wa Douala.

"Kazi yangu ni kutetea watu. Sioni kwanini niseme natetea kila mtu na niwabagua wapenzi wa jinsi moja."

Pia unaweza kusoma:

Akiwa amevalia vazi la rangi nyeusi, Bi Nkom anaeleza taarifa yake kwa sauti ya ukomavu ambayo inaashiria mikimbio ya sheria inayomuandama kila uchao.

Kulingana na kanuni za adhabu za Cameroon, wanaume na wanawake wanaopatikana na hatia ya uhusiano wa kimapenzi wa jinsi moja wanaweza kuhukumiwa kifungo cha hadi miaka mitano gerezani pamoja na faini.

Wanajamii wa LGBT wanakutana pia na unyanyapaa kutoka kwa familia zao na jamii kwa ujumla.

Kwa hiyo, Nkom anachukuliwa kama mama mbadala kwa baadhi ya watu katika nchi yake wanaojivunia waziwazi mwelekeo wao wa kijinsi.

Ingawa Nkom ana watoto wake, mamia, pengine maelfu, ya watu wanamchukulia kama mlinzi wao kutokana na kazi yake ya zaidi ya miongo miwili kutetea wale wanaoshutumiwa kushiriki mapenzi ya jinsi moja.

"Yeye ni kama baba yetu na mama yetu. Yeye ni mama tunayempata wakati familia zetu zinapotutenga," asema Sébastien ambaye sio jina lake halisi , mwanaharakati wa LGBT.

Nkom ni mtetezi wa kujitolea wa Ibara ya Haki za Binadamu ya Ulimwenguni, ambayo ni sehemu ya Katiba ya Cameroon, na anasisitiza kuwa uhuru dhidi ya ubaguzi kwa misingi ya mwelekeo wa kijinsia ni haki ya kimsingi inayopaswa kupewa kipaumbele kuliko sheria za adhabu.

"Haki za kimsingi hazipaswi kukandamizwa, zinapaswa kulindwa," anasema.

Msimamo huu mkali kuhusu watu wa jinsi moja umeletea masimango.

Mwanasheria huyu anasimulia kuwa alikumbana na vitisho vya kupigwa mara kadhaa mitaani na anakiri kuwa alipoanza kazi ya kisheria, alilazimika kuajiri walinzi kwa usalama wake.

Hata hivyo, safari yake ya kuwa mmoja wa viongozi wakuu wa kisheria nchini Cameroon ilianza kabla ya haya yote.

Mnamo mwaka 1969, akiwa na umri wa miaka 24, Nkom alikua mwanasheria mweusi wa kwanza nchini Cameroon, baada ya kusoma katika taifa la Ufaransa (nchi ya kikoloni) na Cameroon.

Anasema mpenzi wake wa wakati huo, ambaye baadaye alikua mume wake, alimhimiza kuendelea na masomo yake.

Kazi yake ya awali ilihusisha uwakilishi wa watu maskini, lakini ni tukio la bahati lililotokea mwaka 2003 lililomuingiza kwenye vita ya kupigania kuondoa uhalifu wa ushoga.

"Kujaribu kushiriki mapenzi ya jinsi moja"

Mwanasheria aliona kundi la vijana wakikamatwa na kufungwa pingu mitaani kwa tuhuma za kuwa wapenzi wa jinsi moja, na baada ya kupitia jalada la kesi, aligundua kuwa walikuwa wanashitakiwa kwa kuwa wapenzi wa jinsi moja.

Hali hii ilimvunja moyo na kuamsha hisia zake za haki.

Kwa Nkom, hakukuwa na shaka: watu wa jamii za jinsi moja wanapaswa kutambulika na kulindwa na Katiba kama haki za kimsingi.

"Nilijua ni lazima nipiganie kuhakikisha haki hii ya kimsingi ya uhuru inalindwa," aliongeza.

Nkom alianzisha Chama cha Kutetea wapenzi wa jinsi moja (Adefho) mwaka 2003, na tangu wakati huo ameongoza na kushiriki katika kesi nyingi.

Moja ya kesi maarufu aliyoongoza ni ya Shakiro, mchekeshaji ambaye alibadili jinsia yake, na rafiki yake, Patricia, ambao walikamatwa mwaka 2021 wakiwa wanakula kwenye mgahawa na baadaye walishitakiwa kwa "jaribio la kuwa wapenzi wa jinsi moja."

Wote walihukumiwa kifungo cha miaka mitano kwa kukiuka kanuni za adhabu na "kukera ustaarabu wa umma."

"Ni pigo kubwa sana, adhabu ya juu kabisa inayotolewa na sheria.

Ujumbe ni wazi: watu wa jinsi moja hawana uhuru nchini Cameroon," alisema Nkom wakati huo.

Shakiro na Patricia waliachiliwa kwa dhamana wakiwa wanangojea rufaa na walikimbilia uhamishoni.

Tangu wakati huo, hali ya watu wa LGBT haijabadilika kwa kiasi kikubwa.

Sébastien, mwanaharakati wa jamii ya LGBT na mratibu wa shirika linalosaidia familia za watoto wa kike, anasema hali imekuwa mbaya zaidi, hasa baada ya wimbo mmoja maarufu wa "mbolé" kuchezwa, ambao unapigia debe mashambulizi dhidi ya watu wa jinsi moja.

Wimbo huo bado unashirikishwa na kuchezwa mara kwa mara katika vilabu maarufu nchini.

"Watu wanatushambulia kwa sababu ya wimbo huu unaohamasisha uhalifu dhidi ya watu wa jinsi moja," anasema Sébastien.

Watu wa LGBT inabidi wafiche utambulisho wao wa kijinsia ili kuepuka mashambulizi.

Hata hivyo, "baadhi ya watu huweka mitego ili kufika karibu nasi na kutushambulia au kupiga ripoti kwa polisi," anasema.

Nkom anasema kuwa alipoona Brenda Biya, binti wa Rais Paul Biya, alijitokeza mwaka jana kama mpenzi wa jinsi moja, aliona kuwa huu ni wakati mzuri wa kubadili sheria.

Brenda Biya alisema alitumai kuwa uwazi wake utaleta mabadiliko katika nchi yake, kama ilivyoripotiwa na vyombo vya habari vya ndani.

Nkom anaamini kuna fursa ya mabadiliko.

"Ninatumia kesi ya Brenda kama mfano. Sasa nina kesi ambayo naweza kujitetea nayo kwa Rais," anasema.

Hata hivyo, Nkom pia amemshauri Brenda kufanya zaidi kwa ajili ya jamii ya watu wa jinsi moja nchini Cameroon.

"Brenda hajajibu tangu nilipozungumza na vyombo vya habari, lakini najua atajibu."

Kwa sasa, mtetezi huyu wa haki za binadamu anaendelea na kazi yake ya kisheria, huku akiona jaribio la hivi karibuni la kuzuia juhudi zake kama kikwazo kingine.

Lakini, hakika, si cha kutosha kumzuia kuendelea na vita aliyoianzisha tangu 2003.

Uganda imepokeaje sheria ya jinsi moja

Huku Cameroon ikionekana bado haijakubaliana kikamilifu na kuwapa uhuru watu wa jinsi moja, nchini Uganda kwenyewe tayari makundi na wanaharakati wanaounga mkono mapenzi ya jinsi wamekwenda katika Mahakama ya Kikatiba , wakitaka kubadilisha sheria hiyo mpya iliyoidhinishwa na Rais Museveni.

Katika hoja yao kwa mahakama wamesema kuwa sheria hiyo ni kinyume na inapinga haki ya kutobaguliwa, kwa kuharamisha mahusiano ya watu wa jinsia moja.

Sheria hiyo mpya iliyoidhinishwa mwaka 2023 inataja kifungo cha maisha kwa wale wanaopatikana na hatia ya kufanya mapenzi ya jinsi moja.

Lakini kwa upande mwingine, viongozi wa kidini wamemsifu Rais Museveni kwa kutia saini sheria ya kupinga mapenzi ya jinsi moja.

''Tunashukuru Rais ametia saini kuwa sheria Sheria ya Kupambana na Mapenzi ya Jinsi Moja …Nchi zinazotetea LGBTQI zimetuonyesha matokeo mabaya.

Tunamshukuru Rais kwa kutosalimu amri kwa vitisho vyao na kuilinda Uganda dhidi ya njia zao za kujiangamiza''.

Alibainisha Askofu Mkuu wa Kanisa la Uganda Samuel Kaziimba katika taarifa yake, huku viongozi wengine madhehebu makuu Uganda wakimuunga mkono.

Mada zinazofanana:

Imetafsiriwa na Maryam Mujahd