Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Lebanon: 'Mtaa wote umetokomezwa' na shambulio la anga la Israel
Emir Nader
BBC News, Beirut
Wakati mashambulizi ya anga yalipotokea Jumatatu usiku, Fouad Hassan, 74, alikuwa ameketi kwenye roshani yake kusini mwa kitongoji cha Jnah Beirut, akisoma jumbe kwenye simu yake.
Hakuna amri ya kuhama iliyotolewa na jeshi la Israel kabla ya roketi hiyo kushambulia nyumba ya watoto wake na wajukuu mwendo mfupi tu.
"Mlipuko huo ulipotokea, nilizimia," Fouad anasema. “Nilichukuliwa kupata oksijeni kutokana na moshi wa shambulio hilo. Nilipopata nafuu, nilitambua kwamba eneo lote lilikuwa limeharibiwa.”
Sasa rundo la chuma na vifusi vipo katika eneo ambako majengo ya makazi yalisimama pamoja kwa karibu. Mahali ambapo majengo bado yamesimama, mali za watu zinaweza kuonekana ndani kupitia mashimo yaliyolipuliwa kwenye kuta.
Trekta moja na takriban wanaume 40 wa eneo hilo wanafanya kazi polepole ya kuchimba na kutafuta miili chini ya vifusi.
"Angalia uharibifu - kitongoji kizima kimeangamizwa, watu hapa wamekufa," Fouad anasema, akionyesha ishara juu ya eneo la bomu. “Mjukuu wangu alifariki hapa, na mjukuu wangu bado yuko katika hali ya kukosa fahamu. Wote wawili walikuwa na umri wa miaka 23.”
Fouad ni mtu anayejulikana sana katika jamii. Muigizaji na mcheshi, ameonekana kwenye televisheni ya Lebanon na anajulikana kwa jina lake la kisanii la Zaghloul. Tunapozunguka eneo la bomu, wenyeji wanakuja kumpa mkono Fouad na kutoa rambirambi.
Akichukua simu yake mfukoni, Fouad anatuonyesha picha ya mjukuu wake, Alaa. Anaonekana kujiamini, akipiga picha akiwa amevalia gauni nadhifu la dhahabu.
"Alikuwa amechumbiwa kwa furaha, akitarajia kuolewa baada ya miezi mitatu," Fouad anasema. "Aliomba kuwa Miss Lebanon na alikatwa vipande vipande. Kwa nini? Kwa nini ulimwengu unaruhusu hili?”
Tangu Israel ianze kuzidisha mashambulizi yake ya anga dhidi ya Hezbollah mwezi Septemba , roketi zimelenga maeo bali mbali ya nchi. Ni kampeni ya kijeshi ambayo viongozi wa Israel wanahisi imewaletea ushindi mkubwa hadi sasa - baada ya kwa viongozi wakuu wa Hezbollah.
Hata hivyo pia ni kampeni ambayo imechukua maisha ya watu wengi wasio na hatia, huku kukiwa na ripoti nyingi za familia nzima kuuawa katika mashambulizi kote nchini.
Zaidi ya watu 1,900 wa Lebanon wameuawa, kwa mujibu wa takwimu za serikali, tangu Israel ilipoongeza mashambulizi ya anga. Takwimu hazitofautishi kati ya wapiganaji wa Hezbollah na raia.
Licha ya kutotoa amri ya kuhama kwa wakaazi mapema Jumatatu usiku, jeshi la Israel baadaye lilisema kwamba lilikuwa linalenga "shabaha ya kigaidi ya Hezbollah", lakini halikufafanua zaidi.
Ripoti za kwanza kutoka eneo la tukio zilidokeza kuwa sehemu ya hospitali ya Rafik Hariri, hospitali kubwa ya umma ya mji mkuu, lilipigwa, jambo ambalo jeshi la Israel lilikanusha.
Uharibifu wa hospitali hiyo ni wa juu juu, lakini kando ya barabara iliyojaa magari yaliyoegeshwa na madirisha yao yamelipuliwa, kuna kitongoji duni ambacho kililengwa.
Mtoto wa Fouad, Ahmed anajiunga nasi. Anatuonyesha picha ya mtoto wake ambaye amelazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi hospitalini hapo, uso wake ukiwa umefungwa bandeji na damu nyingi.
“Hii ilikuwa nyumba yangu;haipo sasa sasa, kama vitu vingine vingi. Hatuna mahali pa kwenda na hatuna nguo. Haya ni mauaji. Hatuna kambi hapa, hakuna Hezbollah, hakuna kitu,” Ahmed anatuambia.
Haijabainika ni kwa nini jeshi lake linachagua kutoa amri za kuondoka kabla ya baadhi ya makombora kushambulia na si mengine - lakini Israel inaposhambulia bila ya onyo katika eneo lenye makazi mengi, maafa ya watu kuwa ya kiholela na makubwa.
Fouad anatueleza jinsi alivyokuwa akicheza watoto wadogo katika mtaa huo waliouawa kwenye shambulio hilo
“Kila nilipoingia katika mtaa , walipiga kelele, ‘Babu, Babu! Umetuletea nini?' Ningewapa peremende, krisps, na popcorn. Vifo vya vinanijaza huzuni; wote walikufa. Mama yao bado amenaswa chini ya vifusi pamoja na mmoja wa watoto wake.”
Tunapoanza kuondoka mahali hapo, ukimya unaonekana miongoni mwa waliokusanyika hapo na tunaona machela iliyobeba mwili uliofunikwa ikichukuliwa na wanaochimba vifusi.
Tunaambiwa kwamba mama alipatikana karibu na mtoto wake.
Imetafsiriwa na Yusuf Jumah