Faida ya pilipili manga na mafuta ya zeituni katika vyakula tunavyokula

Chanzo cha picha, Getty Images
Pilipili manga imekuwa kiungo kinachothaminiwa kwa maelfu ya miaka kwa uwezo wake wa kuongeza ladha hata vyakula visivyo vutia.
Pilipili manga ilipandwa kwa mara ya kwanza zaidi ya miaka 3,500 iliyopita nchini India, ambapo mmea unaoizalisha ulianzia, na kuwa moja ya bidhaa zenye thamani kubwa zaidi katika ulimwengu wa kale.
Leo, wengi wetu tunanyunyiza pilipili manga kwenye chakula kama kiungo, mara nyingi kama kitu cha kawaida tu. Lakini kuongeza pilipili manga kwenye mlo wako kunaweza kuongeza zaidi ya ladha: kunaweza kuongeza kiwango cha virutubisho unachopata kutoka kwa chakula chako.
Kiungo hicho kina kemikali inayorahisisha ufyonzaji wa vitamini na virutubisho vingine kwenye damu.
Vile vile, matone madogo ya mafuta yaliyopo katika maziwa na mafuta ya zeituni pia huboresha upatikanaji wa virutubisho mwilini.
Wanasayansi wanajaribu kutumia viungo hivi kutengeneza aina mpya za vyakula vilivyoimarishwa na kuwasaidia watu ambao wana shida ya kula virutubisho vinavyohitajika ili kudumisha afya njema.
Mojawapo ya matatizo tunayokabiliana nayo hata kwa vyakula vyenye virutubisho vingi ni kama mwili wetu unaweza kufyonza vitamini na madini yanapopita kwenye mfumo wetu wa usagaji chakula.
Kwa mfano, tukila mahindi, bila shaka, kokwa zimejaa virutubisho: ni tajiri kwa ufumwele, protini, vitamini na virutubisho vidogo kama vile potasiamu.
Lakini yeyote ambaye ameangalia haja yake wakati akiwa maliwatoni baada ya kula atashangaa ni kiasi gani cha chakula kilichofyonzwa.
Safu ya nje ya nafaka yenye nta ni vigumu kwa mwili wetu kumengenya, hasa ikiwa hutaitafuna vizuri kabla ya kumeza.

Chanzo cha picha, Getty Images
"Unapokula mahindi matamu [bila kuyatafuna vizuri], hupitia njia yako yote ya utumbo na kuishia chooni, na virutubisho vyote vilivyomo hubaki hapo hapo," anasema David Julian McClements, profesa wa Sayansi ya Chakula katika Chuo Kikuu cha Massachusetts, Marekani.
Kwa bahati nzuri, kwa kutafuna mahindi matamu vizuri, tunaweza kupata virutubisho vingi ndani yake na kumengenywa.
Mfumo wa vyakula mwilini
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Mfano huu unaonyesha ukweli rahisi kuhusu chakula: ili virutubisho viweze kumengenywa na kuwa na manufaa mwilini, lazima kwanza vitolewe kutoka kwenye mfumo wa protini, wanga, mafuta, na vipengele vingine vinavyoipa chakula umbile na muundo wake.
Pia kuna vikwazo vingine vinavyoweza kuzuia usagaji wa vitamini.
Baada ya kutolewa kutoka kwenye mfumo huo wa chakula, vitamini lazima ziyeyuke kwenye umajimaji wa utumbo. Kisha zinahitaji kusafirishwa hadi kwenye utumbo mdogo, ambapo seli maalum zinazoitwa 'enterocytes' huzibeba hadi kwenye damu.
Hata hivyo, vitamini nyingi, ikiwa ni pamoja na A, D, E, na K, ambazo zimeainishwa kama vitamini mumunyifu za mafuta, zinahitaji usaidizi ili kusafirishwa hadi mahali zinapohitajika.
"Vitamini zinazoyeyuka kwenye mafuta haziyeyuki kwenye maji, kwa hivyo ukila na hakuna mafuta kwenye chakula chako, hazitayeyuka na zitapita tu kwenye njia yako ya utumbo na kutoka kwenye kinyesi chako," McClements anasema.

Chanzo cha picha, Getty Images
"Ukila [vitamini] pamoja na mafuta, hujimengenya na kuunda chembe ndogo za 'nanometriki' zinazoitwa 'micelles' ndani ya njia ya utumbo," McClements anaelezea.
"Hizi hunasa vitamini. Kisha, huzisafirisha kupitia majimaji ya utumbo hadi kwenye seli za epithelia, ambapo zinaweza kufyonzwa."
Hata hivyo, baadhi ya watu wanakabiliwa na matatizo ya ziada ya kupata vitamini kutoka kwa chakula.
Watu wenye tatizo la kumeng'enya chakula wanakabiliwa na uwezo mdogo wa kufyonza virutubisho kutokana na uharibifu wa utando wa utumbo.
Hii inaweza kusababishwa na sababu mbalimbali, kama vile ugonjwa wa utumbo mpana, maradhi ya utumbo mwembamba, tiba ya mionzi, na kemikali yaani 'chemotherapy'.
Katika kongosho sugu, wagonjwa hawawezi tena kutoa vimeng'enya muhimu vinavyohitajika kusaga mafuta, protini, na wanga.
Ugonjwa wa ini pia unaweza kuzuia kutolewa kwa nyongo kwenye utumbo mdogo. Nyongo husaidia kusaga mafuta, na bila mafuta ya lishe, mwili hauwezi kunyonya vitamini vinavyoyeyuka kwenye mafuta.
Katika hali hizi, mara nyingi inapendekezwa kuchukua vidonge vya vitamini.
Tatizo la virutubisho

Chanzo cha picha, Getty Images
"Vidonge vya vitamini na madini mengine havipaswi kutumika kote ulimwenguni na watu wengi hawavihitaji," anasema JoAnn Manson, profesa wa tiba katika Shule ya Tiba ya Harvard, ambaye amefanya tafiti kubwa kuhusu vidonge vinavyotumika kama mbadala wa madini mwilini.
Badala yake, anasema kwamba lishe bora inatosha.
Vitamini hazifyonzwi kwa urahisi zaidi zikiwa mfumo wa vidonge. Ili kushughulikia hili, wanasayansi wanabuni njia mpya za kutoa vitamini ili kuboresha ufyonzaji wake.
Nguvu ya viungo
Na hapa ndipo pilipili manga inapojitokeza.
McClements na timu yake walipoongeza pilipili manga kwenye saladi na mchuzi, waligundua kuwa hii inaongeza ufyonzaji zaidi.
Seli za utando wa utumbo kwa kawaida huwa na visafirishaji vinavyotoa virutubisho vinavyofyonzwa na kuvirudisha kwenye njia ya utumbo.
Hata hivyo, kemikali iliyopo katika pilipili manga huzuia visafirishaji hivi, na kuruhusu vitamini au karotenoidi zaidi kufyonzwa ndani ya damu.
Kisha McClements akapata ufunuo: mbinu hii ilikuwa imekuwepo kwa maelfu ya miaka.
"Tulifanya kazi kwa miaka mingi kujaribu kuboresha upatikanaji wa curcumin [kiungo kilichopo kwenye manjano]," anaelezea.
"Tulilinganisha mifumo hii yote tofauti kulingana na protini, mafuta, au wanga, na ikawa kwamba bora zaidi ilikuwa matone haya madogo ya lipidi kama maziwa yenye curcumin iliyoongezwa."
Anaelezea: "Nilikuwa nikitembea katika mji wetu na walikuwa wakitangaza 'maziwa ya dhahabu'. Ilikuwa kinywaji cha kitamaduni na cha kale cha India. Kimsingi, ni ule ule tuliyoiunda, lakini waliitengeneza miaka elfu moja iliyopita."

Chanzo cha picha, Getty Images
McClements na wenzake wameonyesha kuwa viwango vya juu vya curcumin vinaweza kuongezwa kwenye maziwa ya ng'ombe na kutoharibika kwa takriban wiki mbili ikiwa itahifadhiwa kwenye jokofu.
Hivi majuzi, pia wamekuwa wakijaribu kuongeza mchanganyiko huu kwenye maziwa yaliyotokana na mimea.
Lakini je, kuna chochote tunachoweza kufanya ili kuongeza unyonyaji wetu wa vitamini?
Kulingana na McClements, ikiwa utakunywa vidonge vya vitamini, inashauriwa kuvitumia pamoja na mlo wenye mafuta mengi.
"Inapaswa kuwa kitu chenye chembe ndogo za mafuta, kama vile maziwa au mtindi," anapendekeza.
Umuhimu wa kiungo cha juu
Pia ni muhimu kutambua kwamba ingawa mimea ina vitamini nyingi zenye afya, mara nyingi huwa na "virutubisho": molekuli ambazo zinaweza kuingilia uwezo wa mwili wa kufyonza virutubisho fulani.
Kwa mfano, brokoli zina glukosinolati, ambazo zinaweza kuingilia ufyonzaji wa iodini.
Kwa upande mwingine, mboga za majani zina wingi wa oksalati ambayo hufungamana na kalsiamu na kuzuia ufyonzaji wake.
Hata hivyo, mradi tu aina mbalimbali za mimea zinatumiwa, faida za kiafya za vyakula hivi huzidi athari zozote mbaya za lishe.
Hatimaye, ikiwa unataka kufurahia saladi yenye juisi na tamu, chaguo la kiungo cha juu au mafuta linaweza kuleta tofauti kubwa.
Utafiti wa hivi karibuni uliofanywa na McClements na mwenzake Ruojie Zhang, kutoka Chuo Kikuu cha Missouri, ulibaini kuwa kuchanganya sukumawiki (mboga yenye lishe nyingi iliyo na karotenoidi na vitamini C na E) na mafuta ya zeituni kunaweza kusaidia mwili kutumia virutubisho hivyo vyema.
Ugunduzi huo unaweza kuwa moja ya sababu kwa nini lishe zenye mafuta mengi ya zeituni pamoja na matunda na mboga mboga, huwa na afya njema.
Imetafsiriwa na Ambia Hirsi na kuhaririwa na Ambia Hirsi








