Je, Arsenal wana tatizo la kadi nyekundu - na je tatizo hilo linaweza kuwagharimu ubingwa?

Mikel Arteta alisema ni "ajali iliosubiri kutokea" - lakini je, tatizo la kadi nyekundu la Arsenal linaweza kuwa na gharama gani kwa matumaini ya The Gunners ya kutwaa ubingwa?
Mechi nane pekee ndani ya msimu mpya wa Premier League na tayari wachezaji watatu wa Arsenal wamepewa kadi nyekundu.
William Saliba ndiye aliyekuwa wa hivi punde zaidi kuonyeshwa kadi nyekundu baada ya kutimuliwa kwa mara ya kwanza katika maisha yake ya soka katika mchezo wa Jumamosi waliopoteza kwa mabao 2-0 dhidi ya Bournemouth, jambo ambalo lilihitimisha hatua ya Arsenal ya kucheza bila kushindwa.
Wachezaji wengine wawili wa Arsenal, Declan Rice na Leandro Trossard mapema kwenye kampeni ya Arsenal walipatiwa kadi nyekundu na kila wachezaji wake wanapopata kadi hiyo wamepoteza pointi.
Alipoulizwa kwenye Mechi Bora ya Siku kama Arsenal wana tatizo la kinidhamu baada ya kupoteza Jumamosi, mshambuliaji wa zamani wa Uingereza Alan Shearer alisema "lazima kuwe na mabadiliko".
Aliongeza: "Ni wazi kabisa hawatapata pointi za kutosha kama hawatabadilika - umeona michezo ambayo imefanyika tayari msimu huu, wakiwa na sare mbili na kupoteza mechi moja.
"Haiwezi kuendelea."
Hakika, waliachwa na "kazi ya zaida" kufuatia kutimuliwa kwa Saliba dakika ya 30, kulingana na Arteta, lakini je, rekodi ya nidhamu ya The Gunners pia inaweza kuwa mbaya kwa matarajio yao makubwa?
"Kuna mambo tumezungumza"
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kwa muda mfupi, kadi nyekundu ya Saliba ni pigo kwa sababu atakosa mchezo wa nyumbani dhidi ya vinara wa sasa wa Ligi Kuu ya Uingereza Liverpool tarehe 27 Oktoba.
The Gunners kwa sasa wako nyuma ya Liverpool kwa pointi moja kwenye jedwali, lakini baada ya kikosi cha Arne Slot kuishinda Chelsea Jumapili na kisha kuifunga Arsenal, kitasonga mbele kwa pointi saba zaidi ya kikosi cha Arteta.
Mabingwa Manchester City pia wanaweza kupanda juu zaidi ya Arsenal - wapinzani wao wa karibu zaidi katika misimu miwili iliyopita - kwa ushindi dhidi ya klabu ambazo hazijapata ushindi Wolves na Southampton katika mechi zao mbili zijazo.
"Kucheza kwa dakika 65 na wachezaji 10 katika kiwango hiki ni kazi isiyowezekana. Ni ajali inayosubiriwa kutokea ili kutopata pointi," alisema Arteta.
Kwa upande wake masuala ya nidhamu, Mhispania huyo aliongeza: "Kuna mambo ambayo tumejadili kuhusiana na mada fulani. Hakika tunahitaji kucheza na 11 ikiwa tunataka kuwa katika nafasi tunayotaka kuwa.
"Nilifikiri tulichofanya na wachezaji 10 kilikuwa cha ajabu sana."
Kama kadi nyekundu zilizoonyeshwa msimu huu kwa Trossard dhidi ya Manchester City na Rice huko Brighton kwa kuchelewa kuendeleza mechi, mchezo wa Saliba ulikuwa wa kuepukika, huku pasi ya Trossard ikizua hali ambayo mchezaji mwenzake hakuweza kuokoa.
Kiungo Rice alisema "anajivunia" wachezaji wenzake kwa pambano waliloonyesha lakini akaghairi "ujinga" ambao hatimaye uligharimu.
"Tumejiharibia mara tatu katika mechi nane," alisema.
"Hatuwezi kufanya makosa ya kipumbavu. Unahitaji wachezaji wako wote bora uwanjani wakati wote. Imani ni kubwa na tutashikamana."
Je, rekodi yao ya kadi nyekundu inalinganishwaje na washindi wa taji la hapo awali?

Habari zinazoitia wasiwasi Arsenal ni kwamba kukusanya kadi nyekundu hakusaidii uwezekano wa timu kutwaa ubingwa.
Manchester City wameshinda Ligi ya Premia katika misimu yote minne iliyopita na hawajawahi kuwa na zaidi ya kadi mbili nyekundu katika mojawapo ya kampeni hizo.
Kwa kweli, mara ya mwisho walikuwa na zaidi - nne mnamo 2019-2020 - ilikuwa wakati Liverpool ilishinda taji badala yake.
Itabidi urejee msimu wa 2015-16 - wakati Leicester ilipopata ushindi wa kihistoria iliposhinda Ligi ya Premia ikiwa na kadi nyekundu nyingi kama Arsenal ilivyo sasa.
Hata hivyo, Foxes walionyeshwa kadi zao nyekundu tatu katika msimu mzima.
Arsenal tayari wanahesabu gharama, wakiwa wamepoteza jumla ya pointi saba kufuatia matukio hayo - ambapo wangeweza kuanza vyema huku wakisaka taji la kwanza la ligi kwa zaidi ya miaka 20.
Ni mara ya kwanza tangu 2011-2012 kwa wachezaji wa Arsenal kutolewa nje kwa kadi nyekundu katika mechi nane za ufunguzi wa msimu wa Premier League.
Kadi nyekundu hazikuizuia Arsenal ya Wenger

Chanzo cha picha, Getty Images
Wachezaji kupewa kadi nyekundu limekuwa suala nyeti katika kipindi cha Arteta akiwa uwanja wa Emirates.
Tangu alipochukua ukufunzi siku ya Boxing Day 2019, The Gunners wameonyeshwa kadi 18 nyekundu kwenye ligi ya Premier , ambazo ni angalau tano zaidi ya timu nyingine yoyote wakati huo.
Ni suala ambalo amezungumza hapo awali. Mnamo Januari 2022, baada ya kadi tatu nyekundu katika michezo minne mwezi huo, Arteta alisema: "Tulicheza [mechi] tatu zilizopita na wachezaji kumi. Unapofanya hivyo ni vigumu kushinda mechi."
Hata hivyo, rekodi mbaya ya utovu wa nidhamu haikuizuia Arsenal iliposimamiwa na gwiji wa klabu hiyo Arsene Wenger.
Mfaransa huyo alishinda Ligi ya Premia mara tatu akiwa na The Gunners na mara zote tatu timu yake ilipata angalau kadi tatu nyekundu. Mnamo 2001-02 walishinda hata taji licha ya kutimuliwa mara sita katika kampeni hiyo.
Jumla ya kadi nyekundu 78 zilionyeshwa katika mechi 828 za Premier League chini ya Wenger.
Imetafsiriwa na Seif Abdalla












