Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Nne kwa moja - mechi za mchujo za kufuzu kwa Kombe la Dunia kwa timu za Afrika hufanyikaje?
Wagombea wanne watapunguzwa hadi mmoja katika mechi za mchujo za kufuzu kwa kombe la dunia la Fifa 2026 miongoni mwa mataifa ya Afrika kwenye dirisha hili la kimataifa.
Baada ya kukosa nafasi tisa za kufuzu za moja kwa moja za bara hili, Cameroon, DR Congo, Gabon na Nigeria zitasafiri hadi Morocco kwa mechi za mtoano ambapo mshindi atafuzu moja kwa moja.
Lakini, kulingana na orodha yao ya dunia, taifa litakaloibuka mshindi , litakabiliwa na mechi moja au zaidi ili kufuzu katika mchuano wa mwaka ujao nchini Canada, Mexico na Marekani.
BBC Sport Africa inaelezea jinsi hatua hii inavyofanya kazi - na nini kinafuata.
Je, timu hizi zilifikaje katika hatua ya mtoano?
Wanne hao walifikia hatua hii kama wahitimu wanne bora waliomaliza nafasi ya pili katika makundi tisa ya Afrika ya kufuzu kwa Kombe la Dunia.
Matokeo dhidi ya timu iliyo nafasi ya sita katika makundi nane yalipunguzwa kwa sababu Eritrea ilijiondoa usiku wa kuamkia mchuano huo, na kuacha Kundi E na timu tano pekee.
Gabon walikuwa na rekodi bora zaidi, ikifuatiwa na DR Congo na kisha Cameroon.
Nigeria waliingia kinyemela tu hadi mechi ya mchujo kwa tofauti ya mabao, huku Frank Onyeka akifunga bao moja dakika ya 91 katika ushindi wao wa 4-0 dhidi ya Benin na kuiondoa Burkina Faso kwa bao moja.
Je, droo ya hatua ya mtoano ya Afrika iliamuliwa vipi?
Orodha ya kimataifa Fifa ilitumika kupanga mechi za nusu fainali, huku timu iliyoorodheshwa juu zaidi ikikabiliana na iliyo chini zaidi.
Kwa matokeo hayo, Nigeria (ya 41 duniani) itacheza na Gabon (ya 77) siku ya Alhamisi (16:00 GMT) kabla ya Cameroon (ya 54) kumenyana na DR Congo (ya 60) baadaye siku hiyo hiyo (19:00 GMT).
Washindi wa nusu fainali watamenyana Jumapili (19:00 GMT) ili kupata nafasi ya kuendeleza ndoto zao za kufuzu katika Kombe la Dunia mwaka ujao.
Mechi zote tatu zitafanyika katika mji mkuu wa Morocco Rabat.
Kipi kitafuatia kwa washindi?
Washindi wa mchujo barani Afrika watafuzu kwa mchuano wa mabara wa timu sita , ambapo unaratibiwa kuanzia 23-31 Machi 2026 na utaamua timu mbili za mwisho kwenye Kombe la Dunia mwaka ujao.
Mataifa mawili kutoka eneo la Concacaf (Kaskazini, Amerika ya Kati na Carribea) na upande mmoja kutoka kila moja ya mashirikisho ya Asia, Oceania na Amerika Kusini pia yatahusika.
Mataifa sita yatagawanywa katika makundi mawili.
Pande mbili zilizo katika nafasi ya juu zaidi zitatolewa na kutinga fainali moja kwa moja katika kila kundi, huku washindani wanne walio katika nafasi ya chini zaidi wakikutana katika nusu fainali.
Umoja wa Falme za Kiarabu na Iraq zitamenyana na Asia, wakati Bolivia, inayowakilisha Amerika Kusini, na New Caledonia, inayowakilisha Oceania, tayari wakiwa wamejikatia nafasi zao kushiriki.
Ikizingatiwa Bolivia na New Caledonia mtawalia zimeorodheshwa za 76 na 150 katika orodha ya fifa duniani kwa sasa, hiyo inaongeza nafasi ya mwakilishi wa Afrika kutinga moja kwa moja hadi fainali.
Droo ya mechi za mchujo, zitakazochezwa kwa mkondo mmoja wa mtoano, kukiwa na muda wa ziada na mikwaju ya penalti ikihitajika, itafanyika Alhamisi, 20 Novemba.
Je, ni timu gani ilio na fursa ya kushinda mechi za mchujo za Afrika?
Hili ni swali kubwa
Nigeria ndio inayojivunia timu yenye nguvu zaidi kulingana na viwango vya ubora duniani lakini ilipitia kampeni mbaya zaidi ya kufuzu kati ya timu hizo nne za Afrika.
Super Eagles walikuwa na wasimamizi watatu tofauti waliosimamia mechi zao za Kundi C na walitatizika Victor Osimhen alipokosekana kutokana na jeraha, na kuambulia pointi nne tu kati ya 15 zinazowezekana bila mshambuliaji wao mahiri.
Hata hivyo Wenyeji hao wa Afrika Magharibi hawajafungwa katika mechi sita za mashindano hayo chini ya Eric Chelle huku wakijinadi kuepuka kukosa kufuzu kwa Kombe la Dunia mfululizo.
Cameroon ni timu nyengine kubwa ya Afrika ambayo haikufanya vyema , wakimaliza alama nne nyuma ya Cape Verde katika Kundi D.
Indomitable Lions ilishinda mchezo mmoja tu kati ya mitano ya ugenini, ambayo haileti alama sifa nzuri kwa kucheza kwenye ardhi isiyoegemea upande wowote mwezi huu.
Cameroon wanashikilia rekodi ya Afrika ya kucheza mechi nyingi zaidi za Kombe la Dunia, lakini watahitaji kuboresha kiwango chao ili kuendeleza safari yao ya kufuzu katika michuano ya tisa ya kimataifa .
DR Congo, ambayo mechi yake pekee ya awali ya Kombe la Dunia ilishiriki kama Zaire mwaka 1974, ilimaliza kwa pointi mbili nyuma ya Senegal katika Kundi B.
Chui hao walilipia gharama kwa kuruhusu ushindi wa 2-0 dhidi ya Wasenegali hao kuponyoka kwenye ardhi ya nyumbani mnamo Septemba, na hatimaye kupoteza 3-2.
Yoane Wissa wa Newcastle bado hayupo kutokana na jeraha, lakini fowadi mwenzake Cedric Bakambu amekuwa katika hali nzuri katika kufuzu akiwa amefunga mabao manne.
Gabon, ambao wanawania kufuzu Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza, walimaliza wakiwa nyuma kwa pointi moja na Ivory Coast katika Kundi F.
The Panthers wanajivunia washambuliaji wakali Denis Bouanga na Pierre-Emerick Aubameyang, ambao walifunga mabao manane na saba mtawalia katika hatua ya makundi.
Mabao mengi ya Aubameyang yalipatikana alipopachika wavu mara nne dhidi ya Gambia mwezi uliopita kabla ya kutolewa nje kwa kadi nyekundu, ingawa sasa amerejea kutoka kwa adhabu yake.
Je, watakutana na nani kwenye Kombe la Dunia?
Droo ya Kombe la Dunia 2026 itafanyika Ijumaa, Disemba 5, wakati timu 48 zitagawanywa katika vikundi 12 vya timu nne kila moja.
Timu arobaini na mbili kati ya hizo zitaamuliwa wakati wa droo.
Ni washindi wawili tu wa mchujo wa mabara na washindi wanne wa mchujo wa Uropa ndio watakaosalia kujulikana.
Kutokana na hali hiyo, timu ya Afrika itakayoshiriki katika mchujo wa kuwania kufuzu kwa mabara mwaka ujao huenda ikajua timu zote ambazo huenda ikakutana nazo katika kundi lao la Kombe la Dunia - iwapo itafanikiwa.