Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Kocha wa zamani wa mpira wa miguu na mwalimu - sasa ndiye mgombea mwenza wa Harris
Akitoa kauli ya mstari mmoja ulionea kwenye runinga - "hawa jamaa ni wa ajabu tu" - Tim Walz alijitosa kuwania nafasi ya mgombea mwenza wa Kamala Harris.
Kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 60 anakuja na mbinu ya kipekee, ya kusema wazi na yenye lugha kali kwa upinzani wa Republican.
Pia anakuja na wasifu kazi wa kuvutia- mwalimu wa shule ya umma, kocha wa mpira wa miguu na Mlinzi wa Kitaifa kabla ya kuingia kwenye siasa.
Uzoefu wake wa kisiasa, akiwakilisha wilaya inayoegemea chama cha Republican katika Bunge la Congress na kisha kupitisha sera za mrengo wa kushoto kama gavana wa Minnesota, inaweza kuwa na mvuto mpana wakati siasa za Marekani zikiwa na mgawanyiko mkubwa.
Mzaliwa wa kijijini Nebraska, Bw Walz alilima na kuwinda wakati wa kiangazi na alijiunga na Jeshi la Walinzi wa Kitaifa akiwa na umri wa miaka 17. Alihudumu katika kikosi cha kujitolea kwa miaka 24.
Babake, msimamizi wa shule ya umma, alimhimiza kujiunga na jeshi kabla ya kufariki kutokana na saratani ya mapafu wakati Bw Walz alipokuwa na umri wa miaka 19.
Gavana wa Minnesota amezungumza kuhusu jinsi mafao ya walionusurika katika Usalama wa Jamii yalivyomdumisha mama yake, na jinsi Mswada wa GI ulivyolipa elimu yake ya chuo kikuu.
Akiwa na shahada ya ualimu, Bw Walz alichukua kazi ya kufundisha wa mwaka mmoja nchini China wakati wa mauaji ya Tiananmen Square.
Baadaye alikwenda fungate nchini humo na mke wake Gwen Whipple na pia alipanga safari za kipindi cha kiangazi za elimu nchini China kwa wanafunzi wa Marekani.
Baada ya kurejea nyumbani Nebraska, Bw Walz alikuwa mwalimu na mkufunzi wa kandanda wa Marekani hadi mkewe - mwalimu mwingine katika shule hiyo - akamvuta na kumrudisha Minnesota alikozaliwa. Sasa wana watoto wawili.
Akiwa mkufunzi katika Shule ya Upili ya Mankato West, Bw Walz alisaidia kuunda programu ya kandanda ya Marekani ambayo iliongoza shule hiyo kwenye michuano yake ya kwanza ya jimbo.
Pia alipata pongezi kwa kukubali kuwa mshauri wa kitivo cha muungano wa wapenzi wa jinsia moja katika shule hiyo wakati ambapo mapenzi ya jinsia moja yalikuwa hayakubaliki.
Aligombea wadhifa huo kwa mara ya kwanza katika wilaya ya kilimo ambayo inaenea kusini mwa Minnesota, ambayo ni ya vijijini na inayoegemea Republican.
Lakini Bw Walz alifanya kampeni kama mtu mwenye msimamo wa wastani ambaye alijali utumishi wa umma na utetezi wa maveterani, na hivyo kusababisha mvurugo wa uchaguzi uliompa ushindi.
Kwa miaka yake 12 katika Congress, ilikuwa viguju kujua falsafa yake ya kisiasa
Alipiga kura kuunga mkono Sheria ya Huduma ya bei nafuu, alifadhili hatua za kusaidia wafanyakazi, ikiwa ni pamoja na mswada wa kuongeza kiasi cha chini cha mshahara na aliunga mkono juhudi zisizofanikiwa za kupunguza uzalishaji wa kaboni.
Lakini pia alijipata akiungana na wanachama wa Republican na kukubaliana nao katika baadhi ya mambo.
Alipiga kura kuendelea kufadhili vita vya Iraq na Afghanistan, aliunga mkono uchunguzi mkali zaidi wa wakimbizi wanaoingia Marekani, na kujaribu kuzuia uokoaji wa benki na makampuni ya magari katika zama za Obama baada ya msukosuko wa kifedha wa mwaka wa 2008.
Mara baada ya kuidhinishwa na Chama cha Kitaifa cha Wamiliki wa Bunduki (NRA), ambacho kilichangia kampeni yake, alizungumza na kuunga mkono marufuku ya silaha za kushambulia baada ya kufyatuliwa risasi kwa shule ya Parkland na kupoteza uungwaji mkono wao.
Bw Walz alishinda kinyang'anyiro cha ugavana wa Minnesota 2018 kwa zaidi ya pointi 11 lakini muhula wake wa kwanza uligubikwa na janga la Covid na mauaji ya George Floyd na afisa wa polisi huko Minneapolis.
Wanachama wa Republican walimkosoa vikali Bw Walz kwa kujikokota kupeleka Walinzi wa Kitaifa licha ya baadhi ya maandamano kuwa ya vurugu.
Lakini gavana huyo alishinda uchaguzi tena na muhula wake wa pili umesimamia kipindi chenye shughuli nyingi huku Democrats wakidhibiti bunge la jimbo hilo kwa kiti kimoja.
Wanachama wa Democrat wameweka haki za uavyaji mimba, wamepitisha likizo ya kulipwa ya familia na wagonjwa, wameimarisha sheria za bunduki, wamefadhili milo ya shule kwa wote bila malipo na kuwekeza katika nyumba za bei nafuu.
Shughuli hiyo ya kusisimua ilivutia macho ya Rais wa zamani Barack Obama ambaye aliandika: "Ikiwa unahitaji kukumbushwa kuwa uchaguzi una matokeo, angalia kinachoendelea Minnesota."
Akiwa hajulikani sana katika ulingo wa kitaifa, Bw Walz amewavutia wengi katika wiki za hivi karibuni kwa maelezo yake yenye ukali kuhusu wagombeaji wa Republican.
"Hawa ni watu wa ajabu kwa upande mwingine," hivi majuzi aliiambia MSNBC, kauli ambayo imerudiwa sana. "Wanataka kupiga marufuku vitabu. Wanataka kuwa katika chumba chako cha vipimo (na daktari)"
Lakini Warepublican wamekuwa wepesi kuashiria kile alichokifanya huko Minnesota kama kibaya sana kwa Wamarekani wa kawaida.
Tom Emmer, mgombea wa tatu wa cheo cha juu wa Republican katika Baraza la Wawakilishi la Marekani, alimshutumu Bw Walz kwa kujaribu "kugeuza Minnesota kuwa jimbo la California la Kamala Harris".
Lakini washirika, wakiwemo viongozi wa wafanyikazi, wanaamini kuwa Bw Walz anawezakuzidisha mvuto wa Bi Harris kwa wapiga kura wa maeneo ya mashambani na wa tabaka la wafanyakazi.
Angie Craig, mbunge wa chama cha Democrat aliyejitosa katika kinyang'anyiro cha kuchaguliwa tena, alimsifu Bw Walz kama "kiongozi aliyejaribiwa vitani".
Kama "mshindi aliyethibitishwa ambaye hajawahi kushindwa katika uchaguzi katika mapambano mengi magumu", aliiambia BBC kuwa anaamini atakuwa chaguo bora zaidi kwa tiketi ya Harris.
Imetafsiriwa na Yusuf Jumah