Alikumbatia mauti: Jinsi Mfalme wa Saudi alivyouawa na mpwa wake miaka 50 iliyopita

Chanzo cha picha, C Maher/Daily Express/Hulton Archive/Getty Images
Mnamo Machi 25, 1975, Mfalme Faisal wa Saudi Arabia aliuawa huko mji mkuu wa Riyadh. Alipigwa risasi na mpwa wake.
Waziri wake wa mafuta, Ahmed Zaki Yamani, alikuwa amesimama karibu na mfalme wakati risasi zilipofyatuliwa.
Mnamo 2017, binti yake, Dk. Mai Yamani, alizungumza na BBC.
Sitasahau siku hiyo. Nilivumilia maumivu, nayakumbuka hadi leo, uchungu wa baba yangu. Hebu fikiria binadamu amesimama karibu na mshauri wake, bwana wake, rafiki yake, alimshambulia kwa risasi kutoka umbali mfupi.
Mfalme Faisal alipigwa risasi tatu mfululizo huku akiinama kumkumbatia mpwa wake kwa salamu.
Baba yake Dk Yamani, waziri mwaminifu kwa mfalme Faisal kwa miaka 15, alikuwa akimjulisha mfalme, ndiyo maana alikuwa pembeni mwake.
Mfalme Faisal, mtawala wa tatu wa ufalme huu wa jangwa wenye utajiri wa mafuta na mtoto wa tatu wa baba yake mwanzilishi, alikimbizwa hospitalini, lakini alikufa muda mfupi baadaye.

Chanzo cha picha, Claude Salhani/Sygma/Getty Images
Siku hiyo, kilomita chache kutoka upande mwingine wa mji, Mai Yamani mwenye umri wa miaka 18 alikuwa akimsubiri baba yake.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
"Nilikuwa nimeketi katika nyumba ya baba yangu, nimezungukwa na vitabu vyake. Aliingia, akionekana hayuko katika hali yake ya kawaida na mwenye uchungu. Alikwenda moja kwa moja kwenye chumba cha kulia na akaanza kulia na kutamka neno moja tu: 'msiba'."
Huyu hakuwa kama yeye, mtu anayejulikana kwa utulivu na busara. Kisha akamwambia binti yake kilichotokea. "Saa 10 alfajiri, ujumbe wa mafuta wa Kuwait ulikuwa ukienda ikulu kuonana na Mfalme Faisal. Baba yangu, Waziri wa Mafuta, alikwenda huko kumjulisha mfalme," anasimulia.
Mwana wa mfalme huyo, alikuwa na jina kama lile la, Faisal [Ibu Musaed], mpwa wa mfalme, alijiunga na ujumbe wa waziri wa mafuta wa Kuwait. Kisha Faisal alifungua mikono yake kumkumbatia mpwa wake.
Mpwa akatoa bastola ndogo mfukoni na kumpiga mfalme risasi tatu kichwani, huku baba akiwa amesimama karibu yake sana.
Kulingana na baadhi ya ripoti za wakati huo, mshambuliaji huyo aliripotiwa kuwaambia polisi kwamba Yamani alikuwa amesimama karibu naye hivi kwamba alidhani kuwa amemuua pia.
Kisha Yamani akaenda hospitali na mfalme Faisal, ambapo kifo cha mfalme kilithibitishwa.
"Baada ya hapo, kimya kilirejea. Mitaa ya Riyadh ilikuwa tupu na kimya kilitawala."
Mfalme wa mageuzi
Faisal alikuwa mfalme wa Saudi Arabia mwaka wa 1964, akitawala "jangwa lenye ukubwa wa Ulaya Magharibi" na alisifiwa kama "rafiki mpya wa Kiarabu" wa Uingereza, dhamira yake ikiwa ni "kufanya kuwa ya kisasa moja ya nchi zilizo nyuma sana katika Mashariki ya Kati", kama David Dimbleby wa BBC alikuwa ametangaza wakati huo - lakini angeweza kufanikisha suala hilo bila kupoteza kiti chake cha enzi?
Faisal, mmoja wa watoto wakubwa wa Abdulaziz Al Saud, alipigana katika kampeni ya baba yake ya kuunganisha Peninsula ya Arabia, ambayo ilisababisha kuanzishwa kwa ufalme ulioitwa kwa jina lao, Saudi Arabia, miaka thelathini iliyopita. Faisal baadaye alihudumu kama Waziri Mkuu chini ya kaka yake mkubwa, ambaye alikua mfalme baada ya kifo cha baba yao.
Baada ya kutawazwa kwake kwenye kiti cha enzi, Faisal alikuwa na sifa ya kuwa mwanasiasa mwerevu, mcha Mungu, mchapakazi, na mwanamageuzi, aliyezoea kufanya mazungumzo na miji mikuu ya kigeni.
Pia alionekana kama kiongozi anayetaka kutumia utajiri mpya wa mafuta wa nchi hiyo kuipatia Saudi Arabia hali ya kisasa na elimu bora, huduma za afya na mfumo wa mahakama.
Lakini mageuzi ya Mfalme Faisal hayakufurahisha kila mara sehemu ya kihafidhina ya shule ya Uislamu, ambayo familia yake ilishirikiana nayo.
Faisal alipofungua chaneli ya kwanza ya televisheni ya Saudi Arabia katikati ya miaka ya 1960, jengo hilo lilishambuliwa kwa mtutu wa bunduki, likiongozwa na kaka wa mtu ambaye angemuua.
Mfalme Faisal pia alianzisha elimu ya wasichana.
Dakt. Yamani anasema hivi: "Malkia Iffat [mkewe wa pili] alianzisha elimu ya wasichana nchini Saudi Arabia. Ninajivunia kusema kwamba nilikuwa mmoja wa wanafunzi tisa wa kwanza katika shule yake, na Mfalme Faisal aliwasadikisha wakuu wa kidini kwamba kuelimisha wanawake kuliwafanya wawe akina mama bora zaidi. Shule hiyo iliitwa Dar Al Hanan, Shule ya Huruma."

Chanzo cha picha, Bettmann Archive/Getty Images
Yamani alianza kufanya kazi kwa Mfalme Faisal mwaka wa 1960. Hili halikuwa la kawaida, kwani alikuwa mtu wa kawaida, mwenye elimu ya juu na mwanasheria, lakini si mwanachama wa familia ya kifalme ya Saudi. Mfalme Faisal alisoma baadhi ya makala zake na zilimvutia.
"Baba yangu alifungua kampuni yake ya kwanza ya uwakili, kisha akaandika makala za uchochezi, zinazotetea demokrasia na utawala bora. Zilitiwa saini na Abu Mai fulani, baba wa binti anayeitwa Mai, kwa sababu mimi ndiye niliyekuwa mkubwa wake. Kwa hiyo Faisal, wakati huo mwanamfalme, alisema: "Mtu huyu ni nani?" Alikuwa akitafuta mshauri wa kisheria.
Baadaye Mfalme Faisal alimteua Ahmed Zaki, au Sheikh Yamani kama alivyopewa jina la utani, kuwa Waziri wa Petroli.
Kwa pamoja, mfalme na mtumishi wake walitengeneza sera ambayo, kwa mara ya kwanza, iliipa Saudi Arabia udhibiti kamili wa rasilimali yake kubwa ya mafuta na kuifanya kuwa nguvu kuu katika ulimwengu wa Kiarabu na katika uwanja wa kimataifa.
Kuhama kwa nguvu
Mnamo 1973, baada ya vita kati ya Israeli na majirani zake wa Kiarabu, Wasaudi, ambao sasa ndio wazalishaji wakubwa wa mafuta duniani, waliongoza kampeni ya kutumia mafuta kwa mara ya kwanza kama silaha ya kisiasa.
Ugavi wa mafuta kwa nchi zinazounga mkono Israel umepunguzwa, na kusababisha kupanda kwa bei duniani. Sheikh Yamani alitumwa kufikisha ujumbe huo.
"Tunachotaka ni kuondolewa kabisa kwa majeshi ya Israel kutoka katika maeneo ya Waarabu yanayokaliwa kwa mabavu. Na kisha, mafuta yatafikia kiwango sawa na Septemba 1973."
Alikubali kwamba ongezeko kubwa la bei ya mafuta litabadilisha usawa wa nguvu za kimataifa kati ya nchi zinazoendelea na nchi zilizoendelea kiviwanda.
Mabadiliko haya katika usawa wa mamlaka yalitambuliwa wakati, 1974 (mwaka kabla ya kuuawa kwake), Mfalme Faisal alitajwa kuwa Mtu bora wa Mwaka na jarida la Time.
Dakt. Yamani anasema: "Hatujui sababu ya kweli ya kuuawa kwa mfalme, isipokuwa kwamba muuaji alikuwa mtu aliyekuwa na tatizo la kiakili. Wakati huo, nilikuwa na umri wa miaka 18 na nilihisi uchungu wa baba yangu. Bado ninakumbuka."
Sheikh Yamani alisalia kuwa waziri wa mafuta wa Saudi Arabia kwa miaka kumi na moja, hadi 1986.
Dk Yamani aliendelea kusoma katika chuo kikuu cha Marekani na akawa mwanamke wa kwanza wa Saudi kupata udaktari kutoka Oxford.
Ameandika vitabu vingi kuhusu utambulisho wa Waarabu na pia amekuwa mshauri wa benki kama vile Goldman Sachs na kampuni za mafuta kama vile Shell.















