Simulizi ya "Jamhuri ya Kuwait" iliodumu siku nne tu

.
Maelezo ya picha, Saddam Hussein akiwa na Alaa Hussein Ali, ambaye aliongoza serikali ya mpito ya Kuwait na kutangaza kuanzishwa kwa "Jamhuri ya Kuwait.
Muda wa kusoma: Dakika 8

Mnamo Agosti 2, 1990, vikosi vya Iraq vilishambulia Kuwait katika operesheni ya kushtukiza, iliyoamriwa na Rais wa wakati huo Saddam Hussein, kuashiria mwanzo wa moja ya machafuko hatari katika eneo la Ghuba ya Uajemi na kuandaa njia kwa Vita vya Pili vya Ghuba ya Uajemi.

Mgogoro kati ya Iraq na Kuwait ulianza kutokana na mchanganyiko wa mambo ya kisiasa na kiuchumi.

Baada ya kumalizika kwa Vita vya Iran na Iraq mwaka 1988, Iraq ilijikuta katika madeni makubwa hasa kutoka mataifa ya Ghuba yaliyokuwa yakiisaidia Baghdad kifedha wakati wa vita hivyo hasa Kuwait na Saudi Arabia. Kuwait ilidai kulipwa kwa madeni haya.

Mgogoro huo ulizidishwa na shutuma za Iraq dhidi ya Kuwait, ambayo iliishutumu Kuwait kwa kuzalisha zaidi ya mgawo wake katika Shirika la Nchi Zinazouza Mafuta kwa wingi (OPEC), hali ambayo ilisababisha kushuka kwa bei ya mafuta na, hivyo, kupungua kwa mapato ya Iraq.

Iraq pia iliishutumu Kuwait kwa kuiba mafuta kutoka kwa kisima cha mafuta cha pamoja cha Rumaila.

Katika hali hii ya wasiwasi, Saddam Hussein aliamua kuivamia Kuwait, na Agosti 2, 1990, baada ya kuchukua udhibiti wa nchi, Ali Hassan al-Majid (binamu wa Saddam) aliteuliwa kuwa gavana wa kijeshi wa Kuwait.

Pia unaweza kusoma

Serikali ya muda

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Saddam Hussein aliamuru uvamizi wa Kuwait mnamo Agosti 1990

Wakati huo, mamlaka za Iraq zilianza haraka kuchukua hatua ili kuchukua ''uhalali rasmi'' wa taifa Moja ya hatua hizi ilikuwa kuanzishwa kwa taasisi inayoitwa "Jamhuri ya Kuwait," chombo kipya cha kisiasa kwenye magofu ya nchi huru ya Kuwait.

Siku mbili baada ya kuchukua udhibiti wa Kuwait, haswa mnamo Agosti 4, 1990, Saddam Hussein alitangaza kuanzishwa kwa "Jamhuri ya Kuwait." Kulingana na kitabu cha Raja Hassan Manawi "Kuwait: Occupation and Liberation," Saddam alisema kwamba jamhuri mpya itakuwa chombo huru kinachotawaliwa na "mapinduzi maarufu."

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Kulingana na wachambuzi na wanahistoria, tamko hili lilikuwa sehemu ya mkakati wa Saddam Hussein wa kuchukua muda ili kujificha kisiasa.

Badala ya kuinyakuwa nchi hyo kuanzia siku ya kwanza , Iraq ilijaribu kuonyesha hali hiyo kama "mapinduzi ya ndani" yaliyofanywa na "raia wenyewe" dhidi ya "serikali inayotegemea ukoloni na ubeberu."

Vyombo vya habari vya Iraq wakati huo vilitumia maelezo haya kuhalalisha shambulio dhidi ya maoni ya Waarabu na ya kimataifa.

Hatua ya kuanzia ilikuwa uteuzi wa "Serikali ya Muda ya Kuwait Huru", ambayo ilikuwa na maafisa tisa wa zamani wa Kuwait ambao walishirikiana na Iraq au baadaye walituhumiwa kushirikiana nayo.

Kanali Alaa Hussein Ali Khafaji Al-Jaber aliteuliwa kuwa Waziri Mkuu na Amiri Jeshi Mkuu, kwa wakati mmoja akishika nyadhifa za Waziri wa Ulinzi na Waziri wa Mambo ya Ndani.

Luteni Kanali Walid Saud Mohammed Abdullah aliteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Nje, Luteni Kanali Fuad Hussein Ahmed aliteuliwa kuwa Waziri wa Fedha na Mafuta, Meja Fadel Haider Al-Wufqi aliteuliwa kuwa Waziri wa Habari na Uchukuzi, na Luteni Kanali Hussein Zahiman Al-Shammari aliteuliwa kuwa Waziri wa Masuala ya Kijamii.

Kitabu cha "Kuwait kilichoandika simulizi ya Occupation and Liberation" kinasema kuwa Alaa Hussein alizaliwa Kuwait mwaka 1948 na kujiunga na chama cha Iraq Baath Party alipokuwa akisoma katika Chuo Kikuu cha Baghdad. Alikuwa afisa wa zamani katika jeshi la Kuwait.

Televisheni ya taifa ya Kuwait, iliyokuwa chini ya udhibiti wa majeshi ya Iraq, ilitangaza taarifa ya video ya Alaa Hussein akitangaza kuundwa kwa serikali mpya na kuwataka wananchi wa Kuwait kushirikiana na uongozi mpya.

Serikali mpya ilitangaza mfululizo wa maamuzi ya "mapinduzi", ikiwa ni pamoja na kutaifishwa kwa makampuni ya Magharibi, kunyakua mali ya familia inayotawala, kuvunjwa kwa Bunge la Kitaifa la Kuwait, mabadiliko ya Kuwait kuwa jamhuri, na kutoa uraia kwa raia wote wa Kiarabu waliokuwa wakiishi Kuwait wakati huo.

'Serikali ya siku nne'

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Baada ya uvamizi wa kijeshi wa Kuwait, Saddam Hussein alimteua Ali Hassan al-Majid kama gavana wa kijeshi

Serikali hii haikuwa na nguvu za kweli. Wengine waliamini kuwa Iraq ilitumia muundo huu kuhalalisha kuinyakua Kuwait kwa maoni ya umma ya ndani na ya kimataifa. Watu wa Kuwait waliikataa serikali hii na upinzani wa Kuwait ulikataa kushirikiana nayo.

Kwa upande wa muda, serikali hii ilidumu kwa siku nne tu, kwani Saddam Hussein aliamua kuiunganisha rasmi Kuwait na Iraq mnamo Agosti 8, 1990. Alitangaza kwamba serikali ya mpito ya Kuwait iliomba hili kutoka kwake, na hivyo kufanya kuwepo kwake kisheria na kivitendo kutokuwa na maana.

Mnamo Agosti 28, 1990, amri ilitolewa kuanzisha "Mkoa wa Kuwait" kama mkoa wa kumi na tisa wa Iraq. Mkoa huo ulikuwa na wilaya tatu: Kazema (mji mkuu wa Kuwait), Jahra, na Al-Nidaa (Ahmadi).

Aziz Saleh Al-Nu'man, raia wa Iraq, aliteuliwa kuwa gavana wa Kuwait, akimrithi Ali Hassan Al-Majid.

Baada ya kuvunjwa kwa serikali ya mpito, Saddam Hussein alitoa agizo la kumteua Alaa Hussein Ali kuwa Naibu Waziri Mkuu wa Iraq na kuwateua mawaziri wengine kuwa washauri wa rais wenye vyeo vya uwaziri.

Kwa hivyo Kuwait ilitwaliwa kama jimbo la Iraq, na jeshi la Iraq lilianza kutekeleza sheria za Iraq kote nchini, ikiwa ni pamoja na kubadilisha mitaala, kuchukua nafasi ya sarafu, na kupiga marufuku uchapishaji wa magazeti ya Kuwait.

Balozi za kigeni nchini Kuwait zilifungwa, wanadiplomasia wengi walifukuzwa, vizuizi vikali viliwekwa kwa wakazi wa eneo hilo, na mateso, kuwekwa kizuizini, na kuuawa vilitumiwa kama zana za vitisho.

Uwepo wa kijeshi ulitawala maisha ya kila siku nchini, na Saddam Hussein alitangaza kwamba "Kuwait imerejea Iraq."

Wanahistoria wengi na wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanaamini kwamba tangazo la kuundwa kwa "Jamhuri ya Kuwait" halikuwa chochote zaidi ya "onyesho la kisiasa na njia ya Iraq ya kuchukua muda."

Uongozi wa Iraq ulikuwa unafahamu kwamba kutangaza ujio wa moja kwa moja wa Kuwait kuanzia siku ya kwanza kungeudhi jumuiya ya kimataifa, hivyo ulipendelea kueleza haya kama "mapinduzi maarufu ya ndani" na kisha "ombi la kujiunga na Iraq."

Vita na Ukombozi

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Vikosi vya Marekani na Saudia vinaelekea katika Jiji la Kuwait ili kuikomboa Februari 1991

Umoja wa Mataifa ulilaani shambulizi hilo na kuiwekea Iraq vikwazo mnamo Agosti 6 mwaka huo. Kisha, mnamo Novemba 29, Baraza la Usalama lilipitisha Azimio namba 678, lililoidhinisha matumizi ya nguvu dhidi ya Iraq na kuweka makataa ya saa sita usiku Januari 15, 1991, kujiondoa.

Kuanzia mapema Januari 1991, juhudi kubwa za kidiplomasia zilianza kumaliza mzozo bila kutumia nguvu. Kadiri siku zilivyopita, hali ya kutoweza kuepukika ya vita ilizidi kuwa na nguvu.

Juhudi za Waarabu kutatua mgogoro huo zilishindwa vibaya. Javier Perez de Cuellar, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wakati huo, alikutana na Rais wa Iraq Saddam Hussein lakini hakuweza kumshawishi arudi nyuma au hata kuanza mazungumzo ya kujiondoa.

Tarehe 9 Januari 1991, mazungumzo kati ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani James Baker na mwenzake wa Iraq Tariq Aziz pia yalimalizika bila matokeo.

Washington kisha ilitangaza kwamba ilikuwa imetumia njia zote za kidiplomasia kufikia suluhu, na Januari 12, Bunge la Congress la Marekani lilipiga kura ya kuunga mkono azimio la kuanzisha vita dhidi ya Iraq.

Udhibiti wa Iraq dhidi ya Kuwait uliendelea kwa miezi kadhaa, hadi Marekani, ikiongoza muungano wa kimataifa wa nchi 34, ilipoamua kuanzisha operesheni ya kijeshi ya kuikomboa Kuwait. Operesheni hiyo ilianza Januari 16, 1991, iliyopewa jina la "Dhoruba ya Jangwa.

Mnamo Februari mwaka huo, Kuwait ilikombolewa kikamilifu na vikosi vya Iraq vilirudi nyuma chini ya shinikizo kubwa la kijeshi, wakati jeshi la Iraq liliacha uharibifu mkubwa, ikiwa ni pamoja na kuchoma moto visima vya mafuta na kuharibu miundombinu.

Mnamo Machi 14, 1991, Amiri wa Kuwait, Sheikh Jaber Al-Ahmad Al-Sabah, alirejea nchini baada ya miezi kadhaa ya serikali yake kufanya kazi kwa muda kutoka Saudi Arabia.

Baada ya kukombolewa kwa Kuwait, wanachama wa serikali ya mpito inayounga mkono Iraq—isipokuwa Alaa Hussein—walirejea nchini Aprili 27, 1991, na mara moja wakajisalimisha kwa mamlaka ya Kuwait.

Walipelekwa kwa Idara ya Uchunguzi wa Usalama wa Serikali, ambayo ilimaliza uchunguzi wake Mei 15, 1991, na kisha kukabidhiwa kwa Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa Usalama wa Serikali mnamo Julai 22.

Wakati wa uchunguzi, walitangaza uaminifu wao kwa Kuwait na amir wake na kutoa ushahidi dhidi ya Alaa Hussein.

Mnamo Septemba 9, 1991, Ghazi Obaid al-Sammar, Waziri wa Sheria wa Kuwait wakati huo, alitangaza kwamba kesi dhidi ya serikali ya mpito ilikuwa imefungwa, akiongeza kwamba uchunguzi ulihitimisha kwamba wanachama wake "hawakuwa na nia na walikuwa wakipigwa, vitisho, na kuteswa kimwili na kisaikolojia."

Uchunguzi huo ulitokana na ripoti za kijasusi za kijeshi na uchunguzi wa usalama wa taifa.

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Serikali halali ya Kuwait ilirejea baada ya ukombozi mnamo Machi 14, 1991

Alaa Hussein Ali, aliyeongoza serikali hiyo, aliondoka Iraq na kuelekea Uturuki na kisha Norway mwaka 1998, na mwaka 2000, alirejea Kuwait na kujisalimisha ili kujiondoa katika mashtaka ya kushirikiana na Iraq.

Alihukumiwa kifo kwa uhaini mkubwa, lakini hukumu yake ilipunguzwa hadi kifungo cha maisha.

Alaa Hussein Ali aliwaambia majaji kwamba alilazimishwa kukubali urais wa "nchi bandia" baada ya vikosi vya Iraq kutishia kukamata na kuua familia yake.

"Sijui ni kwa nini Wairaq walinichagua kutoka miongoni mwa mamia ya wafungwa wa vita ili kuongoza nchi ya vibaraka nchini Kuwait," aliongeza, akibainisha kuwa vikosi vya Iraq vilimlazimisha kusalia Iraq hadi 1998.

Kuwait ilibatilisha uraia wa Alaa Hussein Septemba iliyopita.

Kisheria, "Jamhuri ya Kuwait" haikuwa na kigezo chochote cha kisheria cha serikali, kwani haikuwa na mamlaka yoyote na, kwa mtazamo wa kisheria, uwepo wake haukuwa na maana yoyote.

Isitoshe, kasi ya uundwaji wake na kuvunjwa kwake inadokeza kwamba kilikuwa chombo cha muda tu cha kuhalalisha uchokozi na si chombo halisi cha kisiasa.

"Serikali Huru ya Muda ya Kuwait" haikutoa sheria yoyote, haikuwa na kazi za kiutawala au kidiplomasia, na haikuanzisha uhusiano wowote na jumuiya ya kimataifa.

Licha ya maisha mafupi ya serikali hii, athari zake za kisaikolojia na kisiasa zimebakia akilini mwa Kuwait. Kwa Kuwait, matukio ya enzi hizo ni kumbukumbu chungu iliyoimarisha mshikamano wao wa kitaifa na kuwakumbusha kwa mara nyingine tena umuhimu wa mamlaka na uhuru.

Pia unaweza kusoma

Imetafsiriwa na Seif Abdalla