Kwa nini haufui taulo lako mara nyingi vya kutosha na kuna athari gani?

Chanzo cha picha, Getty Images
Mataulo tunayojifutia hutumika mara nyingi na kubeba vijidudu vingi wakati huo. Lakini unapaswa kutumia kwa muda gani kabla ya kuyafua?
Pengine umeusugua mwili wako na taulo moja leo tayari.
Lakini kile kitambaa ulichojikausha nacho kilikuwa kisafi kiasi gani?
Wengi wetu huliweka taulo kwenye mashine na kulifua mara moja kwa wiki, wakati utafiti mmoja wa watu 100 uligundua karibu theluthi moja walifanya hivyo mara moja kwa mwezi.
Wachache, kulingana na uchunguzi mmoja nchini Uingereza, wanakubali kufanya hivyo mara moja tu kwa mwaka.
Na ingawa nyuzi hizo laini zinaweza zisionyeshe dalili zozote za uchafu, ni mazalia ya mamilioni ya vijidudu.
Uchunguzi umeonesha kuwa taulo zinaweza kuchafuliwa haraka na bakteria wanaopatikana kwenye ngozi ya binadamu, lakini pia na zile zinazopatikana kwenye matumbo yetu.
Hata baada ya kuoga, miili yetu bado imefunikwa na vijidudu na labda haishangazi tunapojikausha, baadhi ya hivi vijidudu huhamishiwa kwenye mataulo yetu.
Lakini vijidudu wanaoishi kwenye mataulo yetu hutoka kwa vyanzo vingine pia, kuvu na bakteria wanaweza kukaa kwenye nyuzi za taulo wakati wananing'inia.
Baadhi ya bakteria hutoka kwa maji ambayo tumetumia kufua taulo.
Nchini Japan, baadhi ya kaya hata hutumia tena maji ya kuoga yaliyosalia kwa kufua siku inayofuata.
Utafiti mmoja wa watafiti katika Chuo Kikuu cha Tokushima huko Japan uligundua, wakati njia hii ikiwa inaokoa maji kupotea, bakteria wengi wanaopatikana katika maji ya kuoga yaliyotumika yalihamishiwa kwenye taulo na nguo baada ya kusafishwa.
Na kwa sisi tunaopendelea mataulo yetu yakauke kwenye chumba kimoja na choo chako, kuna habari za kuchukiza sana, kila wakati unapoflashi, kuna uwezekano unachafua taulo yoyote iliyo karibu na vumbi jepesi na bakteria kutoka kwenye choo chako, pamoja na chembechembe za taka za mwili za familia yako.
Baada ya muda vijidudu hivi vinaweza kuanza kuunda safu ya bakteria au vijidudu vingine vinavyokua na kushikamana na taulo ambazo zinaweza hata kuanza kubadilisha jinsi taulo zetu zinavyoonekana.
Baada ya miezi miwili, hata kwa kuosha mara kwa mara, bakteria wanaoishi kwenye nyuzi za kitambaa cha pamba huanza kuifubaza nguo.
Lakini labda haishangazi, idadi ya bakteria na aina ya bakteria hutegemea tabia ya kufua katika kaya. Swali la kweli ni, unapaswa kuwa na wasiwasi gani kuhusu bakteria wanaoishi kwenye mataulo yako?

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Mada ya kufua taulo inaweza kuonekana kuwa ndogo, lakini Elizabeth Scott, profesa wa biolojia na mkurugenzi mwenza wa Kituo cha Usafi na Afya cha Chuo Kikuu cha Simmons cha Nyumbani na Jamii huko Boston, Marekani, anavutiwa na kile inachoweza kufichua kuhusu hilo, viini vya bakteria kuenea kuzunguka nyumba.
"Wao sio kawaida tu kukaa karibu na taulo," anasema. "Kitu chochote kinachotuletea madhara kwenye taulo kinaweza kuwa kimetoka kwa mwanadamu."
Kwa kweli, kuna aina nyingi zipatazo 1,000 za bakteria zinazoishi kwenye ngozi yetu pamoja na virusi vingine vingi na kuvu. Lakini nyingi ni nzuri kwetu, kusaidia kutulinda dhidi ya maambukizi kutoka kwa bakteria wengine wasio rafiki, kuvunja baadhi ya kemikali tunazokutana nazo katika maisha ya kila siku na kuchukua jukumu muhimu katika ukuzaji wa mifumo yetu ya kinga.
Bakteria wengi wanaopatikana kwenye taulo ni wale wale tunaowapata kwenye ngozi zetu, lakini pia wanapatikana katika mazingira tunayoishi.
Hizi ni pamoja na aina za bakteria wa Staphylococcus na Escherichia coli, ambao hupatikana kwa wingi kwenye utumbo wa binadamu, lakini pia bakteria wa Salmonella na Shigella, ambao ni sababu za kawaida za magonjwa ya chakula na kuhara.
Lakini baadhi ya bakteria hawa pia ni vimelea vya magonjwa nyemelezi, hawana hatia isipokuwa wanapofika mahali ambapo wanaweza kusababisha madhara zaidi, kama vile jeraha la kujikata, kukuza uwezo wa kutoa sumu fulani au kuweza kuwaambukiza watu walio na kinga dhaifu.
Ngozi yetu pia ni kizuizi cha asili dhidi ya maambukizi. Ni safu yetu ya kwanza ya ulinzi dhidi ya bakteria na vimelea vingine vya magonjwa, kwa hivyo kuhamisha bakteria kutoka kwenye kitambaa hadi kwenye ngozi yetu hakupaswi kututia wasiwasi sana.
Lakini kuna baadhi ya ushahidi kwamba kuosha, kusugua sana ngozi wenyewe kavu kunaweza kuharibu kazi ya ulinzi ya ngozi.
Labda tatizo kubwa hutokea tunavyobeba vijidudu hatari kwenye mikono yetu tunapovikausha kabla ya kugusa mdomo, pua na macho yetu.
Na hiyo inaweza kumaanisha taulo tunazotumia mara nyingi kwenye mikono yetu, labda zinastahili kuzingatiwa zaidi. Taulo za jikoni, ambazo hutumiwa kwenye sahani, mikono na nyuso zetu, pia ni chanzo kingine cha kuenea kwa vijidudu kwenye chakula.
Maambukizi ya tumbo yanayotokana na Salmonella, Norovirus na E. coli "yote yanaambukizwa kupitia taulo", kulingana na Scott. Uchunguzi pia umegundua kuwa virusi kama vile Covid-19 vinaweza kuishi kwenye pamba kwa hadi saa 24, ingawa maambukizi kupitia kugusa nyuso zilizo na virusi haifikiriwi kuwa njia kuu ya kuenea kwa virusi.
Virusi vingine vinavyoenea kwa kugusana, kama vile virusi vya mpox, vinaweza kuwa hatari zaidi na maafisa wa afya hawapendekezi kushirikiana taulo au kitani na watu walioambukizwa.
Utafiti pia umeonesha kwamba virusi vya papilloma ya binadamu, ambayo ni sababu ya kawaida ya warts na verrucae pia inaweza kuenea kwa kushirikiana taulo pamoja na watu wengine.
Hatari ya kusambaza maambukizi kutoka kwenye taulo za mikono zinazoweza kutumika tena ni sababu moja kwa nini hospitali na mabafu ya umma sasa yana mwelekeo wa kutumia taulo za karatasi na vikaushio vya hewa, ingawa ushahidi hauko sawa kuhusu ni chaguo gani kati ya hizo ni bora.

Chanzo cha picha, Getty Images
Ni wazi kadiri tunavyotumia taulo, na kadiri zinavyokaa na unyevu kwa muda mrefu, ndivyo mazingira yanavyokuwa ya ukarimu zaidi kwa vijidudu, na hivyo kuongeza uwezekano wa vijidudu hatari kukua.
Lakini kufikiria juu ya usafi wa taulo kunaweza pia kusaidia kupambana na moja ya masuala makuu ya kiafya yanayokabili ulimwengu, kulingana na Scott na wenzake. Bakteria sugu kwa antibiotics, kama vile MRSA, inaweza kuhamishwa kwa kugusana na vitu vilivyochafuliwa.
Jean-Yves Maillard, profesa wa biolojia katika Chuo Kikuu cha Cardiff, anasema mazoea kama vile kufua taulo mara kwa mara kunaweza kusaidia kupunguza maambukizi ya bakteria na pia kupunguza matumizi ya antibiotics.
Kwa hivyo, ni mara ngapi tunapaswa kufua taulo zetu?
Scott anapendekeza taulo za kufuliwa mara moja kwa wiki. Hatahivyo, pendekezo hili sio sheria iliyowekwa.
"Haina maana kabisa kwa sababu mtu akiumwa anatapika na kuharisha," anasema. "Wanahitaji kuwa na taulo zao na taulo hizo zinatakiwa kusafishwa kila siku. Hiyo ndiyo tunaita usafi unaozungumziwa, unakabiliana na hatari inapotokea."
Utafiti mmoja nchini India uligundua kuwa 20% ya watu waliojibu walikuwa wakifua mataulo yao mara nyingi zaidi ya mara mbili kwa wiki.
Kulingana na Scott, taulo zinahitaji moto zaidi (40-60C, 104-140F) na kufua kwa muda mrefu zaidi kuliko vitambaa vingi vya nyumbani, mara nyingi kwa kuongeza sabuni za antimicrobial.
Sabuni zinaweza kusaidia kuzuia bakteria kutoka kwenye vitambaa na kuua baadhi ya virusi. Bila shaka, kufua mara kwa mara kwa joto la juu huja na gharama ya mazingira.
Imetafsiriwa na Lizzy Masinga












