Bialowieza: Msitu hatari na njia ya siri ya Waafrika wanaokimbilia Ulaya

    • Author, Jasmin Dyer
    • Nafasi, BBC World Service
  • Muda wa kusoma: Dakika 5

Dawit, si jina lake halisi, ni kijana kutoka Ethiopia. Tunakutana naye kwenye bustani tulivu yenye kijani kibichi katika moja ya miji mikubwa ya Poland. Akiwa na aibu na akizungumza kwa sauti ya chini, amevalia koti la kofia lenye rangi ya njano na nyeusi kujikinga na baridi. Anaeleza kuwa alikimbia nchi yake ili kuepuka kulazimishwa kujiunga na jeshi.

Akilipa karibu dola 7,000 za Marekani kwa wasafirishaji haramu, alifanikiwa kufika Poland kupitia Urusi na Belarus. Dawit ni mmoja wa maelfu ya wahamiaji waliovuka mpaka kutoka Belarus kwenda Poland tangu mgogoro wa wahamiaji ulipoanza mnamo 2021.

Upande wa pili wa mpaka huu kuna msitu unaitwa Bialowieza, mojawapo ya misitu ya asili iliyosalia barani Ulaya, na eneo la urithi wa dunia la Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO). Hata hivyo, msitu huu sasa umetumiwa kama njia ya haramu ya kuingia Umoja wa Ulaya. Waafrika na raia wa mataifa mengine wakiwemo wanawake na watoto hutumia njia hii isiyo rahisi hata kidogo.

Serikali ya Poland ilijenga uzio wa urefu wa takriban kilomita 193 mwaka 2022 ili kuimarisha ulinzi wa mpaka wake na ule wa Umoja wa Ulaya. Walinzi wa mpaka wa Poland wanapiga doria usiku na mchana kwa miguu, magari ya kijeshi aina ya Humvee, na vifaru. Pia wanatumia ndege zisizo na ruani 'droni' za kisasa kufuatilia harakati na mienendo ya wahamiaji haramu katika eneo hilo.

Afisa wa polisi wa mpaka, Michal Bura, anasema: "Tunapaswa kuwa hatua moja mbele ya wasafirishaji haramu wa wahamiaji haramu. Tunapaswa kuwa hatua moja mbele ya maadui zetu." Anamuhesabu hata mlinzi wa mpaka wa Belarus kama adui.

"Walinda mpaka wa Belarus wanashirikiana na wahamiaji haramu. Wanawaelekeza wapi wapite na kuwapa vifaa kama ngazi na vikata waya," anaeleza.

Serikali ya Poland pia imetuhumiwa kwa vitendo vinavyotajwa haramu dhidi ya wahamiaji. Ripoti ya Human Rights Watch ya Desemba 2024 iligundua kuwa mamlaka za Poland "zinafukuza watu kwa nguvu na bila kujali mahitaji yao ya ulinzi, na kuwarudisha Belarus kwa njia haramu."

Kwa upande mwingine, Belarus inadaiwa kushiriki katika kurahisisha uingiaji wa wahamiaji haramu barani Ulaya. Kiongozi wa Belarus, Alexander Lukashenko, alikiri mwaka 2021 kuwa hatadhibiti uhamiaji haramu kwenda Ulaya.

Umoja wa Ulaya (EU) iliiwekea vikwazo kampuni ya usafiri ya serikali ya Belarus, Tsentrkurort, kwa kusaidia wahamiaji kufika mpakani. BBC imebaini kuwa kampuni hiyo iliomba visa za utalii za uwindaji kwa raia wa Iraq, wakiwemo watoto wa miaka mitano, ili wapate ruhusa ya kuwa katika maeneo ya hifadhi karibu na Poland.

Serikali ya Belarus inakanusha madai haya na inalaumu EU kwa kukataa kushirikiana katika kutatua mgogoro wa wahamiaji.

Licha ya juhudi za Poland kuimarisha ulinzi wa mpaka, takriban majaribio 30,000 ya kuvuka mpaka yalirekodiwa mwaka 2024, idadi ya pili kwa ukubwa tangu mgogoro uanze. Wale wanaofaulu kufika Poland mara nyingi wanafika wakiwa na hali mbaya kiafya.

Misitu ya Bialowieza ni eneo gumu na lenye msitu mnene. Uzio wa mita 5.5 wenye nyaya za miba umesababisha majeraha mabaya kwa wahamiaji. Kundi la We Are Monitoring linaripoti kuwa watu 89 wamepoteza maisha wakijaribu kuvuka mpaka huo.

Wahamiaji wanasema licha ya vifaa walivyopewa kuwasaidia kuvuka, ni jambo la kawaida kufukuzwa na mbwa wa walinzi wa mpakani wa Belarus huku walinzi hao wakitumia ngumu kuwasukuma watu kuondoka katika eneo lao na kuingia EU.

"Ukikimbia, watakufungulia mbwa," anasema Dawit. "Nimewaona watu wengi waking'atwa na umbwa shingoni na miguuni."

Olga, mfanyakazi wa kujitolea kwa shirika la misaada, anasema wahamiaji wengi wanapitia mateso makubwa. "Wana majeraha ya nyaya za miba. Wengine wamevunjika mikono au miguu baada ya kuruka uzio," anasema.

Shirika lake linatoa msaada wa dharura, mavazi ya joto, na ushauri wa hifadhi. Lakini linahofia mashambulizi kutoka kwa wale wasiopenda uwepo wa wahamiaji.

Kutokana na kuongezeka kwa idadi ya wahamiaji, mahusiano kati ya walinzi wa mpaka wa Poland na Belarus yamebadilika sana.

"Miaka michache iliyopita, tuliweza hata kuvuta sigara pamoja. Leo tunatizamana tu bila kuzungumza," anasema Bura.

Mgogoro huu unaendelea kuvuta hisia na kuibua maswali kuhusu mustakabali wa wahamiaji wanaotafuta maisha bora barani Ulaya.

Wakati huo huo, uchomaji moto msituni na taka zilizoachwa na wale wanaoingia kwenye eneo lililozuiliwa zimebadilisha pia tabia ya wanyama kwenye msitum huo wa Bialowieza.

Ili kuepuka harufu ya binadamu, makundi ya nyati wa Ulaya sasa wanahamia sehemu za msitu ambao walipuuza hapo awali.

Kuongezeka kwa matumizi huleta spishi za kigeni ambazo wataalam wa misitu lazima wafanye kazi ili kuziondoa.

Mateusz Szymura amefanya kazi kama mlinzi wa misitu huo kwa zaidi ya miaka ishirini na ameishi Bialowieza maisha yake yote. Tunapovuka daraja lililofunikwa na theluji ndani ya msitu mnene, anaieleza BBC kwamba mara nyingi huwaona wahamiaji kupitia kazi yake na ana wasiwasi kuhusu Belarusi kutochukua hatua.

"Matatizo katika Msitu wa Bialowieza yatakuwa mabaya zaidi ikiwa (viongozi wa Belarusi) wataendelea kuruhusu kuwepo kwa watu katika maeneo yaliyohifadhiwa," anasema.

Kwa Belarus inatwaja yenyewe inaacha tu wahamiaji waendelee na safari zao ya kwenda nchi zingine za Ulaya. Kazi ya walinzi wake ni kuhakikisha hawasalii kwenye ardhi ya Belarus.

Na mradi uhamiaji haramu ni kama mchezo wa kisiasa wa Belarusi, shida hii itaendelea kuathiri mipaka ya Ulaya.

Dawit aliniambia kuwa watu wengine wengi aliokutana nao katika safari yake wanatazamia kufika Uingereza. Yeye, kwa upande mwingine, aliomba hifadhi nchini Poland na ombi lake linashughulikiwa. "Nataka tu kuwa salama. Ndio maana nabaki hapa," anasema.