Alizaliwa Ufaransa lakini anatafuta fursa barani Afrika

Menka Gomis alizaliwa Ufaransa lakini ameamua mustakabali wake utakuwa nchini Senegal, ambako wazazi wake walizaliwa.
Jamaa huyu mwenye umri wa miaka 39 ni sehemu ya idadi inayoongezeka ya Waafrika wa Ufaransa wanaoondoka Ufaransa, wakilaumu kuongezeka kwa ubaguzi wa rangi na utaifa.
BBC Africa Eye imechunguza jambo hili - linalojulikana kama "msafara wa kimya" - ili kujua ni kwa nini watu kama Bw Gomis wamekatishwa tamaa na maisha nchini Ufaransa.
Raia huyo wa mjini Paris alianzisha wakala mdogo wa usafiri ambao hutoa vifurushi, hasa kwa Afrika, vinavyolenga wale wanaotaka kuunganishwa na mizizi ya mababu zao, na ana ofisi nchini Senegal.
"Nilizaliwa Ufaransa. Nilikulia Ufaransa, na tunajua ukweli fulani. Kumekuwa na ubaguzi mkubwa wa rangi. Nilikuwa na umri wa miaka sita na nilibaguliwa shuleni kila siku," Bw Gomis, ambaye alienda shule katika mji wa bandari wa kusini wa Marseille, anaambia BBC World Service.
"Ninaweza kuwa Mfaransa, lakini pia ninatoka mahali pengine."
Mamake Bw Gomis alihamia Ufaransa alipokuwa mtoto mchanga na haelewi shinikizo yake ya kuacha familia na marafiki kwenda Senegal.
"Siendi tu kwa ajili ya ndoto hii ya Kiafrika," anaeleza, akiongeza kuwa ni mchanganyiko wa wajibu anaohisi kuelekea nchi ya wazazi wake na pia kutafuta fursa.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
"Afrika ni kama Marekani wakati wa... zamani. Nadhani ni bara la siku zijazo. Ni pale ambapo kuna kila kitu kimesalia kujengwa, kila kitu kimesalia kuendelea."
Uhusiano kati ya Ufaransa na Senegal - nchi yenye Waislamu wengi na koloni ya zamani ya Ufaransa, ambayo hapo zamani ilikuwa kitovu muhimu katika biashara ya utumwa uliyovuka Atlantiki - ni mrefu na mgumu.
Uchunguzi wa hivi majuzi wa BBC Africa Eye ulikutana na wahamiaji nchini Senegal walio tayari kuhatarisha maisha yao katika vivuko hatari vya baharini ili kufika Ulaya.
Wengi wao wanaishia Ufaransa ambako, kulingana na Ofisi ya Ufaransa ya Ulinzi wa Wakimbizi na Watu Wasio na Uraia (OFPRA), idadi kubwa iliyorekodiwa iliomba hifadhi mwaka jana.
Takriban watu 142,500 waliomba hifadhi, na karibu theluthi moja ya maombi yote yalikubaliwa.
Haijabainika ni wangapi wanataka kufunga safari ya kurudi Afrika kwani sheria ya Ufaransa inakataza kukusanya data kuhusu rangi, dini na kabila.
Lakini utafiti unasema kwamba raia wa Ufaransa waliohitimu sana kutoka asili ya Kiislamu, wengi wakiwa watoto wa wahamiaji, wanahama kimya kimya.
Wale tuliokutana nao walituambia mitazamo kuhusu uhamiaji inazidi kuwa migumu nchini Ufaransa, huku vyama vya mrengo wa kulia vikiwa na ushawishi zaidi.
Tangu kuteuliwa kwao mwezi uliopita, Waziri Mkuu Michel Barnier na Waziri wa Mambo ya Ndani Bruno Retailleau wameahidi kukabiliana na uhamiaji ulio halali na haramu, kwa kushinikiza mabadiliko ya sheria ndani na katika ngazi ya Ulaya.

Chanzo cha picha, AFP
Fanta Guirassy ameishi Ufaransa maisha yake yote na anaendesha kituo chake cha uuguzi huko Villemomble - kitongoji cha nje cha Paris - lakini pia anapanga kuhamia Senegal, alikozaliwa mama yake.
"Kwa bahati mbaya, kwa miaka michache sasa nchini Ufaransa, tumekuwa tukihisi usalama ukipungua. Ni aibu kusema, lakini hiyo ndiyo hali halisi," kijana mwenye umri wa miaka 34 anaiambia BBC.
"Kuwa mama asiye na mwenzi na kuwa na kijana mwenye umri wa miaka 15 kunamaanisha kuwa daima una fundo hili dogo tumboni mwako. Unaogopa kila wakati."
Alishangazwa mwanawe aliposimamishwa hivi majuzi na kupekuliwa na polisi alipokuwa akipiga soga na marafiki zake mtaani.
"Kama mama ni tukio linalotia kiwewe. Unaona kinachotokea kwenye TV na unaona kinatokea kwa wengine."
Mwezi Juni mwaka jana, ghasia zilizuka kote nchini Ufaransa kufuatia kupigwa risasi kwa Nahel Merzouk kijana mwenye umri wa miaka 17 - raia wa Ufaransa mwenye asili ya Algeria ambaye aliuawa na polisi.
Kesi hiyo bado inachunguzwa, lakini ghasia hizo zilitikisa taifa hilo na kuakisi hali ya hasira ambayo imekuwa ikijijengeka kwa miaka mingi kutokana na jinsi makabila madogo yanavyoshughulikiwa nchini Ufaransa.
Utafiti wa hivi majuzi wa watu weusi nchini Ufaransa ulionyesha kuwa 91% ya wale waliohojiwa walikuwa waathiriwa wa ubaguzi wa rangi.
Kutokana na ghasia hizo, Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Kibinadamu (OHCHR) alitoa wito kwa Ufaransa kushughulikia "masuala ya ubaguzi wa rangi ndani ya vyombo vyake vya sheria".
Wizara ya mambo ya nje ya Ufaransa ilipuuzilia mbali ukosoaji huo, ikisema: "Shutuma zozote za ubaguzi wa kimfumo au ubaguzi unaofanywa na polisi nchini Ufaransa hazina msingi kabisa. Ufaransa na polisi wake wanapambana vikali dhidi ya ubaguzi wa rangi na aina zote za ubaguzi."
Hata hivyo, kulingana na takwimu za wizara ya mambo ya ndani ya Ufaransa, uhalifu wa kibaguzi uliongezeka kwa theluthi moja mwaka jana, na zaidi ya matukio 15,000 yaliyorekodiwa kulingana na rangi, dini au kabila.
Kwa mwalimu wa shule Audrey Monzemba, ambaye ana asili ya Kongo, mabadiliko hayo ya kijamii "yamezua wasiwasi sana".
Mapema asubuhi moja, tunaungana naye katika safari yake kupitia jumuiya ya watu wa tamaduni mbalimbali na ya wafanyakazi kwenye viunga vya Paris.
Akiwa na binti yake mchanga, yeye husafiri kwa basi na gari-moshi, lakini anapokaribia shule anamofanyia kazi, yeye huvua hijabu hijabu yake .
Kwa Ufaransa isiyopendelea dini, kuvaa hijab kumekuwa na utata mkubwa na miaka 20 iliyopita wanaovaa vazi hilo walipigwa marufuku katika shule zote za serikali - ni sehemu ya sababu zinazomfanya Bi Monzemba kutaka kuondoka Ufaransa akitafuta kuhamia Senegal ambapo ana uhusiano.
"Sisemi kwamba Ufaransa sio kwangu, nasema tu ninachotaka ni kuweza kustawi katika mazingira yanayoheshimu imani yangu na maadili yangu, nataka kwenda kufanya kazi bila kulazimika kuvuliwa hijabu yangu," anasema mwanamke huyo mwenye umri wa miaka .
Utafiti wa hivi majuzi wa Waislamu zaidi ya 1,000 wa Ufaransa ambao wameondoka Ufaransa na kwenda kuishi ng'ambo unaonyesha kuwa ni mwelekeo unaoendelea.
Hatua hiyo inafuatia kilele cha chuki dhidi ya Uislamu kufuatia mashambulizi ya mwaka 2015 wakati wapiganaji wa Kiislamu waliwauwa watu 130 katika maeneo mbalimbali kote Paris.
Hofu za kimaadili kuhusu kutokuwa na dini na ubaguzi wa kazi "ndizo kiini cha safari hii ya kimya," Olivier Esteves, mmoja wa waandishi wa ripoti ya Ufaransa, You Love It But You Leave It, aliambia BBC.
"Hatimaye, uhamiaji huu kutoka Ufaransa unaleta shida kubwa, kwani kimsingi ni Waislamu wa Ufaransa walioelimika sana ambao wanaamua kuondoka," anasema.

Tumuangazie Fatoumata Sylla, 34, ambaye wazazi wake wanatoka Senegal, kama mfano.
"Baba yangu alipoondoka Afrika kuja hapa, alikuwa akitafuta hali bora ya maisha kwa familia yake barani Afrika. Alikuwa akituambia kila mara: 'Msisahau mulikotoka.'
Akiwa msanidi wa programu ya utalii, ambaye anahamia Senegal mwezi ujao, anasema kwa kwenda kuanzisha biashara Afrika Magharibi, anaonyesha kuwa hajasahau urithi wake - ingawa kaka yake Abdoul, ambaye kama yeye alizaliwa huko Paris, hajashawishika.
"Nina wasiwasi kumhusu. Natumai atafanya sawa, lakini sihisi haja ya kuunganishwa tena na chochote," anaambia BBC.
"Utamaduni na familia yangu iko hapa. Afrika ni bara la mababu zetu. Lakini sio yetu kwa sababu hatukuwepo.
"Sidhani kama utapata utamaduni wa mababu, au Wakanda wa kuwaziwa," anasema, akimaanisha jamii iliyoendelea kiteknolojia inayoangaziwa katika filamu za Black Panther na vitabu vya katuni.
Huko Dakar, tulikutana na Salamata Konte, ambaye alianzisha shirika la usafiri na Bw Gomis, ili kujua nini kinawangoja Waafrika wa Ufaransa kama yeye wanaochagua kuhamia Senegal.
Bi Konte alibadilisha kazi ya benki yenye malipo makubwa mjini Paris na kuhamia mji mkuu wa Senegal.
"Nilipowasili Senegal miaka mitatu iliyopita nilishtuka kusikia wakiniita 'Frenchie'," mwanamke huyo wa miaka 35 anasema.
"Nilijiambia: 'Sawa, ndiyo, kweli, nilizaliwa Ufaransa, lakini mimi ni Msenegali kama wewe.' Kwa hivyo mwanzoni, tuna hisia hii ambapo tunajiambia: 'Jamani, nilikataliwa Ufaransa, na sasa ninakuja hapa na pia nimekataliwa hapa.'
Lakini ushauri wake ni: "Lazima uje hapa kwa unyenyekevu na ndivyo nilivyofanya."
Kuhusu uzoefu wake kama mfanyabiashara, anasema imekuwa "ngumu sana".
"Mara nyingi mimi huwaambia watu kwamba wanaume wa Senegal wanachukia wanawake. Hawapendi kusikia hivyo, lakini nadhani ni kweli.
"Wanapata wakati mgumu kukubali kuwa mwanamke anaweza kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni, kwamba wakati mwingine mwanamke anaweza kutoa 'maagizo' kwa watu fulani, kwamba mimi kama mwanamke naweza kumwambia dereva aliyechelewa: Hapana, si sawa kuchelewa.'
"Nadhani tunapaswa kujidhihirisha zaidi kidogo."
Hata hivyo, Bw Gomis ana furaha anaposubiri uraia wake wa Senegal.
Kampuni yake ya Wakala wa usafiri inaendelea vizuri na anasema tayari anafanyia kazi mradi wake unaofuata – ambayo ni programu ya uchumba ya Senegal.
Imetafsiriwa na Kuchapishwa na Seif Abdalla












