Idris Elba: Kwa nini ninapanga kuhamia Afrika?

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Thomas Naadi
- Nafasi, BBC
- Muda wa kusoma: Dakika 3
Mwigizaji wa Uingereza Idris Elba ameiambia BBC kwamba atahamia Afrika ndani ya muongo mmoja ujao, ikiwa ni sehemu ya mipango yake ya kusaidia tasnia ya filamu barani humo.
Nyota huyo mwenye umri wa miaka 52, ana mpango wa kujenga studio ya filamu katika visiwa vya Zanzibar nchini Tanzania, na studio nyingine katika mji mkuu wa Ghana, Accra.
Mzaliwa wa London, Elba, ambaye mama yake anatoka Ghana na baba yake anatokea Sierra Leone, ana uhusiano mkubwa na Afrika.
Anataka kutumia uwezo wake ili kuunga mkono biashara ya filamu inayoendelea kukua - kwani anasema ni muhimu Waafrika wapate kusimulia hadithi zao wenyewe.
"Kwa hakika nafikiria kuhamia hapa; sio kufikiria, nitahamia," alisema katika mahojiano kando ya mkutano wa tasnia ya filamu huko Accra.
"Nafikiri [nitahamia] katika miaka mitano ijayo, au 10, Mungu akipenda. Niko hapa ili kukuza tasnia ya filamu - huo ni mchakato wa miaka 10 - sitaweza kufanya hivyo nikiwa ng'ambo. Napaswa kuwa ndani ya nchi, ndani ya bara."
Lakini haahidi kuishi nchi moja.
"Nitaishi Accra, nitaishi Freetown [mji mkuu wa Sierra Leone], nitaishi Zanzibar. Nitajaribu kwenda kule wanakosimulia hadithi - hilo ni muhimu sana."
Lengo moja alilo nalo ni siku moja kutengeneza filamu katika studio yake mjini Accra.
‘Hadithi zetu wenyewe’

Chanzo cha picha, IKULU TANZANIA
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Elba, ambaye aliigiza kama kiongozi wa Afrika Kusini aliyepinga ubaguzi wa rangi Nelson Mandela katika filamu ya Long Walk to Freedom 2013, anaamini ni muhimu kwa Waafrika kuwa watu muhimu katika mchakato wa utengenezaji wa filamu. Iwe mbele ya kamera, nyuma ya kamera na pia katika ufadhili, usambazaji, uuzaji na kuonyesha filamu hiyo.
Anaamini, kama vile watazamaji wa filamu ulimwenguni kote wanavyojua tofauti kati ya miji ya Marekani ya New York na Los Angeles, bila ya kuwahi kuitembelea, siku moja watakuwa na uelewa mzuri zaidi wa bara la Afrika.
"Ukitazama filamu yoyote au kitu chochote kinachohusiana na Afrika, utakachoona ni kiwewe, jinsi tulivyokuwa watumwa, jinsi tulivyotawaliwa, na vita lakini utakapo kuja Afrika, utagundua kwamba sio kweli.
"Kwa hivyo, ni muhimu sana tuwe na hadithi zetu wenyewe juu ya mila zetu, utamaduni wetu, lugha zetu, na tofauti kati ya lugha moja na nyingine. Ulimwengu haujui hilo."
Huku Nollywood ya Nigeria ikizalisha mamia ya filamu kwa mwaka, ni tasnia yenye mafanikio makubwa katika nchi hiyo. Pia kuna utamaduni, haswa katika nchi za Afrika zinazozungumza Kifaransa, wa kutengeneza filamu zenye ubora wa hali ya juu.
Elba hapo awali alitambua uwepo wa vipaji katika tasnia ya filamu barani Afrika, lakini akasema ‘kunakosekana vifaa.’
Ripoti ya 2022 ya Unesco pia iligusia jambo hilo.
Shirika la Umoja wa Mataifa la Utamaduni lilisema licha ya "ukuaji mkubwa katika uzalishaji (wa filamu), biashara ya utengenezaji filamu katika bara zima inatatizwa na masuala kama vile uharamia, mafunzo duni na ukosefu wa taasisi rasmi za filamu.”
Elba anaamini kwa njia sahihi na ushirikishwaji wa serikali zilizo tayari kuunda mazingira wezeshi, mzunguko mzuri unaweza kuanzishwa.
"Tunapaswa kuwekeza katika kusimulia hadithi zetu kwa sababu unaponiona, unajiona ni kama wewe mwenyewe na hilo hututia moyo."
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Yusuf Jumah












