Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
'Hakuna aliyeokoa maisha zaidi yake': mtu ambaye alivumbua mkanda wa kiti cha kwenye gari
Mnamo mwaka 1958, mhandisi wa mitambo wa Uswidi Nils Bohlin (1920-2002) alipewa jukumu na mtengenezaji wa gari la Uswidi la Volvo kuunda mkanda wa kiti cha gari ambao ulifanya kazi vizuri.
Hii ilitokea baada ya jamaa wa Mkurugenzi Mtendaji wa Volvo Gunnar Engelau kufariki katika ajali ya gari, ambayo ilisaidia kampuni hiyo kuongeza hatua zake za usalama.
Kabla ya 1959, mikanda ya ‘two-point’ yaani ncha mbili pekee ndiyo ilipatikana kwenye magari; na mara nyingi, watu pekee ambao walijifunga mara kwa mara walikuwa madereva wa mbio za magari.
Mikanda hiyo yenye ncha mbili iliyofungwa mwilini, huku ikipitia tumboni, katika ajali za mwendo kasi ilijulikana kusababisha majeraha makubwa kwa ndani.
Bohlin daima alikuwa na wasiwasi juu ya usalama.
Hadi wakati huo, alikuwa mbunifu wa ndege katika kampuni ya kutengeneza ndege ya Uswidi ya Saab na huko alikuwa amesaidia kutengeneza viti vya kwenye ndege.
Katika kubuni mkanda mpya wa usalama, alijikita zaidi kwenye kuvumbua mbinu bora zaidi ya kumlinda dereva na abiria dhidi ya athari za upunguzaji mwendo wa kasi unaotokea wakati gari linapoanguka.
Na katika muda wa miezi mitatu tu, Bohlin aliunda mkanda wa kiti wa aina ya ‘3-point’, bidhaa ambayo ingebadilisha milele viwango vya usalama katika sekta ya magari.
Mikanda mpya ilifunga sehemu ya juu na ya chini ya mwili; mikanda yake iliunganika kwenye usawa wa nyonga na kujifunga kwenye kile Bohlin alichoita "hatua isiyohamishika" chini ya nyonga, ili iweze kuushikilia mwili kwa usalama katika tukio la ajali.
Volvo alifurahishwa na uvumbuzi huo na akaamua kuachilia hati miliki kwa watengenezaji wengine wa magari.
Bidhaa iliyoundwa na Bohlin inakadiriwa kuokoa maisha zaidi ya milioni 1.
Kulingana na Bohlin (kama alivyonukuliwa na The New York Times katika kumbukumbu yake ya mwaka wa 2002): “Ilikuwa ni suala la kutafuta suluhisho ambalo lilikuwa rahisi na lenye ufanisi...”
"Sidhani kama kuna mtu yeyote ambaye ameokoa maisha ya wengi kama yeye," mtoto wa kambo wa Bohlin, Gunnar Örnmark, aliambia BBC.
Lakini wakati mkanda wa usalama kwenye gari ulipokuwa lazima ulimwenguni kote katika miaka ya 1970, si madereva wote waliopenda wazo hilo.
Wengi walilalamika kuhusu hali ya kutokuwa huru wakati unaendesha gari.
Hivyo, ili kuongeza uelewa kuhusu umuhimu wa kuvaa mkanda wa usalama, Bohlin alisafiri ulimwenguni kote ili kuonyesha uvumbuzi wake kwa njia isiyo ya kawaida:
"Alikuwa na haya kidogo alipozungumza na sisi kuhusu hilo (mkanda wa three-point). Angesema, 'Sio jambo kubwa,'” anakumbuka Örnmark.
Kulingana na mtoto wake wa kambo, Bohlin alikuwa na "roho nzuri, kama Santa Claus".
Bohlin aliingizwa katika Ukumbi wa Umaarufu wa Kitaifa wa Wavumbuzi wa Marekani pamoja na Thomas Edison na Graham Bell, wavumbuzi wa balbu ya umeme na simu, mtawalia.
Alifariki dunia asubuhi ambayo alipaswa kupokea tuzo. Örnmark akachukua nafasi yake.
"Nilikuwepo kupokea tuzo na kutoa hotuba kwa ajili yake. Lilikuwa jambo gumu zaidi kuwahi kufanya maishani mwangu," anasema.
“Nilimalizia hotuba yangu kwa kusema, ‘Usisahau kufunga mkanda wako’.
Tangu mwaka 1959, wahandisi wamefanyia kazi uboreshaji tu wa aina hiyo ya mkanda lakini muundo wa msingi unabaki kuwa wa Bohlin.