Twitter yamshtaki Elon Musk kwa mpango wa kutaka kuachana na ununuzi kwa kampuni hiyo wa $44bn

Elon Musk mmiliki wa kampuni ya Tesla

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Elon Musk mmiliki wa kampuni ya Tesla

Twitter imempeleka bilionea Elon Musk mahakamani ili kujaribu kumshurutisha kununua kampuni hiyo ya mitandao ya kijamii, na kuanzisha vita vya kisheria na mtu huyo tajiri zaidi duniani.

Hatua hii inafuata baada ya Bw Musk kutangaza kuwa anaondoka kwenye pendekezo lake la $44bn (£37bn) la kuchukua mtandao wa Twitter siku ya Ijumaa.

Alidai Twitter haikutoa habari kuhusu idadi ya akaunti feki na zile zinazochukuliwa kama zizizotakikana yaani ‘spam’ kwenye jukwaa hilo.

Sasa Twitter imeomba mahakama ya Delaware iamuru Bw Musk kukamilisha muunganisho huo kwa $54.20 uliyokubaliwa kwa kila hisa ya Twitter.

‘’Baada ya kuweka suala hili kwa umma la kuchukua Twitter, na baada ya kupendekeza na kisha kusaini makubaliano ya kujiunganisha kwa muuzaji, Bw Musk inaonekana anaamini kwamba yeye - tofauti na yeyote yule chini ya sheria ya mkataba wa Delaware - yuko huru kubadili mawazo yake, kuharibu kampuni, kutatiza shughuli zake, kuharibu thamani ya wenye hisa, na kuondoka,’’ ilisema kesi hiyo.

Mwenyekiti wa Twitter Bret Taylor aliweka ujumbe kwenye mtandao wa Twitter kwamba tovuti ya microblogging ilitaka ‘’kumuwajibisha Elon Musk kwa kukiuka majukumu yake ya kimkataba.’’

Bw Musk Jumanne akiweka ujumbe kwenye Twitter: ‘’Oh kejeli lol alama ya kuashiria kucheka kwa sauti kubwa.’’

Kesi hiyo ilisema Bw Musk amejitoa katika mpango huo kwa sababu ‘’hautumiki tena kwa maslahi yake ya binafsi.’’

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Bw Musk ndiye Mtendaji Mkuu wa kampuni ya magari ya umeme ya Tesla.

Kesi hiyo ilisema kwamba baada ya Bw Musk kukubaliana na mpango huo, soko la hisa lilianguka, pamoja na hisa za Tesla.

‘’Thamani ya hisa za Bw Musk katika Tesla, mtangazaji wa utajiri wake binafsi, imepungua kwa zaidi ya $100bn kutoka kilele chake cha Novemba 2021. Kwa hivyo [Bw] Musk anataka kutoka,’’ ilisema.

Badala ya kubeba gharama ya kudorora kwa soko la hisa, kama makubaliano ya kuunganisha yanavyohitaji, [Bw] Musk anataka kuihamisha kwa wamiliki wa hisa wa Twitter,’’ iliongeza.

Bei ya hisa za Twitter imeshuka kwa zaidi ya 8% katika mwezi uliopita, na mwezi Mei ilishuka kutoka kiwango cha juu cha zaidi ya $50 kwa kila hisa, huku Bw Musk akihoji idadi ya akaunti ghushi na taka kwenye Twitter na kusema mpango huo ‘’umesitishwa kwa muda.’’

Siku ya Ijumaa, Bw Musk alisema alikuwa akijiondoa katika mpango huo, akidai ukosefu wa habari kuhusu akaunti za barua zisizohitajika yaani ‘spam’ na uwakilishi usio sahihi ulifikia ‘’tukio hilo mbaya’’.

Pia alisema Twitter kuwatimua watendaji kunamaanisha kuwa haikuwa ikitimiza wajibu wake.

Katika kujibu, Twitter ilisema inapanga kufuata hatua za kisheria ili kutekeleza makubaliano hayo, ikisema ‘’imejitolea kufunga shughuli ya suala la mauzo waliyokubaliana na Bw Musk.’’

Mkataba wa awali wa kuunganisha unajumuisha ada ya kuvunja mtandao huo $1bn.

Bw Musk, aliyejitambulisha kama ‘’mtetezi huru wa kujieleza’’, alikuwa ameahidi kulegeza sheria za udhibiti wa maudhui kwenye Twitter mara tu kampuni hiyo inapokuwa chini ya umiliki wake.

Amekuwa mkosoaji mkubwa wa Twitter kupiga marufuku baadhi ya akaunti, kama vile ya Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump.

Bw Musk pia ametaka kuwepo kwa uwazi zaidi kuhusu jinsi jukwaa hilo linavyowasilisha tweets kwa watumiaji - mfumo ambao kwa sasa unaruhusu baadhi yao kukuzwa na kupewa hadhira pana zaidi.

Hisa za Twitter zilipanda kwa zaidi ya 4% huko New York Jumanne na kuongeza 1% katika biashara ya baada ya saa.

Hata hivyo hisa bado ziko karibu $20 chini ya bei ya ofa ya Bw Musk ya $54.20.