Paul Kagame: Rais anayetaka kuongoza muhula wa nne madarakani

Chanzo cha picha, AFP
- Author, Didier Bikorimana
- Nafasi, BBC Great Lakes service
Kuna nafasi ndogo sana ya maboresho kwa Rais wa Rwanda Paul Kagame katika uchaguzi wa Jumatatu baada ya kupata karibu 99% ya kura mara ya mwisho.
Kiwango cha ushindi wake mwaka wa 2017, pamoja na asilimia 95 mwaka wa 2003 na 93% mwaka wa 2010, vilizua maswali kuhusu ukweli wa demokrasia katika uchaguzi huo.
Ukosoaji ambao mkimbizi wa zamani na kiongozi wa waasi anaupuuzia kwa ujasiri.
"Kuna wale wanaofikiri kuwa 100% sio demokrasia," Bw Kagame aliwaambia maelfu ya wafuasi waliokuwa wakishangilia katika mkutano wa kampeni magharibi mwa Rwanda mwezi uliopita.
Akizungumzia uchaguzi mahali pengine, bila kutaja nchi husika, aliongeza: “Kuna wengi waliopigiwa kura wakiwa madarakani kwa asilimia 15... Je, hiyo ndiyo demokrasia?''
Kinachotokea Rwanda ni mambo ya Rwanda, rais alisisitiza.
Wafuasi wake walikubali, wakiimba "waje wajifunze" huku wakipeperusha bendera nyekundu, nyeupe na buluu za chama tawala cha Rwandan Patriotic Front (RPF).
Akiwa na urefu wa zaidi ya futi 6 (m 1.83), baba mwenye umri wa miaka 66 mwenye watoto wanne alipunguza ukali akiwa mwenye kuvutia katikati ya umati.
Anaweza kutabasamu na kufanya utani, lakini kiongozi huyo anayevalia miwani anaweza kuiweka sura ya mzee aliyekasirishwa.
Anavyozungumza taratibu na kwa kufikiria humlazimu msikilizaji kuzingatia na anachosema na anapozungumza huwaanaelewa wazi, hafichi maneno yake.
Hata wakati ambapo anatumia lugha ya mafumbo au ya kidiplomasia zaidi, atatumia vidokezo kuwajulisha watu anachozungumza.
End of Unaweza kusoma

Chanzo cha picha, AFP
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Maisha ya Bw.Kagame yametokana na mzozo kati ya makabila ya Watutsi na Wahutu wa Rwanda.
Ili kuondokana na hili, serikali yake sasa inasisitiza kwamba watu wajitambulishe kuwa Wanyarwanda badala ya kabila.
Akiwa rais tangu mwaka 2000, anagombea muhula wa nne, lakini Bw Kagame amekuwa kiongozi wa nchi hiyo ya Afrika Mashariki tangu Julai 1994. Hapo ndipo jeshi lake la waasi lilipoiondoa serikali ya Wahutu wenye msimamo mkali ambao walikuwa wamepanga mauaji ya kimbari ya mwaka huo.
Awali aliwahi kuwa makamu wa rais na waziri wa ulinzi.
Wafuasi wake wengi, miongoni mwao baadhi ya wanasiasa wakuu wa nchi za Magharibi, wanamsifu kwa kuleta utulivu na kuijenga Rwanda baada ya mauaji makubwa ambapo watu 800,000 wa kabila la Watutsi na Wahutu wenye msimamo wa wastani waliuawa.
Baadhi wanashutumu jeshi lake la wakati huo la waasi kwa mauaji ya kulipiza kisasi wakati huo, lakini serikali yake imekuwa ikisema mara kwa mara yalikuwa matukio nadra kutokea na kwamba waliohusika waliadhibiwa.
Rais hajachelea katika ukosoaji wake dhidi ya nchi za magharibi lakini pia hutafuta uungwaji mkono wa nchi hizo na wakati mwingine anatumia majuto yao katika kushindwa kuzuia mauaji ya kimbari
Rwanda pia ilikuwa mshirika na mnufaika wa kifedha katika mpango wa Uingereza ambao sasa haujakamilika kuwapeleka wanaotafuta hifadhi nchini humo.
"Nitampigia kura PK, bila shaka," anasema mwanafunzi wa chuo kikuu Marie Jeanne, akimtaja Bw.Kagame kwa herufi zake za kwanza za jina lake.
“Angalia jinsi ninavyosoma vizuri. Kama asingekuwa rais, huenda nisingesoma vizuri labda kutokana na ukosefu wa usalama,” aliiambia BBC.
Kwake, jibu la nani angempigia kura lilikuwa dhahiri, lakini kuna majina mengine mawili ya kuzingatia kwenye karatasi ya kupigia kura kwa wapiga kura milioni tisa waliojiandikisha.
Frank Habineza wa chama cha Democratic Green Party na Philippe Mpayimana wa chama cha Independent, wote wanawania tena, baada ya kuwania katika uchaguzi wa urais miaka saba iliyopita.
Hatahivyo, mara ya mwisho walipata takriban 1% ya kura kati yao.
Vyama vingine vya kisiasa vimemuunga mkono Bw. Kagame kuwa rais.
Mwanasiasa wa upinzani Diane Rwigara, mkosoaji mkubwa wa Bw.Kagame, alizuiwa kushiriki kwa madai kwamba hakuwasilisha nyaraka sahihi, ambapo alipuuzilia mbali akidai ni kisingizio cha kumzuia kugombea.

Chanzo cha picha, AFP
Bw.Kagame pia ameshutumiwa kwa kuwanyamazisha, kupitia kifungo na vitisho, wapinzani wengine muhimu. Aliwahi kukiambia kituo cha habari cha Al Jazeera kwamba hapaswi kuwajibika kwa upinzani dhaifu.
Mtandao wake wenye nguvu wa majasusi umedaiwa kutekeleza mauaji ya kuvuka mpaka na utekaji nyara.
Wanadaiwa hata kumlenga kiongozi wao wa zamani, mkuu wa zamani wa ujasusi Kanali Patrick Karegeya, ambaye alitoroka Rwanda baada ya kutofautiana na Bw. Kagame.
Aliuawa mwaka wa 2014 akiwa chumbani kwake katika hoteli ya kifahari katika jiji kuu la Afrika Kusini, Johannesburg.
"Walitumia kamba kumnyonga," alisema David Batenga, mpwa wa Kanali Karegeya.
Bw.Kagame hakuchukua hatua kubwa kujitenga na mauaji hayo, huku akikana rasmi kuhusika kwa vyovyote vile.
"Huwezi kuisaliti Rwanda na usiadhibiwe kwa hilo," aliuambia mkutano muda mfupi baadaye. "Mtu yeyote, hata wale ambao bado wako hai, watavuna matokeo. Mtu yeyote. Ni suala la muda."
Katika jitihada za kutafuta usalama nyumbani, imesababisha rais huyo kutuma wanajeshi katika nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo akisema wanafuatilia kundi la waasi wa Kihutu.
Rwanda pia inashutumiwa kwa kuunga mkono kundi la waasi la M23 huko, jambo ambalo inakanusha, licha ya ushahidi mwingi, ikiwa ni pamoja na ripoti ya hivi karibuni ya Umoja wa Mataifa.
"Kwa kweli kusema ukweli, (uchaguzi) ni mchezo wa kuigiza," anasema Filip Reyntjens akitafakari kuhusu kura hiyo. Mwanasayansi huyo wa siasa za Ubelgiji ni mtaalamu wa eneo la Maziwa Makuu.
"Kwa kweli sijui nini kitatokea wakati huu, lakini chaguzi zilizopita zimekuwa ... sarakasi.
"Ninamaanisha tume ya taifa ya uchaguzi inakisia badala ya kuhesabu kura," anadai, akinukuu ripoti ya mwisho ya ujumbe wa waangalizi wa Umoja wa Ulaya (EU) ya 2003 na ripoti ya ujumbe wa waangalizi wa Jumuiya ya Madola ya 2010.
Tume ya uchaguzi ya Rwanda inasema kwenye tovuti yake kwamba inaendesha "chaguzi huru, za haki na za uwazi ili kukuza demokrasia na utawala bora nchini Rwanda".
"Kwangu mimi, uchaguzi ujao wa rais nchini Rwanda si tukio," anasema Dk Joseph Sebarenzi, spika wa zamani wa bunge la Rwanda, ambaye alipoteza wazazi na wanafamilia wengi wakati wa mauaji ya kimbari, na sasa anaishi uhamishoni Marekani.
"Uchaguzi ni kama mchezo wa mpira wa miguu ambapo mratibu pia ni mshindani, anachagua washindani wengine, anaamuru watu kuhudhuria mchezo, na ambapo kila mtu anamjua mshindi aliyeamuliwa mapema lakini lazima aoneshe kama mchezo ni halisi."
Bw Kagame, ambaye ni shabiki mkubwa wa soka na anafuatilia kwa karibu klabu ya Ligi Kuu ya Uingereza Arsenal, anakana maelezo haya.

Chanzo cha picha, AFP
Alizaliwa mwaka wa 1957 katika familia tajiri katikati mwa Rwanda, alikuwa mtoto wa mwisho kati ya watoto watano.
Lakini, akiwa na umri wa miaka miwili tu, alikua mkimbizi katika nchi jirani ya Uganda, akikimbia mateso na unyanyasaji wa mwishoni mwa miaka ya 1950 pamoja na familia yake na maelfu ya watu wengine kutoka jamii ya Watutsi walio wachache.
Licha ya kuwa mtoto wakati huo, Bw.Kagame amesema bado anaweza kukumbuka ''Tuliweza kuona watu wakichoma nyumba huko''.
"Walikuwa wakiua watu. Mama yangu alikuwa amekata tamaa sana. Hakutaka kuondoka mahali hapa," rais alimwambia mwandishi wa habari wa Marekani na mwandishi wa wasifu asiye rasmi Stephen Kinzer.
Mauaji haya yalikuja baada ya wakoloni wa Ubelgiji kubadili kabila wanaloliunga mkono, na kupendelea wasomi wanaoibuka kutoka kabila kubwa la Wahutu, ambao baadhi yao waliteswa vibaya chini ya utawala wa kifalme wa Watutsi.
Rwanda ilipata uhuru wake mwaka 1962.
Mwishoni mwa miaka ya 1970, Bw Kagame alifanya mfululizo wa ziara za siri nyumbani.
Akiwa katika mji mkuu, Kigali, alitembelea hoteli fulani huko Kiyovu, mojawapo ya vitongoji tajiri zaidi vya jiji hilo. Baa yake ilikuwa maarufu kwa wanasiasa, maafisa wa usalama na watumishi wa umma ambao walipiga porojo huku wakinywa bia baada ya kazi.
Bw.Kinzer aliandika kwamba kiongozi wa baadaye alisikiliza mazungumzo yao huku akinywa soda ya chungwa akiwa ameketi peke yake kwenye meza na kuepuka kufuatiliwa.
Ziara hizi katika nchi yake zilizidisha shauku yake katika kazi ya ujasusi.
Alipata mafunzo ya ujasusi wa kijeshi nchini Uganda na kujiunga na uasi uliofanikiwa nchini humo ulioongozwa na Yoweri Museveni ambao ulimfanya achukue mamlaka mwaka wa 1986.
Bw.Kagame alipata mafunzo zaidi nchini Tanzania, Cuba na Marekani.
Kisha aliongoza jeshi lake la waasi wengi wa Kitutsi ambalo liliingia Rwanda mwaka 1990.
“Mafunzo yalikuwa ya manufaa. Cuba, katika vita vyake na Marekani na uhusiano na Urusi, ilikuwa imeendelea sana katika masuala ya kijasusi. Pia kulikuwa na elimu ya kisiasa: Mapambano yanahusu nini? Unayaendeleza vipi?” alimwambia Bw Kinzer.

Chanzo cha picha, AFP
Amejaribu kuendeleza mapambano kwa kulenga maendeleo ya kiuchumi, Bw.Kagame alipendekeza Rwanda ingeiga Singapore au Korea Kusini na kupata maendeleo kizazi hata kizazi.
Ingawa Rwanda ilikosa kufikia lengo lake la nchi yenye uchumi wa kati kufikia 2020, Prof Reyntjens anasema "hii ni nchi inayoendeshwa vyema".
"Tatizo nchini Rwanda ni uongozi wa kisiasa, hakuna uwanja wa usawa, hakuna nafasi kwa upinzani, hakuna uhuru wa kujieleza, ambao unahatarisha kufuta mafanikio ya utawala bora wa wasomi."
Lakini Bw Kagame anasisitiza kuwa umati mkubwa wa wafuasi kwenye mikutano yake ni mfano mmoja tu wa imani na upendo wa Wanyarwanda walio nao kwake na matakwa yao kwamba aendelee kuwa kiongozi wao, ingawa aliwahi kusema kuwa alikuwa ameandaa mrithi ifikapo 2017.
Kwa sababu ya mabadiliko ya katiba, anaweza, kwa nadharia, kubaki madarakani hadi 2034.
"Muktadha wa kila nchi" ni muhimu, Bw.Kagame alisema katika mahojiano ya moja kwa moja kwenye kituo cha utangazaji cha serikali mwezi uliopita, akizungumzia suala la muda wake madarakani.
“(Magharibi wanasema): ‘Oh umekuwa madarakani kwa muda mrefu sana’. Lakini hiyo sio kazi yako. Ni masuala ya watu hawa hapa."
Maelfu ya maili nchini Marekani, Dk Sebarenzi anasema hajui mustakabali wa nchi yake, inayojulikana kwa upendo kama ardhi ya milima elfu, lakini anaongeza: "Historia inaonesha kwamba katika nchi ambazo mkuu wa nchi ana nguvu zaidi. kuliko taasisi za serikali, mabadiliko ya mamlaka yanaweza kugeuka kuwa vurugu, na kusababisha vipindi vya machafuko baada ya utawala."
Imetafsiriwa na Lizzy Masinga na kuhaririwa na Maryam Abdalla












