Kagame anawania muhula wa nne kuwa rais wa Rwanda

Na Danai Nesta Kupemba

BBC News, London

TH

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Rais Paul Kagame alishinda uchaguzi uliopita kwa asilimia 99 ya kura

Rais wa Rwanda Paul Kagame, ambaye anaogopwa na kusifiwa kwa njia sawa, analenga kuendeleza utawala wake wa miaka 24 katika uchaguzi amabao wachambuzi wanasema atapata ushindi mkubwa.

Ametawala kila chaguzi tangu kuwa rais mwaka 2000, na zaidi ya 90% ya kura. Mnamo 2017 alishinda kwa 99%.

Bw Kagame mwenye umri wa miaka 66, anakabiliwa na wagombea wawili pekee ambao waliidhinishwa kugombea - wagombea wengine walizuiwa na tume ya uchaguzi inayosimamiwa na serikali.

Rais Kagame amekuwa akitawala siasa za Rwanda tangu majeshi yake ya waasi yachukue mamlaka mwishoni mwa mauaji ya halaiki ya mwaka 1994 ambayo yaliua takriban Watutsi 800,000 na Wahutu wenye msimamo wa wastani.

Tangu wakati huo, amesifiwa kwa kusimamia muimariko wa ajabu wa nchi na kuunganisha Rwanda

"Rwanda ilifutwa miaka 30 iliyopita - lakini kwa hisani ya uongozi wa Kagame na chama chake tawala Rwanda iliweza kujenga uthabiti," Dk Felix Ndahinda, msomi kuhusu eneo la Maziwa Makuu, aliiambia BBC.

Lakini wakosoaji wake wamemshutumu Bw Kagame kwa kutoruhusu upinzani wowote - kiasi cha kupanga mauaji ya wapinzani nje ya mipaka ya nchi hiyo .

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Bw Kagame amekuwa akitetea vikali rekodi ya Rwanda kuhusu haki za binadamu, akisema nchi yake inaheshimu uhuru wa kisiasa.

Lakini mchambuzi mmoja aliiambia BBC uchaguzi huo ulikuwa ni "utaratibu" tu.

Takriban watu milioni tisa wamejiandikisha kupiga kura, kulingana na tume ya uchaguzi, na takriban milioni mbili ndio wapiga kura wa mara ya kwanza.

Mshindi wa muda anapaswa kujulikana kufikia Jumanne asubuhi.

Wapiga kura watamchagua rais na wabunge 53 wa Baraza la chini la Bunge siku ya Jumatatu, huku wabunge wengine 27 wakichaguliwa siku inayofuata.

"Nina furaha sana kuhusu kupiga kura kwa mara yangu ya kwanza, siwezi kusubiri," Sylvia Mutoni aliambia BBC.

Kwa vijana wengi nchini Rwanda, Bw Kagame ndiye kiongozi pekee ambaye wamewahi kumjua.

Hata wakati akiwa makamu wa rais na waziri wa ulinzi kutoka 1994 hadi 2000 alikuwa kiongozi halisi wa nchi, na amekuwa rais tangu 2000.

Wagombea wawili wa upinzani - Frank Habineza, wa chama cha Democratic Green Party na Philippe Mpayimana ,mgombea huru - wote walishiriki katika uchaguzi wa 2017, ambapo wote pamoja walipata chini ya asilimia 1% ya kura .

Lakini hawajakata tamaa.

"Ninaamini demokrasia ni mchakato," Bw Habineza aliambia podikasti ya BBC Focus on Africa.

"Watu bado wana hofu ya kutoa maoni yao. Ninapigania uhuru wa kusema, uhuru wa vyombo vya habari," alisema.

Na baadhi ya Wanyarwanda wanamsikiliza. Mpiga kura mmoja aliambia BBC kuwa hatampigia kura rais aliye madarakani.

Celestin Mutuyeyezu, 28, aliwahi kumuunga mkono Bw Kagame, lakini uchaguzi huu amebadilishwa mawazo na Bw Habineza.

"Alisema mambo mazuri juu ya kupambana na ukosefu wa ajira, na amenipata," alisema.

Lakini kumshinda Rais Kagame sio jambo rahisi .

Diane Rwigara, mkosoaji mkubwa wa rais, alizuiwa kugombea katika uchaguzi huo. Aliondolewa pia katika uchaguzi wa 2017.

"Rwanda inatambuliwa kama nchi ambayo uchumi umekuwa ukiboreka. Lakini kimsingi, ni tofauti. Watu wanakosa mambo ya msingi maishani kama vile chakula, maji, makazi," aliiambia BBC.

Tume ya uchaguzi ilisema ameshindwa kutoa nyaraka sahihi.

TH

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Wanyarwanda wengi wamemfahamu Paul Kagame pekee kama kiongozi wa nchi

Ingawa nchi inaendelea kukabiliwa na viwango vya juu vya ukosefu wa ajira kwa vijana, ni moja ya nchi zinazokua kwa kasi kiuchumi barani Afrika.

Bw Kagame anasifiwa kwa mabadiliko ya kiuchumi na utulivu wa Rwanda katika miongo mitatu iliyopita.

Rwanda inajulikana duniani kote kwa mji wake mkuu safi na kuwa na idadi kubwa zaidi ya wabunge wanawake, 61%.

Katika kitabu Rwanda, Inc. Waandishi wa Marekani Patricia Crisafulli na Andrea Redmond wanamtaja Bw Kagame zaidi kama Afisa Mkuu Mtendaji wa kampuni kuliko kiongozi wa kisiasa kwa sababu ya "nia yake ya ubora" katika kila sekta nchini.

Pia ni mwanasiasa mjanja.

Licha ya mara kwa mara kuzikosoa nchi za Magharibi, anajaribu kukuza washirika muhimu - kwa mfano kwa kufanya kazi na Uingereza katika mpango wake uliofutwa sasa wa kuwaleta wanaotafuta hifadhi nchini Rwanda.

Rwanda pia imekuwa ikitumia nguvu yake na ushawishi katika jukwaa la kimataifa, kwa kujenga mvuto wake kupitia michezo, utamaduni, na burudani.

Nchi hiyo ndogo ya Afrika Mashariki ni nyumbani kwa Ligi ya mchezo wa Kikapu ya Afrika, ambayo ni ushirikiano na NBA. Iliandaa Mkutano wa Wakuu wa Serikali wa Jumuiya ya Madola mnamo 2022 na nyota wa kimataifa kama Kendrick Lamar wamefanya tamasha huko.

Diplomasia ya Bw Kagame pia ina upande mgumu sana.

Uchaguzi huo unakuja siku chache baada ya ripoti ya Umoja wa Mataifa kusema kuwa kuna wanajeshi 4,000 wa Rwanda katika nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ambako wanatuhumiwa kuunga mkono kundi la waasi la M23.

Rwanda haikukanusha madai hayo na kuiambia BBC kuwa serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo haina dhamira ya kisiasa ya kusuluhisha mzozo huo wa mashariki mwa nchi hiyo yenye utajiri wa madini, ambao umeshuhudia miongo kadhaa ya machafuko.

Katika kampeni Bw Kagame aliahidi kuilinda Rwanda dhidi ya "uchokozi wa nje" huku kukiwa na mvutano kati ya nchi jirani za DR Congo na Burundi.

Imetafsiriwa na Yusuf Jumah