Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Kanisa la Anglikana linatazamia matumizi ya lugha isiyo ya kijinsia katika kumtaja Mungu
Kanisa la Anglikana litaangalia matumizi ya maneno yasiyoegemea jinsia kumrejelea Mungu katika sala, lakini taasisi hiyo iliyodumu kwa karne nyingi ilisema hakuna mipango ya kukomesha jinsi sala za sasa zinavyofanyika.
"Wakristo wanatambua tangu zamani kwamba Mungu si mwanamume wala si mwanamke," msemaji wa Kanisa alisema. "Lakini aina mbalimbali za njia za kuhutubia na kuemuelezea Mungu zinazopatikana katika maandiko hazijaonyeshwa kila mara katika ibada yetu."
Lakini aliongeza kuwa "hakuna mipango kabisa ya kukomesha au kurekebisha kwa kiasi kikubwa" sala zilizoidhinishwa na kwamba hakuna mabadiliko yanayoweza kufanywa bila "sheria kubwa".
Maoni hayo yanafuatia kutokana na mjadala wa Sinodi Kuu, baraza linaloongoza la Kanisa, ambapo padri aliuliza juu ya kukuza lugha shirikishi zaidi katika aina za ibada zilizoidhinishwa na kutafuta chaguzi kwa wale wanaotaka kuzungumza juu ya Mungu kwa "njia isiyo ya jinsia".
Msemaji huyo alisema kumekuwa na shauku kubwa ya kuchunguza lugha mpya tangu kuanzishwa kwa aina zake za sala katika lugha ya kisasa zaidi ya miaka 20 iliyopita.
Askofu Michael Ipgrave, makamu mwenyekiti wa tume ya kiliturujia ya Kanisa hilo, alisema Kanisa limekuwa "linachunguza matumizi ya lugha ya kijinsia kuhusiana na Mungu kwa miaka kadhaa".
Majadiliano hayo ni jaribio la hivi punde zaidi la Kanisa, ambalo ni kitovu cha mojawapo ya taasisi kongwe zaidi za Kikristo duniani, ili kuendana na dhana zinazobadilika kwa kasi kuhusu jinsia na ujinsia katika miongo ya hivi karibuni.
Baraza hilo la kidini mwezi uliopita lilitoa mapendekezo yanayoonyesha kuwa lingekataa kuwaruhusu wapenzi wa jinsia moja kuoana katika makanisa yake, lakini likasema makasisi wanaweza kuwabariki kanisani.
Pia iliomba radhi kwa watu wa LGBTQI+ kwa kukataliwa na uhasama ambao wamekabiliana nao.
Tume ya Imani na Utaratibu wa Kanisa - ambayo inashauri juu ya theolojia - itafanya kazi na tume ya kiliturujia katika kuangalia maswali kuhusu suala la jinsia, msemaji alisema.