'Nikipiga risasi ya kwanza, nitakuua mwanangu'

"Nina hakika nitakuua – nikipiga risasi ya kwanza," baba anaonya.

Anampigia simu mwanawe wa kiume, ambaye anahudumu katika jeshi la Myanmar.

Bo Kyar Yine alijiunga na upinzani wenye silaha baada ya mapinduzi ya kijeshi yaliyoiondoa serikali ya Myanmar iliyochaguliwa kidemokrasia Februari 2021-vita vya kikatili vya wenyewe kwa wenyewe vilivyofuata vimegawanya familia yake.Sasa anapigana dhidi uongozi wa jeshi ambao mtoto wake anatetea.

"Jeshi linaharibu nyumba, kuzichoma moto," Bo Kyar Yine anasema, akimsihi mwanawe kuondoka jeshini.

"Inaua watu, inapiga risasi kuwaua waandamanaji isivyo haki, inaua watoto bila sababu, inabaka wanawake.Huenda hujui hilo." "Hayo ni maoni yako, baba. Hatuoni hivyo," Nyi Nyi anajibu kwa heshima.

Licha ya kukanusha vile, ukatili unaofanywa na wanajeshi umeenea sana na umethibitishwa. Baada ya simu hiyo, Bo Kyar Yine anasema anajaribu kuwashawishi wanawe wote kuachana na upinzani.

"Hawasikii kwa hivyo itakuwawatajua wenyewe tutakutana vitani".

"Katika maharagwe machache, kuna mawili au matatu magumu. Ni sawa katika familia," anasema. "Inawezekana kwamba wengine sio wazuri."

Bo Kyar Yine na mkewe Yin Yin Myint walikuwa na watoto wanane - watoto wao wawili wa kiume walipojiunga na jeshi, walijivunia. Baba aliweka picha za sherehe yao ya kuhitimu jeshini kama kumbukumbu. Wanawe wote wawili wakawa maofisa.

Ilikuwa heshima kubwa kuwa na askari wa wana, anasema. Huu ulikuwa wakati ambapo watu katika sehemu hii ya katikati mwa Myanmar walikaribisha jeshi katika vijiji vyao wakiwa na maua.

Yin Yin Myint anasema familia nzima ilifanya kazi mashambani kutafuta pesa ili wavulana hao wawili wapate elimu na kujiunga na jeshi.

Kabla ya vita vya wenyewe kwa wenyewe, kuhudumu katika Tatmadaw, kama majeshi ya Myanmar yanavyojulikana, iilikuwa ni hadhi kubwa katika kijamii na kiuchumi kwa familia.

Lakini mapinduzi ya mwaka jana yalibadilisha kila kitu.Bo Kyar Yine alipoona jeshi likiwakandamiza waandamanaji wasio na silaha wa demokrasia hakuweza tena kuwaunga mkono na kuwataka wanawe kuondoka jeshini.

"Kwanini waliwapiga risasi na kuwaua watu waliokuwa wakiandamana? Kwanini waliwatesa? Mbona wanaua watu bila sababu?" anauliza.

Anasema yote hayo yamemvunja moyo.

Kabla ya mapinduzi ya kijeshi, Bo Kyar Yine alikuwa mkulima ambaye hajawahi kushika bunduki.

Sasa, yeye ni kiongozi wa kitengo cha wanamgambo wa kiraia. Wao ni sehemu ya mtandao legelege unaoitwa Jeshi la Ulinzi la Wananchi (PDF), ambao wanapigania kurejesha demokrasia dhidi ya jeshi kubwa zaidi na lenye silaha bora zaidi.

Anawataja wanajeshi sasa kama "mbwa", neno la dharau sana nchini Myanmar.

"Wakati kundi la mbwa linapoingia [kwenye kijiji], kuwabaka wanawake, kuchoma nyumba na kupora mali... Inabidi tusimame dhidi yao," anasema.

Bo Kyar Yine anaongoza kitengo cha wapiganaji wapatao 70 wanaounga mkono demokrasia wanaojiita Wild Tigers.

Wana bunduki tatu tu za moja kwa moja. Wanawe wengine wanne wanapigana pamoja naye. Wanawe wengine wawili katika jeshi wako umbali wa kilomita 50 tu kutoka kambi yao ya waasi.

"Tulifikiri tunaweza kutegemea wana wetu askari," anasema Yin Yin Myint kwa huzuni. "Lakini sasa wanatusumbua."

'Mlio wa risasi ulisikika kama mvua'

Ilikuwa saa tatu asubuhi mwishoni mwa Februari wakati kitengo cha PDF cha Bo Kyar Yine kilipokea simu kutoka kwa kijiji cha karibu. Jeshi lilikuwa likiwavamia.

"Tunahitaji msaada, mbwa [askari] wameingia katika kijiji chetu, njooni mtusaidie. Tutumie nguvu," ulikuwa ujumbe.

Min Aung, mwanawe wa pili, alikuwa wa kwanza kujiandaa kuondoka. Mama yake, akijua kwamba hawezi kumzuia, alimwomba arudi salama.

The Wild Tigers waliondoka kwa msafara wa pikipiki. Bo Kyar Yine alipanda mbele na Min Aung, akiongoza kitengo kama kawaida.

Walikuwa wakisafiri kwa njia waliyoizoea ambayo ilikuwa salama siku za nyuma walipoviziwa.

"Hakukuwa na mahali pa kujificha, hakuna miti mikubwa au kitu chochote," anasema Min Naing, mtoto mwingine wa kiume. "Walitupiga risasi kama popcorn zinazojitokeza," anasema.

"Tulikuwa kwenye uwanja wa mauaji. Silaha zetu hazikulingana na zao." Bo Kyar Yine aliwaamuru warudi nyuma. Walijificha nyuma ya shamba la mpunga.

"Mtu kati yao alionekana kunijua," anasema Bo Kyar Yine. Anahisi ndiye alikuwa lengo la mashambulizi yao.

"Niliwafyatulia risasi nikianza kukimbia kisha nikaendelea kufyatua risasi na kukimbia." Yin Yin Myint alikuwa akingoja kwa wasiwasi kambini na aliweza kusikia kinachoendelea.

"Milio ya risasi ilikuwa ikasikika kama mvua inanyesha," anasema huku akitokwa na machozi.

Saa chache baada ya shambulio hilo, wanajeshi walichapisha picha za picha za waliofariki kwenye mtandao wa Facebook, wakijigamba kuwa wamewaua watu 15. Hapo ndipo Yin Yin Myint alipogundua kuwa alikuwa amempoteza Min Aung, mtoto aliyekuwa naye karibu zaidi. “Mwanangu alinijali sana,” asema.

"Angenisafisha jikoni. Alinifua nguo zangu. Alikusanya saroni zangu kutoka kwenye mstari wa kufulia. Alikuwa mzuri sana kwangu." Mnamo Juni, wanajeshi waliteketeza nyumba ya familia hiyo na mali zao zote pamoja na nyumba 150 katika kijiji chao.

Kumekuwa na mashambulizi ya uchomaji moto yanayofanywa na wanajeshi kote nchini hasa katikati mwa Myanmar.

Inaonekana kuwa wanajeshi walijua jukumu la Bo Kyar Yine katika upinzani - ikiwa wanafahamu kuwa ana wana katika vikosi vya jeshi haijulikani wazi.

Yin Yin Myint anajitahidi kukabiliana na yote aliyopoteza. "Nyumba yangu iliteketea na nikampoteza mwanangu. Siwezi kuvumilia kwa kweli. Akili yangu haiko sawa na mwili wangu, ni kama nina kichaa," anasema.

Tangu jeshi lichukue mamlaka, zaidi ya watu milioni 1.1 kote Myanmar wameyakimbia makazi yao na takriban nyumba 30,000 zimeteketezwa.

Zaidi ya watu 2,500 wamethibitishwa kuuawa na vikosi vya usalama tangu mapinduzi hayo, Chama cha Msaada kwa Wafungwa wa Kisiasa kinasema.

Jumla ya takwimu za majeruhi kwa pande zote mbili zinakadiriwa kuwa mara 10 zaidi, kulingana na data kutoka kwa kikundi cha ufuatiliaji wa migogoro cha Acled.

Wanajeshi wamekubali hasara katika uwanja wa vita, lakini hawakutoa maelezo yoyote. Familia ilijaribu kwa siku mbili kuuchukua mwili wa Min Aung lakini haikuwezekana kwa sababu askari walilinda eneo hilo.

"Sikuweza hata kuchukua mifupa yake," anasema mama yake. "Nina hasira kuhusu hilo. Nataka kwenda kupigana lakini hawatanichukua kwa sababu mimi ni mwanamke wa zaidi ya miaka 50."

'Sitakuacha wewe au mtu yeyote'

Bo Kyar Yine anaamini uasi huo maarufu utashinda na atajenga upya nyumba ya familia.

Lakini vita vya wenyewe kwa wenyewe vinapozidi, hii inaonekana kuwa ndoto mbali sana.

Wakati wanawe wawili wa kati wanakataa kuondoka jeshini familia inabaki imegawanyika, ikionyesha mgawanyiko wa taifa.

"Hatupigani na jeshi kwa sababu tunataka," Bo Kyar Yine anamwambia mwanawe mwanajeshi. "Ni kwa sababu viongozi wa mbwa wako sio waadilifu kwa hivyo inabidi tupigane. Kwa sababu yako ndugu yako alichukuliwa."

Nyi Nyi anajibu kwamba anajua kaka yake amekufa. "Njoo uangalie kijiji chako. Sasa hivi ni majivu," baba yake anamwambia kwa hasira.

"Hatukuweza hata kuhifadhi picha zako. Jinsi moyo wangu unavyoumia."

Bo Kyar Yine kisha anaonya mwanawe. "Ukifika eneo langu na kuanzisha vita, sitakuacha au mtu yeyote. Nitasimama na watu tu - siwezi kusimama na wewe," anasema, kabla ya kukata simu.

*Majina yote katika ripoti hii na maelezo ya maeneo yafichwa ili kulinda utambulisho wa watu.